Connect with us

General News

Anavyojichumia hela kama mkulima mdogo wa maua – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Anavyojichumia hela kama mkulima mdogo wa maua – Taifa Leo

UJASIRIAMALI: Anavyojichumia hela kama mkulima mdogo wa maua

NA PETER CHANGTOEK

UKUZAJI wa maua yanayouzwa ughaibuni, umekuwa ukidhaniwa na wengi kuwa, unafaa kuendeshwa tu na kampuni kubwakubwa zinazoyatumia mashamba makubwamakubwa.

Hata hivyo, kulingana na mkulima tuliyekutana naye juzi, hii ni zaraa inayoweza pia kuendeshwa hata na wakulima wanaoyatumia mashamba madogo.

Katika eneo la Sagana, Kaunti ya Nyeri, Simon Muriuki, 47, amekuwa akishughulikia ukuzaji wa maua aina ya Arabicum na Ammi, ambayo anasema yana faida mno.

Huyauza kwa kampuni ya Wilmar Flowers, iliyoko mjini Thika.

“Mimi ni mkulima kwa uamuzi, si kwa bahati. Nina fahari kuwa mmoja kati ya wakulima wanaoipatia nchi hii dola, kupitia kwa maua,” asimulia.

Hapo awali, alikuwa na changamoto kuyapata maji ya kutumia katika kilimo. Hata hivyo, shirika la Upper Tana liliwashika mkono, pamoja na wakulima wengine.

“Lilitusaidia kupata mabomba ya maji. Kwa sasa, mimi hufanya kilimo bila wasiwasi,” asema Muriuki.

Shirika hilo lilipowasaidia, ndipo kampuni ya Wilmar Flowers ilipoanza kuwapa kandarasi ya kuyakuza maua, kwa sababu maji hayakuwa tatizo tena, na hivyo wangeendesha shughuli hiyo pasi na wasiwasi.

Anadokeza kwamba, maua aina ya Arabicum huchukua muda wa miezi mitatu na nusu ili yaanze kuchumwa. Anaongeza kuwa, maua hayo huchumwa kwa muda wa mwezi mmoja na nusu au wiki sita mfululizo.

Kwa wiki moja, yeye huchuma kati ya mashina 1,000 na 2,000.Yanapokuwa tayari kuchumwa, mashina hukatwa.

Arabicum huwa na gredi tatu; ya kwanza, ya pili na ya tatu. Gredi 1 ni yale yaliyo na urefu wa sentimita 80-85, gredi 2, sentimita 75 na gredi 3, sentimita 60.

“Gredi ya juu ni sentimita 80 na ya chini ni sentimita 60,” afichua mkulima huyo, akiongeza kuwa, hulitumia shamba ekari mbili kwa kilimo.

Muriuki anasema kuwa, miezi ya Machi, Aprili na Mei, ni bora sana kwa ukuzaji wa maua, maadamu Barani Uropa, hali ya anga si shwari kwa ukuzaji wa maua kwa wakati huo, na hivyo maua yanayokuzwa nchini hupata soko kule.

Huuza shina la ua aina ya Arabicum sentimita 85 kwa Sh12, sentimita 75 kwa Sh8 na lililo na sentimita 60 kwa Sh5.

Anadokeza kuwa, hununua mbegu za Arabicum kwa Sh3,000 kwa gunia moja lililo na ndoo tano. Hupanda mbegu magunia 12 kwa shamba robo ekari, ambapo hutumia Sh36,000 kwa mbegu peke yake.Anasema kuwa, hutumia mtaji wa Sh45,000 kuyakuza maua aina ya Arabicum kwa shamba robo ekari. Baada ya kuondoa gharama ya uzalishaji, hubaki na faida ya Sh40,000.

“Nikipata mashina 10,000 na kuuza kwa Sh8 kila moja, hizo Sh80,000, na ninaweza kupata faida ya Sh40,000 kwa robo ekari,” afichua.

Kwa mujibu wa Muriuki ni kwamba, maua aina ya Ammi ni rahisi kukuza, na hayana changamoto nyingi.

“Mbegu hupandwa kama karoti. Huchukua muda wa miezi mitatu na nusu kuchumwa,” asema.

Anafichua kuwa, kwa shamba mita moja mraba, huchuma mashina kati ya 100 na 200.

Hata hivyo, bei ya aina hiyo ya maua huwa chini, ambapo yeye huuza shina moja kwa Sh4-Sh5.

Gharama ya uzalishaji wa maua aina ya Ammi huwa chini.

Muriuki huzizalisha mbegu anazozipanda kwa shamba lake. Anasema kuwa, gharama ya juu ya uzalishaji wa maua hayo kwa shamba robo ekari ni Sh15,000.

Hupata jumla ya Sh80,000 kwa shamba robo ekari, na hubaki na faida ya takriban Sh55,000.

Anasema kuwa, hakuzi mimea mingineyo, ila maua tu.

“Nina furaha kwa sababu kila mwaka, hupewa kandarasi ya kukuza,” adokeza.

Mkulima huyo ana wafanyakazi wanne – wawili wanaochuma maua shambani, na wawili wanaoyachambua.

Mfanyakazi akichambua maua yaliyochumwa. PICHA | PETER CHANGTOEK

Muriuki anaongeza kuwa, si lazima mkulima awe na shamba kubwa ili kuyakuza maua hayo.

“Hata ukiwa na shamba robo ekari unaweza,” afichua.

Anaeleza kuwa, mipango yake ya siku za usoni ni kulinunua shamba jingine, na kuyakuza maua kwa shamba ekari tano.

Aidha, anapania kulifungua duka la kuuzia maua, hususan jijini Nairobi.