Connect with us

General News

Baadhi ya wanasoka wa haiba kubwa waliowahi kuondoka katika vikosi vyao wakiwa wachezaji nguli kabla ya kurejea – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Na CHRIS ADUNGO

CRISTIANO Ronaldo ameondoka Juventus baada ya miaka mitatu na kurejea kambini mwa Manchester United miaka 11 baada ya kuagana na kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kuyoyomea Uhispania kwa rekodi ya Sh12 bilioni kuchezea Real Madrid.

Marejeo ya Ronaldo yanafanyika wiki chache baada ya fowadi wa zamani wa Man-United na Everton, Romelu Lukaku kuagana na Inter Milan ya Italia na kurudi Chelsea.

Hii hapa orodha ya wanasoka wengine wa haiba kubwa waliowahi kuondoka katika vikosi vyao wakiwa wachezaji nguli kabla ya kurejea katika maisha yao ya baadaye kitaaluma.

ROMELU LUKAKU – Chelsea

Awamu ya kwanza: 2011-2014

Awamu ya pili: 2021-hadi sasa

Aliondoka Stamford Bridge mnamo 2014 bila kupata fursa ya kuwajibikia kikosi cha kwanza cha Chelsea waliomtuma kwa mkopo kambini mwa West Bromwich Albion na Everton.

Baadhi ya wanasoka wa haiba kubwa waliowahi kuondoka katika vikosi vyao wakiwa wachezaji nguli kabla ya kurejea – Taifa Leo
Straika wa Chelsea, Romelu Lukaku wakati wa mechi dhidi ya wenyeji Arsenal. Picha/ AFP

Baada ya kupokezwa mkataba wa kudumu na Everton, alianza kumezewa mate na Chelsea kwa mara nyingine ila akahiari kutua Man-United.

Aliondoka Man-United mnamo 2019 na kutua Inter Milan aliowasaidia kutwaa taji la Serie A kwa mara ya kwanza baada ya miaka 11 mnamo 2020-21.

Ufanisi huo uliwachochea Chelsea kumhemea upya na akajiunga nao kwa rekodi ya Sh15.2 bilioni muhula huu. Katika mchuano wake wa kwanza katika awamu ya pili kambini mwa Chelsea, alifunga bao na kusaidia washikilizi hao wa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kupepeta Arsenal 2-0 ugani Emirates.

DIDIER DROGBA – Chelsea

Awamu ya kwanza: 2004-2012

Awamu ya pili: 2014-2015

Anachukuliwa kuwa miongoni mwa wavamizi bora wa muda wote kambini mwa Chelsea baada ya kusaidia kikosi hicho kunyanyua jumla ya mataji 10 katika vipute tofauti.

Nyota huyo raia wa Ivory Coast alitwaa mataji matatu ya EPL na taji moja la UEFA katika kipindi cha miaka minane ya awamu yake ya kwanza.

Baada ya miaka miwili kambini mwa Shanghai Shenhua na Galatasaray, Drogba alirejea Chelsea chini ya kocha Jose Mourinho mnamo 2014 na kusaidia kikosi hicho kunyakua taji jingine la UEFA.

THIERRY HENRY – Arsenal

Awamu ya kwanza: 1999-2007

Awamu ya pili: 2012 (kwa mkopo)

Ndiye mshambuliaji bora wa muda wote wa Arsenal. Aliagana na kikosi hicho baada ya miaka minane akijivunia kunyanyua mataji mawili ya EPL na akiwa sehemu ya kikosi kilichokamilisha kampeni za kipute hicho mnamo 2003-04 bila kupoteza hata mechi moja.

Alisajiliwa na Barcelona mnamo 2007 kabla ya kuhamia Amerika kuvalia jezi za New York Red Bulls mnamo 2010.

Mnamo 2012, Henry alirejea uwanjani Emirates kwa mkopo wa miezi miwili ili kujaza mapengo ya Marouane Chamackh na Gervinho waliokuwa wakiuguza majeraha mabaya ya muda mrefu.

Alifunga bao la ushindi dhidi ya Leeds United kwenye Kombe la FA katika mchuano wake wa kwanza katika awamu ya pili na kupachika wavuni goli jingine la ushindi wa 2-1 dhidi ya Sunderland na kunyanyua Kombe la FA.

ROBBIE FOWLER – Liverpool

Awamu ya kwanza: 1993-2001

Awamu ya pili: 2006-2007

Alistahiwa sana na mashabiki wa Liverpool jijini Merseyside. Alivunja mioyo ya mashabiki wengi alipoagana na kikosi hicho mnamo 2001 na kujiunga na Leeds United waliojivunia huduma zake kwa miaka miwili kabla ya kutua Manchester City.

Baada ya kuachiliwa na Man-City mnamo 2006 kutokana na wepesi wa kupata majeraha mabaya, Fowler alirejea Liverpool na kufungia kikosi hicho mabao 12, yakiwemo manane katika EPL.

GARETH BALE – Tottenham

Awamu ya kwanza: 2007-2013

Awamu ya pili: 2020-2021 (kwa mkopo)

Alijijengea jina katika awamu ya kwanza kambini mwa Spurs kabla ya kuweka rekodi ya kuwa mchezaji ghali zaidi duniani alipojiunga na Real Madrid mnamo 2013.

Baada ya kujivunia mafanikio makubwa kambini mwa Real, nyota huyo raia wa Wales aliwekwa pembeni na kocha raia wa Ufaransa, Zinedine Zidane aliyemtuma kwa mkopo kambini mwa Spurs mnamo 2020.

Licha ya kutoridhisha sana katika kampeni za Wales kwenye Euro 2020, Bale anajitahidi kufufu makali yake kambini mwa Real chini ya kocha Carlo Ancelotti aliyerejea ugani Santiago Bernabeu mwishoni mwa msimu wa 2020-21 baada ya kuagana na Everton.

WAYNE ROONEY – Everton

Awamu ya kwanza: 2002-2004

Awamu ya pili: 2017-18

Umaarufu ulianza kumwandama mnamo 2002 baada ya kufungia Everton bao la ushindi dhidi ya Arsenal katika EPL na kusajiliwa na Man-United muda mfupi baadaye.

Nyota huyo ambaye ni mfungaji bora wa muda wote katika timu ya taifa ya Uingereza alijivunia kipindi cha miaka 13 ya kuridhisha ugani Old Trafford. Akiwa huko, alinyanyua mataji matano ya EPL na moja la UEFA kabla ya kurejea Everton. Katika kipindi cha msimu mmoja pekee ugani Goodison Park, Rooney aliibuka mfungaji bora wa Everton na akaagana tena na kikosi hicho mnamo 2018 ili kujiunga na DC United ya Amerika inayoshiriki Major League Soccer (MLS).

SOL CAMPBELL – Arsenal

Awamu ya kwanza: 2001-2006

Awamu ya pili: 2010

Aligonga vichwa vya habari na kuchemsha hasira za mashabiki wa Tottenham alipoagana na kikosi hicho cha London Kaskazini na kutua Arsenal mnamo 2001 bila ada yoyote.

Baada ya miaka mitano kambini mwa Arsenal, beki huyo wa zamani wa Uingereza aliyoyomea Portsmouth waliomdumisha kwa miaka mitatu kabla ya kuhamia Notts County.

Alisajiliwa upya na kocha Arsene Wenger mnamo 2009-10 na akahudumu ugani Emirates kwa msimu mmoja kabla ya kuhamia Newcastle United waliomtegemea hadi alipostaafu rasmi.

PAUL POGBA – Man Utd

Awamu ya kwanza: 2009-2012

Awamu ya pili: 2016-hadi sasa

Alichezea kikosi cha kwanza cha Man-United mara saba pekee kabla ya kujiunga na Juventus ya Italia akiwa na umri wa miaka 19. Akiwa Italia, alijikuza zaidi kitaaluma na kuibuka kuwa miongoni mwa viungo bora zaidi duniani.

Mnamo 2016, Man-United waliweka mezani kima cha Sh12.4 bilioni ili kujinasia upya maarifa ya sogora huyo raia wa Ufaransa. Japo makali yake yalididimia katika misimu ya kwanza ya awamu yake ya pili ugani Old Trafford, nyota huyo kwa sasa ameimarika pakubwa na amekuwa akihusishwa na uwezekano mkubwa wa kurejea Juventus au kutua Real Madrid.

JERMAIN DEFOE – Tottenham

Awamu ya kwanza: 2004-2008

Awamu ya pili: 2009-2014

Katika msimu wake wa kwanza kambini mwa Spurs ambao walimsajili kutoka West Ham United, Defoe alikuwa fowadi wembe aliyetegemewa pakubwa na timu ya taifa ya Uingereza.

Mnamo 2008, aliagana na Spurs na kuhamia Portsmouth waliokuwa wakinolewa na kocha Harry Redknapp.

Baada ya msimu mmoja kambini mwa Portsmouth, Redknapp aliajiriwa na Spurs na akahiari kumrejesha Defoe kambini mwa kikosi hicho.

Sogora huyo alihudumu Spurs kwa miaka mingine mitano ambapo alipachika wavuni mabao 79 na kukamilisha kipindi chake cha usogora kambini mwa kikosi hicho akishikilia nafasi ya sita kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote.

JUNINHO – Middlesbrough

Awamu ya kwanza: 1995-1997

Awamu ya pili: 1999-2000 (kwa mkopo)

Awamu ya tatu: 2002-2004

Nyota huyo raia wa Brazil alipenda kikosi cha Middlesbrough kiasi cha kukichezea katika vipindi vitatu tofauti. Alisaidia Middlesbrough kutinga fainali ya Kombe la FA na League Cup mnamo 1997. Hata hivyo, aliyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Atletico Madrid baada ya Middlesbrough kuteremshwa ngazi mwishoni mwa msimu wa 1997 kwenye EPL.

Alirejea Middlesbrough kwa mkopo mnamo 1999-2000 kabla ya makali yake kushuka kutokana na majeraha mabaya ya mara kwa mara.

Hata hivyo, alipokezwa tena mkataba wa kudumu na kikosi hicho mnamo 2002 na akakisaidia kutwaa taji la League Cup mnamo 2004 na kufuzu kwa soka ya bara Ulaya.

NEMANJA MATIC – Chelsea

Awamu ya kwanza: 2009-2011

Awamu ya pili: 2014-2017

Chelsea walimsajili kiungo huyo raia wa Serbia kwa Sh234 milioni pekee mnamo 2009. Hata hivyo, aliwajibishwa katika kikosi cha kwanza mara tatu pekee kabla ya kutumwa kambini mwa Vitesse Arnhem kwa mkopo kisha akapokezwa mkataba wa kudumu na Benfica ya Ureno.

Baada ya kuhudumu Benfica kwa miaka mitatu, Chelsea waliweka mezani Sh3.3 bilioni na kumsajili Matic upya.

Katika awamu yake ya pili, alisaidia Chelsea kutia kapuni mataji mawili ya EPL kabla ya Man-United kumsajili kwa Sh6.4 bilioni mnamo 2017.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending