TAHARIRI: Bajeti mwaka huu isaidie kukwamua Wakenya kiuchumi
NA MHARIRI
WAKENYA leo wanasubiri kwa hamu na ghamu kufuatilia yaliyomo kwenye Bajeti ya Mwaka wa Kifedha wa 2022/23 ambayo ni ya mwisho kwa utawala wa Jubilee tangu uingie mamlakani mnamo 2013.
Bajeti hiyo itakuwa ikosomwa kwenye kikao cha pamoja cha mabunge ya Seneti na lile la Kitaifa na Waziri wa Fedha Balozi Ukur Yatani kuanzia saa nane mchana.
Bw Yatani atakuwa akisoma makadirio hayo ambayo ni ya Sh3.2 trilioni ikilinganishwa na ya mwaka huu unaokamilika wa kifedha ambao ulikuwa Sh3.3 trilioni.
Kinyuma na miaka iliyopita ambapo mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yamekuwa yakiwasilisha bajeti yao siku moja mwezi Juni, mara hii Kenya itakuwa ikisoma bajeti yake mapema kwa kuwa taifa litakuwa likifanya uchaguzi mkuu mnamo Agosti 9, 2022.
Hasa bajeti hiyo inatarajiwa itatoa fedha ambazo zitagharimia miradi mbalimbali ya serikali na pia kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) ili iimarishe maandalizi yake kwa kura hiyo.
Wakati bajeti hiyo itakuwa ikisomwa, ni vyema kutambua kuwa huu ni msimu mgumu zaidi kiuchumi huku pia taifa likiwa limezingirwa na madeni tele.
Kiwango cha mzigo wa deni la taifa sasa kimefikia Sh8.2 trilioni.Hii ina maana kuwa kiasi kikubwa cha fedha kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023 kitaelekezwa kulipa madeni hasa yale ambayo yamekopwa wakati wa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake Dkt William Ruto.
Bajeti hiyo pia inasomwa wakati ambapo kiwango cha umaskini nchini kimepanda huku ikikadiriwa kuwa asilimia 65 ya Wakenya hawawezi kujikimu vyema maishani kwa sababu wamelemewa na umaskini.
Aidha hali ni tete nchini kutokana na kupanda kwa bei ya vyakula, saruji pamoja na mafuta ambayo uhaba wake unaendelea kushuhudiwa hata baada ya serikali kulipa kampuni zinazowasilisha bidhaa hiyo Sh13 bilioni.
Hii ni licha ya kampuni hizo kusisitiza zinaidai serikali Sh32 bilioni.Ingawa serikali ilipunguza bei ya mbolea hadi nusu, inasubiriwa kuonekana iwapo hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama ya kilimo hasa baada ya Waziri wa Kilimo Peter Munya kutangaza kuwa ni wakulima waliosajiliwa pekee ndio watanufaika.
Mazingira ya sasa ya kisiasa pia yataamua jinsi ambavyo bajeti hiyo itatekelezwa kwa kuwa atakayerithi Urais baada ya uchaguzi mkuu ndiye atatimiza yote yaliyomo.
Kwa hivyo, Wakenya wanafaa watumie hekima yao kumchagua kiongozi ambaye atawakwamua kutokana ugumu wa maisha unaoshuhudiwa sasa na kubuni nafasi za ajira kuokoa hali.
Next article
TUSIJE TUKASAHAU: Mswada unaolenga kupunguza ushuru kwa…