Balala imani tele atasalia serikalini
NA KENNEDY KIMANTHI
WAZIRI wa Utalii, Bw Najib Balala, amesisitiza atakuwa ndani ya serikali itakayoundwa baada ya uchaguzi wa Agosti, ingawa amezidi kuacha wengi wakibahatisha kuhusu upande wa kisiasa atakaoegemea.
Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Bw Balala alisema kwa sasa bado ana majukumu ya kutekeleza katika wizara anayosimamia na anaamini ataendelea kutumikia wananchi hata baada ya serikali mpya kuchaguliwa.
Waziri huyo ni mmoja wa wale waliotarajiwa na wengi kujiuzulu ili kushindania nyadhifa za kisiasa kwa vile wamewahi kuwa viongozi wa kisiasa miaka iliyopita, lakini wakakwamilia serikalini.
Wengine ambao hawakujiuzulu ni Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe, mwenzake wa Ulinzi, Bw Eugene Wamalwa, Bw Ukur Yatani wa Wizara ya Fedha, na Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya.
“Wakati mwingine siasa nyingi kupita kiasi hufunika mafanikio yako. Isitoshe, watu huwa hawali siasa. Wakati mwingine inahitajika uchukue muda kuwaza na kusubiri yatakayojiri.
Nitatumikia wadhifa wangu wa sasa hadi mwishoni mwa uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta,” akasema Bw Balala.
Waziri huyo huhusishwa sana na siasa za Pwani kutokana na mchango wake wa miaka mingi katika masuala ya uongozi wa ukanda huo.
Licha ya kuwa Bw Balala hajashikilia kiti chochote cha uongozi wa kisiasa kwa vipindi vitatu vya chaguzi zilizopita, amekuwa akifanikiwa kupata nyadhifa za uwaziii serikalini kwa muda huo wote.
Hata hivyo, huku mawaziri wenzake wakijitokeza wazi kuonyesha pande za kisiasa wanazoegemea hasa kati ya Muungano wa Azimio la Umoja na Kenya Kwanza, mbunge huyo wa zamani wa Mvita hajaonyesha upande anaoegemea.
“Hakuna mtu atakayekuwa katika upinzani. Huko kuna upweke na hata wale wanaoshindania viti vya kisiasa wanafahamu hivyo. Nimekuwa katika utumishi wa umma tangu mwaka wa 1998 na nitakuwa ndani ya serikali ijayo kutumikia katika wadhifa wowote ule utakaokuwepo kwa manufaa ya Wakenya,” akasema.
Bw Balala alijizolea umaarufu wakati alipohudumu kama Meya wa Mombasa katika mwaka wa 1998 hadi 1999.
Alikuwa mbunge wa Mvita kuanzia mwaka wa 2002 hadi 2013, ambapo alipewa uwaziri katika wizara mbalimbali ikiwemo michezo, turathi za kitaifa na utalii.
Uhusiano wake na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, ulianza kuyumba baadaye alipodaiwa kuwa na misimamo inayotofautiana na ya chama hicho.
Katika mwaka wa 2012, aliamua kuungana na Rais Kenyatta, Naibu Rais William Ruto na Gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu kuunga Muungano wa Jubilee. Alifanya hivyo kupitia chama chake cha Republican Congress.
Ni kupitia kwa chama hicho ambapo aliwania useneta Mombasa lakini akashindwa na Bw Hassan Omar, ambaye wakati huo alikuwa mwanachama wa ODM. Alifanikiwa kuwa ndani ya baraza la mawaziri baada ya uchaguzi wa 2013 hadi sasa, na kuibuka kuwa mwanasiasa pekee wa Pwani katika baraza hilo.