TAHARIRI: Bila kukuza soka yetu tusahau nafasi za bara Ulaya
NA KITENGO CHA UHARIRI
Katika siku za hivi majuzi, idadi kubwa ya Wakenya wamekuwa wakisajiliwa na timu za bara Ulaya zenye hadhi ya wastani.
Kijana Mkenya wa majuzi zaidi kusajiliwa na klabu ya kigeni ni chipukizi beki Frank Odhiambo ambaye amesainiwa na Djugardens ya Sweden kwa kandarasi ya miaka mitano.
Odhiambo anaungana na kikoa kingine cha vijana machachari wa Kenya wanaozumbua riziki ya maana ughaibuni, wanaojumuisha straika nambari moja wa Kenya, Michael Olunga aliye kule Qatar, Eric Otieno na Henry Meja walio Sweden, beki wa kutegemewa Joseph Okumu anayesakatia klabu ya Gent ya Ubelgiji, Erick Johana wa Sweden na Ayub Timbe (Thailand).
Kinadada nao hawajaachwa nyuma kwani kunao Mwanahalima Adam anayefanya vitu vyake huko Uturuki, Dorcas Shikobe anayepiga soka ya kulipwa nchini Cyprus na Esse Akida anayedunda boli na klabu ya PAOK ya Ugiriki.
Naam, licha ya mafanikio kama hayo, Kenya bado haijafikia upeo wake katika kupeleka talanta zake za kabumbu, na hata za michezo mingine, katika mataifa hayo ya ughaibuni.
Tangu ulimwengu kuumbwa, Kenya imewahi kujivunia mchezaji mmoja pekee katika Ligi Kuu ya Uingereza, ambayo ndiyo maarufu zaidi duniani. Mchezaji huyo si mwingine isipokuwa Victor Wanyama ambaye kwa sasa anasakatia Montreal Impact ya Canada baada ya kupigia Tottenham Hotspur na Southampton kwa zaidi ya miaka mitano kwa jumla.
Ripoti zinasema mwanasoka huyo alikuwa akilipwa takribani Sh40 milioni kwa mwezi wakati akiondoka klabu hiyo ya Uingereza.
Wachezaji wengine waliowahi kujaribu zaidi ni kaka yake Wanyama, McDonald Mariga aliyesajiliwa na Inter Milan ya Italia ambapo pia alivuna hela nzito na Dennis Oliech aliyechezea timu kadhaa za Ufaransa. Timbe na Olunga wamewahi kusajiliwa kwa muda mfupi na klabu za Uingereza na Uhispania.
Unapolinganisha wanasoka wetu wanaochezea klabu za nguvu barani Ulaya na mataifa mengine ya bara Afrika, unagundua kuwa taifa hili lingali nyuma zaidi. Mataifa kama vile Nigeria yana zaidi ya wachezaji 100 barani Ulaya.
Tatizo letu ni lipi? Viwango vya soka yetu viko chini. Kwa hivyo, suluhu ni kuhakikisha tumeweka mikakati kabambe ya kuinua hadhi yetu ya michezo. Vinginevyo tutasalia kutapatapa tu.
Next article
Wabunge kujadidli kero la watu kuuawa na miili yao kutupwa…