Black Mamba kutifua kivumbi kipute cha Afrika
Na JOHN KIMWERE
TIMU ya wanaume ya handiboli ya Black Mamba imepania kupambana kijasho kwenye mechi za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (ECAHF), mwishoni mwa mwezi huu.
Ngarambe hiyo itakayoandaliwa mjini Dar es Salaam,Tanzania, itaanza Novemba 28 hadi Desemba 5.Kikosi hicho cha kocha Martin Abunde kinashiriki baada ya makala ya mwaka jana kufutiliwa mbali kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona.
Kwenye mechi za kukunja kampeni za Ligi Kuu ya Kitaifa ya Handiboli (NHL) nchini muhula huu, Black Mamba ilizaba Ulinzi kwa mabao 31-30. Paul Ondara na Martin Nguli wa Mamba waliibuka wafungaji bora wakitikisa wavu mara tisa na tano, mtawalia.
Kwa upande wa Ulinzi, Musa Munyasia na Noah Cheruiyot walicheka na nyavu mara saba na tano mtawalia.“Tunajiandaa vilivyo kushiriki ngarambe za mwaka huu. Tutajituma kiume dhidi ya wapinzani ili kuwalambisha sakafu na kubeba kombe,” alisema kocha Abunde.
Aliongeza kuwa wanafahamu bayana mechi hizo hazitakuwa rahisi, lakini akasisitiza kuwa kamwe hana hofu kwani masogora wake wamekaa vizuri kukabili yeyote.Kocha huyo alikiri mechi za ligi zimewanoa vilivyo wachezaji wake tayari kwa kibarua hicho jijini Dar.
Timu nne; mbili za wanaume na mbili za wanawake – zimethibitisha kushiriki makala hayo ya ECAHF. Wanaume kuna Black Mamba na NCPB nao wanawake wanawakilishwa na Nairobi Water Queens na NCPB. “Bila shaka hatutakuwa na la ziada ila kujikaza kwa udi na uvumba kutetea taji hilo, ambalo tumebeba mara tatu mfululizo,’’ kocha wa Nairobi Water, Jack Ochieng, alihoji na kuongeza kuwa wanatarajia ushindani mkali kutoka kwa mahasimu wao klabu moja ya nchini Congo.
Katika tamati ya ligi kuu Jumapili iliyopita, kwenye kitengo cha wanaume Halmashauri ya Nafaka na Mazao nchini (NCPB) ilihifadhi ubingwa wake ikizoa pointi 34.Nao wasomi wa Chuo cha Strathmore walimaliza nafasi ya pili wakitia kapuni alama 32.
Sawa na Black Mamba huku timu hizo zikitofautishwa na mabao 65 pekee.Vikosi vilivyomaliza nafasi tatu za mwisho ni Vickers, Generations na washiriki wapya Makueni Bees, iliyoburuta mkia bila alama.
Msimu uliokamilika ulijumuisha timu 19 za wanaume na nane za wanawake.Upande wa wanawake, Nairobi Water Queens ilihifadhi taji lao bila kushindwa wala kudondosha alama hata moja.Vipusa hao waliibuka kidedea kwa kusajili alama 28 wakishinda mechi zote 14.
Nao vipusa wa Ulinzi Sharks walitua nafasi ya pili kwa pointi 24, sita mbele ya NCPB. Kocha Albert Murunga wa Amazon Ladies, iliyomaliza ya mwisho kwa kuvuna alama mbili pekee, alisema: “Tunaenda kujipanga upya kwa ajili ya kinyang’anyiro cha msimu mpya maana tunahitaji kuboresha mchezo wetu.” .
Next article
Hesabu ngumu za Man-U kumleta Poch’ Old Trafford