Connect with us

General News

Dadake Raila ajiondoa kwa mbio za ugavana – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Dadake Raila ajiondoa kwa mbio za ugavana – Taifa Leo

Dadake Raila ajiondoa kwa mbio za ugavana

NA RUSHDIE OUDIA

DADAKE kiongozi wa ODM Raila Odinga Ruth Odinga amejitosa kwenye kinyang’anyiro cha kiti cha Mwakilishi wa Kike, Kaunti ya Kisumu katika uchaguzi mkuu ujao.

Awali, Bi Odinga, ambaye ni naibu gavana wa zamani wa kaunti hiyo, alikuwa ametangaza azma ya kuwania ugavana wa kaunti hiyo kabla ya kujiondoa.

Mwanasiasa huyo sasa amejitosa katika kinyang’anyiro cha kiti hicho ambacho kimevutia wawaniaji tisa.

Mshikilizi wa kiti hicho wakati huu, Rozah Buyu hajabaini ikiwa atakitetea au atapambana na Bw Olago Aluoch katika kinyang’anyiro cha kiti cha ubunge cha Kisumu Mjini Magharibi.

Wengine wanaomezea mate kiti hicho cha Mwakilishi wa Kike, Kisumu, ni aliyekuwa Waziri wa Utalii katika kaunti hiyo Rose Kisia, meneja wa jiji la Kisumu Doris Ombar na Bi Grace Akumu ambaye aliwania kiti cha ubunge cha Nyakach na kubwagwa.

Wengine ni Profesa Judith Attyang, ambaye juzi alijiuzulu kutoka wadhifa wa Waziri wa Ardhi, Kisumu, Bi Beatrice Otieno, Diwani wa Seme Central Sally Okudo na Valentine Otieno mwenye umri wa miaka 22.

Bi Odinga alitangaza azma yake Jumanne jioni wakati wa maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa. Alitoa tangazo hilo kupitia mtandao wa kijamii.

“Katika siku hii kuu ambapo nilizaliwa, naanza kuzaliwa upya. Kuzaliwa upya ili nifanye kile ambacho nafahamu vyema, kuwatumikia watu,” akasema.

“Nimeamua kuwatumikia watu wa Kisumu na nitasaka idhini yao niwahudumie kama Mwakilishi wa Kike. Ni vizuri kusikiza maoni ya watu lakini kamwe usijaribu kupuuza wito wako.” Bi Odinga akasema.

Wapinzani wake walimkaribisha katika kinyang’anyiro hicho lakini hamna aliyetangaza kujiondoa. Dkt Kisia alisema Bi Odinga ni mshindani mstahiki.

“Yeye, sawa na wengine, ni mshindani wangu. Kwa kuwa mimi ni mmoja wa wanachama waanzilishi wa ODM nitasaka tiketi ya chama hicho kuwania kiti hiki. Sitajiondoa,” akasema.

Dkt Kisia aliwania wadhifa huo katika uchaguzi mkuu wa 2013 lakini akashindwa na Bi Rose Nyamunga, ambaye sasa ni Seneta Maalum.

Kwa upande wake Bi Akumu ambaye ni kiongozi mwanzilishi wa chama cha Citizens Convention Party, alisema ni haki ya kidemokrasia ya Bi Odinga kuwania kiti hicho.

“Ni wazi kwamba sote ambao tunawania kiti hicho ni viongozi wenye uwezo na tajriba ya uongozi. Lakini wakati mwingine baadhi yetu tunaweza kufanya maamuzi yasio ya busara ambaye yatageuka kutuathiri,” akasema.

Lakini wawaniaji wengine wanahisi kuwa Bi Odinga anafaa kuwania kiti kingine wala sio hicho cha Mwakilishi wa Kike.

“Ruth amewahi kuhudumu kama naibu gavana na ana uwezo mkubwa. Mbona sasa asiwaruhusu wanawake wengine kwa kuwania viti vingine pamoja na wanaume?” mwananiaji mmoja akasema.