MWALIMU WA WIKI: Elisha Otoyi
NA CHRIS ADUNGO
MWALIMU anaweza kuwa kiini cha wanafunzi wake kufeli masomoni.
Kumwadhibu mwanafunzi kunastahili kuwa hatua ya mwisho kabisa katika juhudi za kumrekebisha.
Kumkosoa mwanafunzi anapoendelea kutoa maelezo wakati wa kujifunza ni kosa. Mwalimu mzuri atasubiri mwanafunzi amalize kutoa maelezo yake (hata kama si sahihi) ndipo amwelekeze vilivyo.
Mwalimu bora anapaswa kumsaidia mwanafunzi kuelewa wala si kukariri anachofundishwa. Asifundishe wala kuadhibu wanafunzi wakati ana hasira na awatie moyo hata wanapokosa kufaulu vyema katika mitihani na kufikia matarajio yake.
Haya ni kwa mujibu wa Bw Elisha Otoyi ambaye sasa ni Naibu Mwalimu Mkuu katika shule ya msingi ya Janeiro Junior Academy, Kaunti ya Homabay.
“Usidhani kwamba kuogopwa na wanafunzi ni sifa au jambo litakalowafanya wafaulu katika somo lako. Mwanafunzi akimchukia mwalimu, basi atachukia pia somo lake na mwishowe hatafaulu,” anasema.
Otoyi alizaliwa mnamo 1983 katika kijiji cha Kambata, eneo la Karachuonyo Magharibi, Kaunti ya Homabay. Alianza safari ya elimu katika chekechea ya Shauri Yako, Homa Bay (1986–1988) kabla ya kujiunga na shule ya msingi ya Shauri Yako (1989–1996).
Alisomea baadaye katika shule ya upili ya Gogo Mixed, Karachuonyo (1997-1999) kisha Asego Academy, Homa Bay (2000) kabla ya kujitosa katika biashara ya kuuza vibanzi mjini Homa Bay.
Ilikuwa hadi 2011 alipozidiwa na kiu ya ualimu na akapata fursa ya kufundisha Kiswahili katika shule ya Shanzu Preparatory, Mombasa kabla ya kuhamia Visual Junior Academy, Kilifi (2012-2013). Alirejea Homabay mnamo 2014 na akawa mwalimu katika shule ya msingi ya M.A Mbita Academy, Homabay.
Akiwa huko, alisomea taaluma ya ualimu katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Migori (2016–2018) na akaajiriwa na shule ya Janeiro Junior Academy mnamo 2019. Alijiendeleza kitaaluma kwa kusomea stashahada ya elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Kenya Institute of Special Education (KISE), Migori kati ya 2019 na 2021.
Anakiri kuwa alama nzuri zilizozolewa na watahiniwa wa Janeiro Junior Academy katika KCPE 2021 ni zao la juhudi zake kutenga Jumatano na Ijumaa kuwa ‘Siku za Kiswahili’ shuleni pamoja kuwashirikisha wanafunzi katika mijadala na usomaji wa mara kwa mara wa gazeti la ‘Taifa Leo’.
Zaidi ya ualimu, Otoyi pia ni mshairi shupavu na mwandishi stadi wa vitabu vya Kiswahili. Baadhi ya hadithi ambazo amechangia vitabuni ni ‘Haidhuru’ katika antholojia ‘Mateka na Hadithi Nyingine’ na ‘Siri Kali ya Serikali’ katika ‘Mali ya Mama na Hadithi Nyingine’.
Amechangia pia idadi kubwa ya mashairi katika diwani ‘Malenga wa Kenya’, ‘Wosia na Mashairi Mengine’, ‘Wasifu wa Timothy Omusikoyo Sumba’ na ‘Malenga wa Afrika’. Baadhi ya mashairi yake vilevile huchapishwa katika ‘Taifa Leo’ chini ya lakabu ‘Isah Bin Omar’ au ‘Malenga wa Wanyonge’.
Ari ya kuchangia makuzi ya Kiswahili ilimpa Otoyi msukumo wa kushirikiana na Bw Sumba, Bw Henry Momanyi na Bw Alfred Lobawoi kuasisi kundi la ‘Malenga Wamilisi’ mnamo Februari 2021.
Kundi hili linalojivunia zaidi ya wanachama 100 linalenga kukuza vipaji vya waandishi chipukizi na kuwanoa zaidi watunzi waliobobea. Linaazimia pia kutunga miswada ya diwani za ushairi, hadithi fupi, riwaya na tamthilia pamoja na kuandika vitabu vya kiada, kushiriki mijadala ya kitaaluma katika vyombo vya habari na kuchangia makala katika majarida ya kitaifa na kimataifa.
Kwa pamoja na mkewe Bi Eunice Akinyi, mwalimu Otoyi amejaliwa watoto wanne – Andrew Arshavin, Trazy Evelyne, Aaron Ramsey na Melvonejoy.
Next article
Barcelona waponda Real Madrid katika gozi la El Clasico