Familia kadhaa zakosa miili ya jamaa zao Yala
NA KASSIM ADINASI
FAMILIA nyingi zilizokuwa na matumaini ya kupata miili ya wapendwa wao kutokana na uchunguzi wa DNA uliofanyika katika hospitali ya Yala, zimepata mshtuko baada ya matokeo kuonyesha jamaa zao si miongoni mwa watu ambao miili ilipatikana Mto Yala.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Gem, Bw Charles Chacha, kati ya sampuli zilizokusanywa kwa uchunguzi, ni watu 11 ambao matokeo ya DNA yalioana na za familia zao.
“Hadi sasa kuna miili 11 ambayo imetambuliwa na kuzikwa. Kuna miili mingine 16 ambayo matokeo yao hayawiani na sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa familia za kufanyiwa DNA,” akasema Bw Chacha.
Aliongeza: “Kuna familia nyingine ambazo bado zinakuja na tunachukua sampuli zao ili kufanyia vipimo. Idadi ya miili ambayo imeondolewa mto Yala sasa ni 27, japo kuna familia ambazo bado hazijatambua maiti za wapendwa wao.” Afisa huyo alishutumu vyombo vya habari kwa kueneza habari zisizo za kweli kuhusu idadi ya miili ambazo zimepatikana mtoni humo.
“Kwanini baadhi ya wanahabari wanataja nambari ambayo si sahihi. Miili yote ambayo iliondolewa mtoni Yala ni 27; na ni 11 ambayo familia zao zimetambuliwa kisha kuzikwa.
“Maafisa wa polisi hawajazika mtu. Isitoshe, kuna familia ambazo bado zinakuja kusaka wapendwa wao. Hata leo (jana) kuna familia mbili zilizofika kituoni na sampuli ya damu zao ikachukuliwa ili kufanyiwa uchunguzi wa DNA,” alihoji Bw Chacha.
Mnamo Januari 14 kulizuka taarifa kwamba kuna miili imekuwa ikilea mto Yala baada ya kutupwa huko na watu wasiojulikana.
Miili 24 ilifikishwa kwenye hifadhi ya maiti katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Yala baada ya kutolewa mtoni humo.
Kwa mujibu wa mpiga mbizi kutoka eneo hilo Okero Okite, miili hiyo ilipatikana baada ya kutupwa kutoka nyanda za juu za mto huo.
“Baadhi ya miili ilitupwa nyanda za juu huku mingine ikisafirishwa na kub – wagwa mtoni na magari mawili karibu na ufuo. Miili mingi ilikuwa imefunikwa kichwani kwa mifuko ya plastiki na mikono kufungwa,” akaeleza Bw Okite ambaye alishirikiana na polisi kuiondoa miili hiyo.
Awali polisi waliahidi kuendesha uchunguzi wa kina kwa ushirikiano na na familia ambazo wapendwa wao walipatikana mtoni, ili kubaini kiini cha tukio hilo la kihayawani.
“Tutahakikisha kuwa familia za watu ambao miili yao ilitupwa mtoni zinapata haki,” akasema Msemaji wa Polisi, Bw Bruno Shioso, alipozuru chumba cha kuhifadhia maiti cha Yala.
Miili mingi ilikuwa katika hali mbaya na haingeweza kutambuliwa bila uchunguzi wa DNA.
“Baadhi ya miili ilikuwa imeanza kuoza; mingine imebaki mifupa na fuvu pekee. Njia ya kuitambua ni kupitia DNA pekee,” akasema Afisa Mkuu wa Serika – li wa Uchunguzi wa Maiti, Dkt Johansen Oduor, alipoongoza shughuli ya kufanyia miili husika upasuaji ili kufanikisha uchunguzi.
Next article
Vigogo wa kizazi kipya wadhibiti Pwani kisiasa