Familia yafurahia Krismasi baada ya miaka 32
Na KENYA NEWS AGENCY
ILIKUWA furaha tele kwa familia moja maskini katika kijiji cha Chasimba, Kaunti ya Kilifi baada ya mhisani kuitunuku zawadi ya vyakula na bidhaa nyingine wakati wa Sherehe ya Krismasi mnamo Jumamosi.
Kwa mara ya kwanza baada ya miaka 32, familia ya mama Mbodze Munga, 51 ilisherehekea Krismasi ya aina yake huku watoto wake 19 na mumewe Benson Munga Charo, 53 wakifichua kuwa wamekuwa wakila mihogo kila krismasi tangu wajaliwe mtoto wa kwanza 1986.
Hata hivyo, mhisani Benjamin Kai, ambaye ni Afisa wa Mipango ya Kiuchumi katika Kaunti ya Kilifi, mnamo Jumamosi aliipa familia hiyo msaada wa vyakula na kuwatimizia mahitaji mengine hali iliyowapa furaha nyusoni huku ikibainika wamekuwa wakipitia hali ngumu kiuchumi.
“Tangu nijifungue mtoto wangu wa kwanza mnamo 1986 hadi leo nina mtoto wangu wa 19 , tumeishi maisha magumu sana. Krisimasi zote nimekuwa nikisaka mboga na mihogo ili kuwalisha watoto wangu 19. Leo (Jumamosi) nimefurahi sana tutakuwa tukila chakula tunachokipenda,” akasema Bw Mbodze akiwa amebubujikwa na machozi ya furaha.
Mwanamke huyo alifichua kuwa hawezi kutumia njia za kisasa kupanga uzazi kwa sababu madaktari walimweleza atakuwa akiweka maisha yake hatarini kwa kuwa anaugua ugonjwa wa shinikizo la damu.
Bw Charo naye hangeweza kuficha furaha yake, akisema kuwa amepambana sana kuwapa wanawe malezi bora huku akipitia nyakati ngumu sana maishani.
“Nimefurahi sana Krismasi hii kwa sababu tumesherehekea kama watu wengine. Nimeteseka sana kwa muda wa miaka 32 nikifanya kazi za kijungu jiko au vibarua kuitafutia familia yangu chakula,” akasema Bw Charo.
Wazazi hao waliirai serikali na wahisani wawasaidie kugharimia matibabu ya mvulana wao mwenye umri wa miaka mitatu Nickson Munga ambaye anaugua ugonjwa wa macho na anafaa apokezwe matibabu spesheli katika Hospitali ya Kenyatta.
Bw Kai alimtaja Bw Mbodze kama shujaa kwa kuwapa malezi watoto 19 huku akisema kuwa amefurahia sana kusherehekea Krismasi na familia hiyo iliyolemewa na umaskini
Pia aliahidi kumlipia karo mmoja wa watoto hao aliyemaliza kidato cha nne katika Shule ya Wasichana ya St Thomas, Kilifi ila hajafanikiwa kujiendeleza kielimu kutokana na ukosefu wa karo.
“Nimefurahia sana kuwa nimefika hapa kusherehekea Krismasi na familia hii. Nitahakikisha kuwa Priscillar Munga anaendelea na masomo yake katika taasisi atakayoipenda mwakani,” akaongeza Bw Kai.
Bw Mbodze pia ana wajukuu 24 ambao pia anaishi nao nyumbani kwake Chasimba.