[ad_1]
‘Fimbo ya Malkia Elizabeth inaunganisha mataifa ya Jumuiya ya Madola’
Na GEOFFREY ANENE
WAZIRI wa Michezo Amina Mohamed alizindua Fimbo ya Malkia Elizabeth katika bustani ya Arboretum jijini Nairobi baada ya fimbo hiyo kuwasili kutoka Cameroon.
Fimbo hiyo inazuru mataifa na maeneo yote 72 yaliyokuwa chini ya utawala wa Uingereza ama kuingia michezo ya Jumuiya ya Madola kutoka Bara Afrika, Ulaya, Asia, Oceania, Caribbean na Americas.
Ziara ya fimbo hiyo kote duniani inalenga kufanya makala yajayo ya michezo ya Jumuiya ya Madola yajulikane.
Ilianzia jijini London mnamo Oktoba 7 na itasafiri siku 294 katika kila kona ya Jumuiya ya Madola.
Kuna zaidi ya wabebaji 7,500 wa fimbo hiyo ambayo safari yake itakamilikia mjini Birmingham ambako makala yajayo ya michezo wa Jumuiya ya Madola itafanyika Julai 28 hadi Agosti 8.
Rais wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) Paul Tergat alikuwa mbebaji wa fimbo hiyo hapa nchini Jumanne. Itakuwa Kenya siku tatu kabla ya kuendelea na safari. Kenya ni kituo cha nane kwa hivyo bado kuna safari ndefu kabla ya kurejeshwa nchini Uingereza wakati wa michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika kwa mara ya kwanza kabisa mwaka 1930.
“Safari ya Fimbo ya Malkia ina ujumbe muhimu kuhusu uendelevu, vijana na usawa. Ujumbe hu0 unaenda sambamba na maono yetu ya kitaifa, matumaini na uthabiti wetu. Unaleta pamoja nguvu zetu kujenga tena mataifa yetu na kufufua uchumi wetu kote katika mataifa ya Jumuiya ya Madola ambayo yameathirika na janga la virusi vya corona. Kila mtu aliyeona Fimbo ya Malkia wakati wa safari yake aliitambua kama ishara ya umoja na utofauti katika mataifa yetu ya Jumuiya ya Madola,” alisema Waziri Amina.
Wengine waliohudhuria hafla hiyo ya uzinduzi ni mwakilishi wa wanamichezo kwenye NOC-K, Humphrey Kayange. Fimbo hiyo itakuwa katika maeneo ya Ngong Hills katika kaunti ya Kajiado hapo Novemba 3.
[ad_2]
Source link