Connect with us

General News

Gavana Mutua atoa madai mazito – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Gavana Mutua atoa madai mazito – Taifa Leo

Ocampo 6: Gavana Mutua atoa madai mazito

NA SAMMY WAWERU

ORODHA ya washukiwa sita wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu 2007 walioondolewa mashtaka na Mahakama ya Kimataifa ya The Hague, ICC, ililenga kupaka tope waliotajwa, amedai gavana wa Machakos, Alfred Mutua.

Dkt Mutua alihudumu kama msemaji wa serikali, chini ya utawala wa Rais mstaafu Mwai Kibaki aliyefariki Ijumaa wiki jana.

Licha ya mahakama hiyo kuwaondolea mashtaka washukiwa kwa kukosa ushahidi wa kutosha, Mutua amesema listi iliyoandaliwa ilikuwa na ushawishi wa kisiasa.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma, ICC, Luis Moreno Ocampo alitaja Wakenya 6 kama washukiwa wakuu waliochochea ghasia za 2007/2008, wanaojumuisha Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake, William Ruto, aliyekuwa mkuu wa utumishi wa umma, Francis Muthaura, kamishna mkuu mstaafu wa polisi, Hussein Ali, aliyekuwa mbunge wa Tinderet Henry Kosgei na mtangazaji Joshua Arap Sang.

Uchaguzi wa 2007, Rais Kibaki na kiongozi wa ODM, Raila Odinga ndio walikuwa wawaniaji wakuu.

Mrengo wa Bw Raila ulipinga matokeo yaloyotangazwa na tume ya uchaguzi wakati huo, ECK.

Ni malumbano yaliyochangia ghasia kuzuka, aliyekuwa Waziri wa Sheria na Haki, Bi Martha Karua akiongoza hafla ya kuapishwa kwa Rais Kibaki.

Aidha, zaidi ya watu 1, 300 waliuawa kinnyama na maelfu kufurushwa makwao.

“Tulijua orodha ya Ocampo 6 hata kabla haijatolewa rasmi. Ilikuwa na ushawishi wa kisiasa kupaka tope watu wengine,” akasema Dkt Mutua, akifichua alikuwa mmoja wa mashahidi wa Rais Kenyatta na Bw Muthaura.

Gavana Mutua alitoa madai hayo Jumatano, kwenye mahojiano na runinga moja nchini katika mdahalo viongozi waliohudumu kwenye serikali ya Rais Kibaki wakielezea walivyotangamana na kigogo huyo akiwa mamlakani.

Mzee Kibaki alifariki akiwa na umri wa miaka 90, Dkt Mutua akisema Rais alikuwa kiongozi mchapakazi ambaye hakusahau majukumu yake kama mume na baba.

Mkewe marehemu aliaga dunia Aprili 2016.

“Mzee Kibaki alimpenda mke wake, Lucy kwa dhati. Alikuwa akitueleza na kumsifu. Udaku ulipoenezwa kuwa ana mke mwingine, alinielekeza niandae hotuba aliyosoma kuthibitisha ana mke mmoja pekee,” Dkt Mutua akasimulia.

Alifichua baada ya kustaafu wadhifa wa msemaji wa serikali kuwania ugavana Machakos, Rais Kibaki alimtuza mamilioni ya pesa kufanya kampeni.

“Aliposkia ninajitosa katika siasa, aliridhishwa na uamuzi wangu na kunipa mfuko – sanduku, uliokuwa na mamilioni ya pesa nifanye kampeni,” akadokeza.