BAHARI YA MAPENZI: Gharama ya ndoa
SIZARINA HAMISI NA BENSON MATHEKA
KUNA rafiki yangu mmoja aliniuliza inakuwaje ndoa nyingi siku hizi hazidumu.
Katika hali halisi, harakati nyingi kuhusiana na ndoa mara nyingi hulenga zaidi harusi, gharama za mwonekano, kufurahisha ndugu, jamaa na marafiki kwa chakula kizuri na vinywaji vya kutosha na wengi husahau lengo kubwa la muunganiko huo ambalo ni maisha ya ndoa baada ya harusi.
Wengi wanaoamua kuingia katika ndoa, hawako tayari kulipa gharama halisi ya kumpata mpenzi sahihi. Na hapa haimaanishi pesa.
Gharama ambayo wengi wanashindwa kuilipa ili kupata mpenzi sahihi sio ya fedha au mali ila mchakato kamili wa kumpata mpenzi sahihi.
Baadhi ya wanaume wa siku hizi wakishapata kipato kidogo na kujiona wanamudu gharama za maisha, wanadhani kwamba wako tayari kuwa na mke na kuanza maisha ya ndoa.
Kwa mtizamo huu, ndipo unapata kijana akishughulika kusaka mwanamke atakayemkubali na kumvutia bila kuangalia mambo mengine ya msingi.
Wengine wataangalia sura, maumbile na hata kipato bila kuangalia mengine yanayohusu uhusiano wa ndoa ikiwemo tabia na mwenendo.
Msisimko halisi ndani ya ndoa unachangiwa zaidi na tabia, mwenendo, kuelewana, kutambuana kuliko pesa, sura ama maumbile.
Hivyo iwapo unakimbilia sura na umbile na usiangalie tabia, ni dhahiri haufahamu umuhimu na thamani ya ndoa.Hii haimaanini kwamba mtu aoe ama aolewe na asiyemvutia. Ni muhimu kuwa na mtu anayekuvutia na ambaye pia unamvutia, hata hivyo sura na muonekano visichukue nafasi kubwa ukasahau thamani na ubora wa tabia ya mhusika.
Tabia, mwenendo, kuelewana na kutambuana ndio injini ya ndoa, ndivyo ambavyo vinatoa tafsiri muafaka katika maisha ya pamoja ya wanandoa.
Je, mwanamke anakuwa na fahari gani kuwa na mwanamume mrefu, mwenye misuli kama trekta la kijiji na pia kipato kikubwa iwapo anamdharau, anampiga na haoni umuhimu wa kumuheshimu.
Naye, mwanamume anakuwa na fahari gani kuwa na mwanamke mwenye umbile namba nane na mwenye kubabaisha wengi ila kahaba wa mji na hamheshimu mumewe.
Ili ndoa ilete thamani na ubora kila mmoja anatakiwa kuwa tayari kulipa gharama na thamani yake. Ni vyema kulipa gharama za mahusiano ili upate mahusiano bora na ya uhakika kuliko kubabaika na mtu.
Usije ukafikiri kwamba kumkubalia haraka mwanamke ama mwanaume ndiyo njia ya kuiwahi bahati yako. Haraka isiyo na mipango sio njia ya kuiwahi bahati bali ni njia ya uhakika ya kukimbilia mikosi na majuto makuu katika maisha yako.
Mahusiano mengi yanavunjika kwa sababu wahusika wanaingia kwa mizuka, wakiangalia zaidi masuala ya gharama, uwezo na mengineyo bila kujuana vizuri.
Labda sababu huyo mwenzake ni mtanashati na anasifiwa na wengi, unakuta binti akitongozwa na kijana huyo hata hajiulizi mara mbili, haraka tu anaingia katika mahusiano.
Baada ya miezi kadhaa anaanza kulalamika kwamba wanaume wabaya kwa sababu ameteswa na kuumizwa sana kihisia.
Maisha ya ndoa hayadumu sababu ya gharama mlizoingia ili kuweza kuishi pamoja, bali huenda zaidi ya masuala ya kipato na uchumi. Ingawa pia uchumi na kipato ni muhimu, lakini visichukue sehemu kubwa ya maamuzi ya uhalisia wa uhusiano ama ndoa.
[email protected]
KABLA ya kuingia katika ndoa, mtu anastahili kufahamu na kutambua thamani ya taasisi hii muhimu na kukubali au kuwa tayari kumudu gharama yake.
Kupata mke au mume hakutoshi kusema kuwa mtu ameingia katika ndoa na kutulia, bali ni utunzaji wa ndoa yenyewe unaoamua ikiwa anafahamu thamani yake.
Ni lazima mtu awe tayari kutia bidii kujenga ndoa yake kwa hali na mali na hii inahitaji kugharimika pakubwa. Pasipo kugharimika kwa wahusika, yaani mume na mke, ndoa haiwezi kunawiri na matunda yake ni majuto.
Ili mtu aweze kugharimika na kujenga ndoa imara na yenye furaha, ni lazima atambue thamani ya ndoa katika maisha yake na jamii kwa jumla.
Watu wasiotambua thamani ya ndoa ni wale wanaodhani kazi ya mume na mke ni kukidhiana haja zao za kimwili pekee. Watu kama hao huwa hawako tayari kujukumika inavyohitajika.
Hapa ni pale unapata mtu akisaliti mke au mumewe kwa kuwa hathamini umuhimu, mchango na kujitolea kwake kukubali kuwa wake. Mtu akithamini ndoa, hawezi kwenda kinyume na viapo vya ndoa.
Wale wasiothamini ndoa, huwa wanachokana mapema na kukwepa majukumu na uwajibikaji. Unapata mwanamume anaachia mkewe jukumu la kutunza watoto huku akiponda raha au mke anaacha kumshughulikia mumewe na kumheshimu.
Majukumu na uwajibikaji katika ndoa huwa yana gharama ghali na anayeyakwepa hajui thamani ya taasisi hii.
Kila wakati, anayethamini ndoa huwa tayari kuhakikisha usalama wa mchumba na watoto na kufanya kila awezalo kukidhi mahitaji yao.
Ndoa nyingi zinasambaratika kwa sababu wengi wanachukulia harusi kama hafla ya kawaida ya burudani bila kufahamu kwamba kuungana kwa wawili kuwa mtu na mkewe huja na mzigo wa majukumu na gharama.
Kugharimika katika ndoa sio tukio la siku moja. Gharama hii huwa inaongezeka kila siku. Hili halifai kusahaulika. Hii ndio sababu mtu akifunga ndoa huwa inasemwa amefunga pingu za maisha.
Watu wanaochukulia ndoa kuwa mzaha huwa wanajidanganya tu. Inahitaji kujipima, kujipeleleza na kukata kauli kabla ya kuamua kuoa au kuolewa.
Watu wawili wanapoingia katika ndoa kila mmoja akijua thamani yake, huwa wanasaidiana kurahisishiana mzigo.
Wawili hawa wakithaminiana, maisha huwa rahisi na yenye raha. Kuthamini ndoa kunahitaji kutupilia mbali mila na desturi kandamizi ziwe za kijamii au tabia ulizozoea.
Mume anayethamini ndoa atamchukulia mkewe kama malkia wake wa maisha, hatamchukulia kama mtumwa au chombo cha kujiridhisha. Mke anayethamini ndoa naye atamtambua na kumheshimu mumewe kama kiongozi wa familia na mshauri.
[email protected]
Next article
TUSIJE TUKASAHAU: Vijana waliojisajili kidijitali kwa…