AFCON: Guinea yakung’uta Malawi katika mechi ya Kundi B baada ya kutolewa jasho
Na MASHIRIKA
GUINEA walifungua kampeni zao za Kombe la Afrika (AFCON) kwa ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Malawi mnamo Jumatatu usiku katika mchuano wa Kundi B mjini Bafoussam, Cameroon.
Bao la pekee na la ushindi katika mchuano huo lilifumwa wavuni na Issiaga Sylla baada ya kushirikiana vilivyo na fowadi Jose Kante katika dakika ya 35.
Hata hivyo, Malawi walipoteza nafasi nyingi za wazi licha ya kumwajibisha vilivyo kipa Aly Keita aliyefanya kazi ya ziada katikati ya michuma ya Guinea na kupangua makombora mazito kutoka kwa Yamikani Chester.
Chini ya nahodha Naby Keita ambaye ni kiungo matata wa Liverpool ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Guinea kwa sasa wanajivunia alama tatu kileleni mwa Kundi B sawa na Senegal waliopepeta Zimbabwe 1-0 kupitia kwa penalti ya Sadio Mane wa Liverpool katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi B mnamo Jumatatu.
Guinea wanaoorodheshwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) katika nafasi ya 81 kimataifa, walikuwa wanafainali wa AFCON mnamo 1976 nchini Ethiopia. Mbali na Naby Keita, wanajivunia pia maarifa ya Amadou Diawara (AS Roma, Italia), Ilaix Moriba (RB Leipzig, Ujerumani) na Aguibou Camara (Olympiacos, Ugiriki).
Malawi wananogesha fainali za AFCON mwaka huu kwa mara ya kwanza tangu 2010 nchini Angola.
Guinea nusura wafunge mabao mawili ya haraka kupitia kwa Ibrahima Sory Conte na Aguibou Camara mwishoni mwa kipindi cha pili kabla ya kipa Keita kudhibiti fataki alizoelekezewa na Micium Mhone, Limbikani Mvaza na Peter Banda.
Ingawa vikosi vyote viwili vilikosa huduma za baadhi ya wanasoka wa haiba kutokana na maambukizi ya virusi vya corona, Malawi ndio walioathirika pakubwa. Waliweza kuunga kikosi cha akiba cha wanasoka wanne pekee huku wakitegemea pia idadi kubwa ya wachezaji wa timu B katika kikosi cha kwanza.
Guinea kwa sasa wanajiandaa kuvaana na wanafainali wa AFCON 2002 na 2019, Senegal huku Malawi wakipepetana na Zimbabwe katika mechi nyinginezo za Kundi B mnamo Januari 14, 2022.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO