Hatimaye Ruto apanua wilbaro
Na CHARLES WASONGA
HUKU wabunge wakirejea bungeni kesho kuamua hatima ya mswada unaopendekeza usajili wa vyama vya miungano kabla ya uchaguzi mkuu ujao, Naibu Rais William Ruto anaonekana kulegeza msimamo kuhusu pendekezo hilo.
Hii ni licha ya kwamba wabunge wandani wake wameshikilia kuwa watauangusha mswada huo unaolenga kufanikisha mipango ya kugeuza vuguvugu la Azimio la Umoja kuwa chama cha kisiasa.
Dkt Ruto amewaalika kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na Bw Moses Wetang’ula wa Ford Kenya kwa mazungumzo ya kubuni muungano kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, mwaka huu.
“Ninaendelea kuongea na Mudavadi na Wetang’ula ili tuunde serikali pamoja, kwa mapenzi ya Mungu. Na hii ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa zaidi,” Dkt Ruto akasema alipohudhuria fainali ya dimba la Malala Super Cup katika uwanja wa Mumias Complex, Kakamega Ijumaa wiki jana.
“Jambo muhimu wakati huu ni kwamba tunapaswa kufanya kazi pamoja ili tushinde uchaguzi mkuu ujao. Kwa hivyo, binafsi nitawatafuta Mudavadi na Wetang’ula ili kwa pamoja tufanye uamuzi wa mwisho,” akaongeza.
Jana, Katibu Mkuu wa chama cha Dkt Ruto, United Democratic Alliance (UDA) Veronica Maina alithibitisha kauli ya mkubwa wake.
“Kama UDA, tumewaalika rasmi Mudavadi na Weteng’ula kwa mazungumzo. Tunasubiri majibu yao. Wakikubali tutawasikiliza kwa sababu UDA ni chama cha demokrasia. Hii ni licha ya msimamo wetu wa awali kuwa yeyote anayetaka kutuunga mkono sharti ajiunge na UDA,” akanukuliwa na gazeti la Daily Nation.
Lakini akihojiwa katika runinga ya Citizen Jumanne wiki jana, Dkt Ruto alisema japo anazungumza na Bw Mudavadi, chama cha UDA kitadhamini wagombeaji kote nchini likiwemo eneo la Magharibi, ngome ya kiongozi huyo wa ANC.
“UDA ni chama cha kitaifa na kitasimamisha wagombeaji kote nchini hata kwa huyo rafiki yangu. Hatutaki hii dhana ya kwamba sehemu hii au ile ni ngome ya mtu fulani,” Dkt Ruto akasema.
Katika kampeni zake maeneo mbalimbali nchini mwaka jana, Naibu Rais alisisitiza kuwa UDA haitabuni muungano na vyama vingine kabla ya uchaguzi mkuu, akisema hatua hiyo itaipaka tope la ukabila.
“Vyama vidogo vidogo ni vyombo vinavyotumiwa na viongozi wao kijitafutia vyeo. Kwa hivyo, wale ambao wanataka kufanya kazi nasi wavunje hivyo vyama vyao vya kikabila ili wajiunge na UDA,” Dkt Ruto akasema katika mkutano wa hadhara Kaunti ya Kwale, mnamo Desemba 8, 2021.
“Miungano haitadumu ikiwa imeundwa kwa misingi ya nyadhifa ambazo viongozi watapata. Tunapinga hizi siasa za vyeo na mamlaka. Maslahi ya wananchi sharti yapewe kipaumbele,” akaongeza.
Ni msimamo huo uliomtenganisha Dkt Ruto na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri ambaye ni kiongozi wa chama cha The Service Party (TSP) na Mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria anayeongoza Chama Cha Kazi (CCK).
Wawili hao ambao wamekuwa washiriki wake wakuu kutoka eneo la Mlima Kenya wamedinda kuvunja vyama vyao.
Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanasema Naibu Rais ameamua kulegeza msimamo wake kuhusu wazo la kuunda muungano kabla ya uchaguzi baada ya kung’amua kuwa anahitaji uungwaji mkono hasa Magharibi mwa Kenya.
“Dkt Ruto anaongozwa na hitaji la kikatiba kwamba mgombeaji wa urais sharti apate angalau asilimia 25 ya kura kutoka kaunti 24 na zaidi. Hii ni mbali na kupata asilimia 50 na kura moja miongoni mwa kura zote za urais, kabla ya kutawazwa mshindi,” akasema David Monda.
“Aliwakataa akina Kiunjuri na Kuria kwa imani kwamba ataweza kupata asilimia 25 ya kura za urais kutoka kaunti za Mlima Kenya. Hana uhakika kama huu kutoka kaunti za Magharibi mwa Kenya kwa sababu mpinzani wake mkuu Raila Odinga amepenya zaidi eneo hilo.Hii ndiyo maana ‘anawatongoza’ Mudavadi na Wetang’ula ambao wana usemi wa kisiasa eneo hilo,” anaongeza Prof Monda, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Maasai Mara.
Kwa upande wake, Bw Mark Bichachi anasema Dkt Ruto anatamani kubuni muungano na viongozi hao wa Magharibi kama njia ya kuyeyusha ushawishi wa Bw Odinga eneo hilo.
“Anataka kuzima wimbi la Azimio la Umoja ambalo linavumishwa na Katibu Mkuu wa COTU, Bw Francis Atwoli, Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya miongoni wa viongozi wengine wa eneo,” akasema mdadisi huyo.
Katibu Mkuu wa Ford Kenya Chris Wamalwa jana aliambia Taifa Leo kwamba chama hicho hakina habari kwamba kiongozi wake amealikwa kwa mazungumzi na UDA.
“Nadhani hizo ni kauli zinazolenga kuwafurahi watu fulani wakati kama huu wa kampeni, kwa manufaa yao. Afisi yangu haijapokea barua yoyote kutoka kwa UDA wakati huu kuhusu suala hilo. Ford Kenya ingali katika muungano wa One Kenya Alliance na hivi karibuni tutatangaza mgombeaji wetu wa urais,” akasema Mbunge huyo wa Kiminini.
Next article
Kenya yarejelea uuzaji mifugo Oman