Connect with us

General News

Himizo haki za mifugo ziheshimiwe – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Himizo haki za mifugo ziheshimiwe – Taifa Leo

AKILIMALI: Himizo haki za mifugo ziheshimiwe

Na SAMMY WAWERU

SHIRIKA la kutetea haki za wanyama duniani limekuwa likiibua mdahalo jinsi wanyama hasa wa nyumbani wanavyofugwa.

World Animal Protection, shirika lisilo la kiserikali (NGO), kwenye mjadala wake; kuanzia malezi na matunzo, usafirishaji na uchinjaji wa mifugo, limekuwa likilalamikia wanavyohudumiwa.

Kufuatia utafiti wa 2021, linasema wafugaji na wafanyabiashara wanaendelea kukiuka haki za mifugo.

“Ni muhimu ifahamike ubora wa nyama zinazotua mezani unaambatana na jinsi mifugo wanatunzwa,” anasema Dkt Victor Yamo kutoka shirika hilo.

Dkt Yamo ambaye ni meneja wa kampeni kutetea haki za wanyama, anasisitiza mifugo wanapaswa kulishwa chakula chenye virutubisho vya kutosha na vilivoafikia ubora wa bidhaa.

Hitaji la chakula linaenda sambamba na kuwanywesha maji ya kutosha na safi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ratiba ya chanjo inatekelezwa kikamilifu.

Aidha, wanapougua mfugaji awe ange kuhakikisha wanahudumiwa na vetinari kupata matibabu.

Mifugo kufungwa kwenye pikipiki

Kando na malezi na matunzo bora, Dkt Yamo anasisitiza haja ya mifugo kusafirishwa kwa njia na vyombo vya uchukuzi inavyofaa.

“Si ajabu kuona mbuzi kadha wamefungwa kwenye pikipiki, au ng’ombe waliorundikwa kwenye lori. Ni hatia. Si haki kuwatendea unyama kama huo, wana haki kwa mujibu wa sheria za kimataifa kulinda wanyama na mifugo,” afisa huyo afafanua.

World Animal Protection imekuwa ikizua wasiwasi kuhusu haki za mifugo nchini, kutokana na utafiti uliofanywa katika vichinjio kadha Nairobi na Kiambu, kikiwemo kile cha Ndumbu-Ini, kati ya Januari na Machi 2021.

“Tulifuatilia mifugo kuanzia kwa wafugaji – wanavyolelewa, kusafirishwa na kutunzwa na kugundua wengi wanakiuka haki za wanyama,” Dkt Yamo anasema.

Wanapowasilishwa kwenye kichinjio, wanapaswa kupumzika muda usiozidi saa 18. “Wakati huo, wapewe lishe na maji,” ashauri mtaalamu huyo.

Ikiwa na makao yake makuu Rumuruti, Kaunti ya Laikipia, Ngare Narok Meat Industries Ltd inasema huruhusu mifugo kupumzika kati ya saa 24 – 48 baada ya kufikishwa kichinjioni.

“Kabla kuchinjwa, hukaguliwa kwa kina na mavetinari ili nyama zinazofikia wateja wetu ziwe salama,” adokeza Rhoda Mbogo, afisa.

Rhoda Mbogo (kulia) kutoka Ngare Narok Meat Industries Ltd na mwenzake kazini wakionyesha vipande vya nyama ambayo kampuni hiyo huuza, wakati wa maonyesho ya nyama KICC, jijini Nairobi. PICHA | SAMMY WAWERU

Kampuni hiyo ina kichinjio cha kisasa, chenye mitambo na mashine zilizoimarika pamoja na matrela yenye jokofu kusafirisha nyama Nairobi na Kiambu, wateja wakuu wakiwa hoteli, mikahawa, na wanaoagiza kwa minajili ya hafla.

Kulingana na Rhoda, uchinjaji hufanywa kwa kutumia mashine za umeme ambazo hukata shingo mara moja hivyo basi kuepushia mifugo kuhisi uchungu usiomithilika.

“Uchungu unapokuwa mwingi, huachilia homoni zinazoathiri ubora wa nyama,” aonya Dkt Yamo.

Rhoda anaiambia Akilimali kwamba baada ya mifugo kuchinjwa, huning’inizwa ili kumwaga damu na maji hatua inayolegeza misuli na kufanya nyama kuwa mwororo na tamu.

Mteja akichagua kipande cha nyama, kutoka kwa sehemu mbalimbali za viungo vya muifugo iliyochinjwa na kampuni ya Ngare Narok Meat Industries Ltd, wakati wa maonyesho ya nyama KICC, jijini Nairobi. PICHA | SAMMY WAWERU

Ngare Narok Meat Industries Ltd huuza nyama zake kulingana na viungo vya mwili, kila sehemu ikiwa na bei yake.

Mwishoni mwa mwaka uliopita, kampuni hiyo ilishiriki maonyesho ya siku mbili ya nyama, Nairobi KICC Meat Expo.