Connect with us

General News

Historia fupi kuhusu chimbuko la lugha ya Kiswahili na Waswahili – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Historia fupi kuhusu chimbuko la lugha ya Kiswahili na Waswahili – Taifa Leo

Historia fupi kuhusu chimbuko la lugha ya Kiswahili na Waswahili

NA BITUGI MATUNDURA

SI jambo rahisi kuandika kuhusu mapisi au historia ya Kiswahili na Waswahili kwa sababu ya upana wa mada yenyewe.

Hata hivyo, kuna kauli za kijumla ambazo hufumbata taswira pana kuhusu asili ya Waswahili na lugha yao, mawanda na umuhimu wa Kiswahili Afrika ya Mashariki, Afrika na janibu au sehemu nyingine duniani kote.

Kwa hivyo, chimbuko la Kiswahili, maenezi, lahaja zake, usanifishaji, sera ya lugha katika ukanda wa Afrika ya Mashariki, upanuzi wa leksikoni au msamiati wa Kiswahili ni baadhi ya vitovu vikuu ambavyo ni mseto unaoakisi historia nzima ya lugha ya Kiswahili na mustakabali wake.

Wataalamu wa lugha wamekisia idadi ya wazungumzaji wa Kiswahili kote ulimwenguni kuwa baina ya watu milioni 120 – 150. Wengi wa wazungumzaji hawa ni wenyeji wa Afrika ya Mashariki na Kati na Maeneo ya Maziwa Makuu. Ingawa Kiswahili ni lingua franka ya Afrika Mashariki, wasemaji asilia (watu wanaozungumza Kiswahili kama lugha yao ya ‘kwanza’ ni takriban kati ya milioni 5 hadi 15.

Fasihi simulizi inadokeza kwamba Waswahili walitoka sehemu za kaskazini ya pwani ya Kenya – mahali panapoitwa Shungwaya karibu na mji wa Lamu. Kutoka mahali hapa, walihamia sehemu nyingine za pwani ya Afrika Mashariki kwa sababu ya vita, njaa, magonjwa n.k.

Waswahili asilia (kindakindaki) chambacho mtaalamu Ireri Mbaabu waliitwa Wangozi na walizungumza Kingozi. Hili ni jina la lakabu lililotokana na vitendo vyao vya kupima ardhi kwa kutumia kanda za ngozi.

Jina ‘Waswahili’ ama lilitokana na ‘Wa- ziwa –hili’ (watu wa ziwa hili) au asili ya Kiarabu ‘Sahil’ (umoja) na ‘Sawahil’ (wingi) kwa maana ya watu wa pwani. Ireri Mbaabu anadai kuwa neno ‘Kiswahili’ lilianza kutumika sehemu ya kaskazini ya pwani karibu na mji wa Lamu kati ya mwaka 700 – 800 Baada ya Yesu Kristo.

Hii leo, Kiswahili si lugha ya Pwani tu. Imekwisha kupasua kingo zake na kuenea katika sehemu mbalimbali ulimwenguni – na kupanua mawanda na maana ya ‘Mswahili’, jinsi inavyofahamika.

Kwa hiyo, kuna makundi manne ya ‘Waswahili’. Kwanza, kuna Waswahili wenye asili ya Kibantu. Pili, ni Waswahili waliozaliwa kutokana na ndoa kati ya Waarabu na Waswahili asili (kindakindaki). Tatu, ni ‘Waswahili’ wanaotoka katika makabila mengine ya Kiafrika ambao wanashabikia na kuuenzi utamaduni wa Mswahili. Mwisho, kuna kundi la watu wanaoenzi na kuishughulikia lugha ya Kiswahili katika ulingo wa taaluma.

Ramani ya lugha inaonesha kuwa Kiswahili ni mojawapo ya lugha kumi na moja zenye wazungumzaji wengi zaidi barani Afrika.

Kiswahili ndicho kinashikilia nafasi ya kwanza kwa kuwa na takribani zaidi ya wazungumzaji milioni 100 barani Afrika. Lugha nyingine Afrika ni Amharic, Kioromo, pamoja na Kiarabu (Afrika Kaskazini). Katika Afrika ya Magharibi, tuna Kiyoruba na Igbo. Katika eneo la Afrika ya Kusini tuna Kizulu na Kishona.

Kati ya lugha hizi zote, Kiswahili kimeungwa mkono na wataalamu wengi kuwa lugha ya mawasiliano mapana katika bara hili. Wataalamu hao ni pamoja na Wole Soyinka, Chinua Achebe (Afrika Magharibi), Mohammed Hassan Abdulaziz, Ngugi wa Thiong’o, Ali Mazrui (Afrika Mashariki) miongoni mwa wengine.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

[email protected]