MAKALA MAALUM: Hofu chemchemi za majimoto Kaunti ya Kwale zikianza kupoa
NA SIAGO CECE
CHEMCHEMI za Mwananyamala zilizoko Dzombo, Kaunti ya Kwale, kwa miaka mingi zimekuwa na mchango mkubwa katika utamaduni wa jamii ya Wamijikenda.
Eneo hili la ekari 300 ambako wazee wa Kaya hufanya matambiko yao pia ni kivutio cha watalii kinachovutia wageni wengi.Hivi karibuni, chemchemi nne ndogo za majimoto zimepungua nguvu.
Wenyeji sasa wana wasiwasi kuwa thamani ya kitamaduni ya chemchemi hizo inafifia polepole. Kwa mujibu wa John Mutua, mkazi wa Dzombo mwenye umri wa miaka 63, maji hayo yanaonekana kupoa.
Mutua amekuwa mkazi wa eneo hili kwa miongo minne na hivyo ameona chemchemi hizi zilipoanza kubadilika kutoka kivutio cha jamii hadi kuwa kivutio cha watalii wa kimataifa.
“Tulikuwa tukileta mayai yetu na mihogo tuitokose hapa. Lakini hilo halifanyiki tena. Kwa miaka kadhaa sasa, ukiweka chakula hapo hakipikiki. Viwango vya joto vimepungua mno,” Bw Mutua alisema.
Alisema sehemu hiyo si kivutio cha watalii pekee, bali pia ni mahali patakatifu ambapo wenyeji na wazee hufanyia maombiPia, hufanyia matambiko ya kurudhisha mizimu wakati wa ukame ili kuitisha mvua.
“Wazee hasa wa Mijikenda walikuwa wakija hapa ili kuongelesha miungu. Wangeimba na kucheza na kutoa dhabihu zao huku wakichinja mnyama. Inaaminika maombi hayo maalum yalikuwa ya kulinda ardhi,” alisema.
Bi Susan Masai, mkazi mwingine alisema kuwa kubadilika kwa joto la maji kunaweza kuwa ni matokeo ya watu kwenda kinyume na imani za wenyeji na sheria zilizowekwa kwa watu wanaotembelea chemchemi hizo.
Kukiuka sheria hizi, alisema, inaweza kuwa sababu mojawapo ya Mwanyamala, ambayo pia ni kama hekalu, kupoteza thamani yake.
“Baba yangu aliniambia kuwa mwanamke yeyote ambaye alikuwa akinyonyesha au ambaye yuko kwenye hedhi hangeruhusiwa karibu na chemchemi. Yeyote anayepaka marashi na watoto wasio na meno pia hawakuruhusiwa kusogea karibu na maji. Wavulana na wanaume wadogo pekee ndio walioruhusiwa,” alisema, akiongeza kuwa mahali hapo palikuwa na ‘nguvu za kiasili’.
Kulingana naye, watu walikuwa wakichota maji kwenye chemchemi na kuyatumia kuoga ili kuponesha vidonda.
Baadhi ya wakazi wa Dzombo, Lungalunga, Kaunti ya Kwale wakijionea chemchemi mojawapo ya majimoto mnamo Januari 30, 2022. PICHA | SIAGO CECE
Wakati huu, utangamano wa makabila, dini na jamii mbalimbali katika eneo linalopakana na hapo, kulingana na Bi Masai, umefanya iwe vigumu kwa jamii kufuata mila za Wamijikenda.
“Kwa sababu tunaenda kanisani, hatuamini tena mila hizo. Maadili ya kitambo yameharibiwa na njia za kisasa. Tunaamini kwamba haya ni maji ya asili, na hivyo kuvunja kanuni za kitamaduni za Wamijikenda,” alielezea.
Katika ardhi ya chemchemi hizo, kuna sehemu yenye kichaka ya mviringo ambapo inaaminika kuwa tembo walimezwa.
Bi Masai alisema hakuna mtu anayeruhusiwa kutembea karibu na eneo hilo kwa sababu wenyeji wanaamini kuwa ‘ardhi ingewameza’ kwani inatikisika.
Wanyama wengine kama ng’ombe na mbuzi pia wanaaminika kutoweka baada ya kuingia katika eneo hilo. Sasa wafugaji hukwepa eneo hilo wanapochunga mifugo yao.
Pia kuna hekalu mbili katika eneo hilo, na wakazi wametaja moja kama mwanamume na nyingine kama mwanamke.
Ya kike ni chemchemi ya moto. Lakini wa kiume ana jiwe na mti wa mbuyu uliodumaa.
Wakazi wa eneo la Dzombo, Lungalunga, Kaunti ya Kwale wakiwa katika sehemu spesheli ya matambiko karibu na chemchemi moja ya majimoto. PICHA | SIAGO CECE
Katika madhabahu hayo, kuna ushahidi wa shughuli za matambiko kufanyika hivi majuzi, kwani kuna mabaki ya chembe za moto na chupa za kile kinachoaminika kuwa marashi yanayotumika katika matambiko.
Huku wenyeji wakitoa hofu kwamba hekalu hilo linapoteza thamani yake na huenda maji yakawa baridi hivi karibuni, mwanajiolojia, Bw Fredrick Wafula, anasema sivyo ilivyo.
Kulingana na wataalamu, chemchemi za Mwananyamala zilisababishwa na volkeno kwenye mlima mdogo wa Dzombo ambao uko karibu na chemchemi hizo.
Nguvu za volkeno kwenye ardhi katika eneo hilo bado zinaendelea kupasha joto maji.
Bw Wafula alieleza kuwa joto la maji linaweza kushuka kwa sababu ya kupungua kwa nguvu hizo za volkeno chini ya ardhi.
“Nguvu za volkeno kwa kweli zimepungua. Inamaanisha kuwa joto kidogo linatolewa na ndiyo sababu maji yanaweza yasiwe moto kama yalivyokuwa. Lakini kadiri shughuli za volkeno zinavyoongezeka, ndivyo joto na maji yanavyozidi kuwa moto,” alieleza.
Alisema hakuna ushahidi kwamba maji siku moja yatabadilika kuwa baridi. Maadamu dunia ingali inazunguka, harakati nyingi zaidi za chini ya ardhi zitatokea ambazo zitasababisha joto.
Mwanajiolojia huyo aliongeza kuwa chemichemi hizo zitabadilika mara kwa mara na maji hayawezi kuwa kwenye joto la kawaida kila wakati.
Licha ya hofu ya wenyeji kwamba maji yatapoa kabisa, serikali ya kaunti imeanza kuorodhesha maeneo yote ya vivutio vya watalii, ikiwa ni pamoja na chemchemi za Mwananyamala, na kuyaendeleza ili kunufaisha jamii zinazowakaribisha.