Connect with us

General News

Hofu ya ODM kumezwa na Azimio yaongezeka – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Hofu ya ODM kumezwa na Azimio yaongezeka – Taifa Leo

Hofu ya ODM kumezwa na Azimio yaongezeka

CHARLES WASONGA NA RUSHDIE OUDIA

HOFU imetanda miongoni mwa viongozi na wafuasi wa chama cha ODM kwamba huenda chama hicho kikamezwa baada ya vuguvugu la Azimio la Umoja kusajiliwa rasmi kuwa chama cha muungano.

Wasiwasi mkuu wa wakereketwa wa ODM ni kuwa huenda chama hicho kikapata wajumbe wachache katika Bunge la kitaifa na Seneti kwenye uchaguzi mkuu ujao, hivyo kumnyima kiongozi wake Raila Odinga nguvu ikiwa atakuwa rais.

Hii ni kutokana na mfumo unaopendekezwa wa uteuzi wa wagombeaji ambapo ODM itazimwa kudhamini wagombeaji katika ngome za vyama tanzu katika Azimio la Umoja.

Wadadisi wanasema ikiwa pendekezo hilo litaidhinishwa katika mkataba wa kuundwa kwa muungano huo, Bw Odinga atageuzwa mateka wa wabunge wa vyama tanzu endapo atashinda urais na kuunda serikali.

“Pendekezo hili la hatari kwa mustakabali wa ODM ndani ya muungano wa Azimio la Umoja. Hii ni kwa sababu wabunge wa kila chama watakuwa wakiwajibika kwa viongozi wa vyama vyao wala sio Bw Odinga kama rais,” anasema mchanganuzi masuala Mark Bichachi.

Mchanganuzi wa siasa, Salim Odeny anasema chama cha ODM kina kila sababu ya kuingiwa na wasiwasi kuhusu vyama vingine ndani ya Azimio.

“ODM wanapoendelea kueneza ujumbe wa Azimio, hawafai kusahau chama chao. Wanapasa kutia bidii kukijenga mashinani wasije wakapoteza umaarufu hasa katika ngome zao,” akadokeza Bw Odeny.

Akiongea jijini Nairobi mnamo Januari 15, Bw Odinga alidokeza kuhusu uwezekano wa mfumo huo wa vyama tanzu kutengewa maeneo kutumika wakati wa mchujo wa wagombeaji Aprili mwaka huu.

MCHUJO

“Tutakuwa na maelewano miongoni mwa vyama washirika katika Azimio wakati wa uteuzi wa wagombeaji. Kwa mfano katika ngome ya Jubilee sisi kama ODM hatutasimamisha wagombeaji wa viti mbalimbali. Kwa upande mwingine katika ngome yetu, wafuasi wa Jubilee watatuunga mkono na hawatadhamini wagombeaji,” akasema.

“Lengo letu katika Azimio ni kuhakikisha kuwa tunawafungia nje maadui wetu ili wasipate viti katika

maeneo ambako vyama vyetu vina ushawishi,” Bw Odinga akaongeza.

Kuna karibu vyama 15 ambavyo vimetangaza kuunga mkono azma ya urais ya Bw Odinga chini ya mwavuli wa wa Azimio la Umoja.

UMAARUFU MASHINANI

Miongoni mwao ni Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta, Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) kinachoongozwa na mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi, Kenya United Party (KUP) cha Gavana wa Pokot Magharibi John Lonyangapuo, United Democratic Movement (UDM) chake Gavana wa Mandera Ali Roba na Pamoja African Alliance (PAA) cha Gavana wa Kilifi Amason Kingi.

Ikiwa mfumo huo wa kila chama ndani ya muungano wa Azimio la Umoja kuachiwa maeneo ambako kina wafuasi wengi utatumiwa, ina maana kuwa ODM itapoteza viti katika Kaunti ya Kilifi ambako PAA ina mzizi na kaunti za Trans Nzoia, Bungoma na Kakamega ambako DAP-K ina ushawishi mkubwa.

Licha ya kuwa ndani ya Azimio, DAP-K kimeanza kunyemelea ngome za ODM kwa kusajili wanachama na kufungua ofisi zake, hatua ambayo imetia hofu chama cha chungwa.

Chama hicho kinajiuza kwa kauli kuwa chama cha jamii ya Waluhya na kutishia uthibiti wa ODM eneo hilo, na kimesisitiza kitakuwa na wagombeaji kwenye nyadhifa zote isipokuwa urais.

Wakati huu ODM ina wajumbe 73 katika Bunge la Kitaifa na maseneta 17 katika Seneti. Hata hivyo, baadhi ya wabunge hao wamekaidi chama hicho na sasa wanaegemea chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto.

Ni kutokana na hofu ya ODM kumezwa ambapo Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya anapinga wazo hilo na kupendekeza kuwa muafaka uzingatiwe katika uteuzi wa wagombeaji chini ya muungano wa Azimio la Umoja.

Dalili nyingine ya kumezwa kwa ODM na muungano huo ulijitokeza juzi wakati wa kampeni za kumvumisha Bw Odinga katika Kaunti ya Siaya.

Baadhi ya wabunge na wafuasi wa chama hicho walielezea wasiwasi kwamba huenda rangi yake kuu ya manjano, ikayeyushwa na rangi ya samawati ambayo ni kitambulisha cha Azimio la Umoja. Pia ilidhihirika kwamba baadhi ya wafuasi wa ODM wamesahau kauli mbiu yake ya “Chungwa Moja, Maisha Bora”.

Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo alipigwa na butwaa alipotamka “ODM” lakini umati ukajibu “Mbele Pamoja” badala ya “Chungwa Moja, Maisha Bora” “Mbele Pamoja” ni kauli mbiu ya vuguvugu la Azimio la Umoja ambalo hivi karibu litasajiliwa rasmi kuwa chama cha muungano, kulingana na hitaji la sheria mpya ya vyama vya kisiasa.