Connect with us

General News

Huduma zadorora katika hospitali za umma – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Huduma zadorora katika hospitali za umma – Taifa Leo

Huduma zadorora katika hospitali za umma

NA WAANDISHI WETU

MAELFU ya wagonjwa katika hospitali za umma nchini wanateseka kutokana na huduma duni, kukosa dawa na vifaa vya kimsingi vya matibabu.

Japo serikali za kaunti zimetumia mamilioni ya pesa kujenga hospitali za kifahari, nyingi hazina vifaa vya kazi kama nyembe, glavu, barakoa na wataalamu wa kuendesha mashini.

Uchunguzi wa Taifa Leo katika hospitali nyingi za umma kote nchini umefichua hali ya kusikitisha ya wagonjwa zaidi ya watatu kulazwa katika kitanda kimoja wakiwemo akina mama wanaojifungua.

Ingawa mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Martin Wambora analaumu Shirika la Kusambaza Dawa na Vifaa vya Matibabu (KEMSA) kwa uhaba wa dawa katika hospitali za umma, wahudumu wanalalamika kuwa, serikali za kaunti zimeshindwa kuboresha huduma hospitalini, jambo linalofanya gharama ya matibabu kuwa ghali kwa maskini.

“CoG imependekeza Kemsa ifanyiwe mabadiliko, na serikal za kaunti ziruhusiwe kununua dawa kwingine ili kuepuka kuvurugwa kwa usambazaji wa bidhaa za matibabu kwa kaunti,” akasema Bw Wambora katika taarifa.

Katika Hospitali ya Rufaa ya Nyahururu, Kaunti ya Laikipia wagonjwa hadi watatu wanatumia kitanda kimoja katika wodi.

“Wagonjwa ni wengi. Sasa hivi, binti yangu niliyemleta ajifungue wikendi iliyopita amelala kitanda kimoja na akina mama wengine watatu,” akasema Bi Lilian Mumbi.

Mhudumu wa afya katika hospitali hiyo alisema, wamekuwa wakipokea wagonjwa wengi ilhali hawana mahali pa kutosha kuwalaza.

Wakazi wamekuwa wakidai baadhi ya madaktari hupanga na wenye maduka ya kuuza dawa na wahudumu wa maabara kuwalipisha wagonjwa ada za juu za matibabu.

“Si mara moja nimeelekezwa nikapimwe na kununua dawa nje ya hospitali. Tunashangaa ni nini kilichofanyika kwa kuwa uongozi wa kaunti unazidi kushikilia kuwa huduma kama hizo zinapatikana katika vituo vya umma,” mkazi mwingine

Ingawa serikali za kaunti zimejenga hospitali za kisasa, ndani hazina vifaa vya matibabu na wagonjwa hulazimika kuvinunua kutoka maduka ya dawa

Hospitali za umma nchini hazina vifaa vya kazi kama vile nyembe, glavu, barakoa na wataalamu wa kuendesha mashini akalalama.

Hospitali katika Kaunti ya Homabay ziko katika hali mbaya, jambo linalosababisha huduma kuwa duni. Ripoti ya Kamati ya Afya ya Bunge la Kaunti hiyo inafichua uozo mkubwa katika hospitali kuu ya Rufaa ya Homabay.

“Nguo wanazotumia wagonjwa zimechakaa kwani zilinunuliwa 2018. Wagonjwa hulazwa katika vitanda vidogo ambavyo vimechanika. Kila kitanda kilichukua zaidi ya mgonjwa mmoja. Vifaa vya matibabu ni vya kitambo na madaktari wameelezea hofu yao kuhusu hali mbaya ya hospitali hiyo,” yasema ripoti ya kamati hiyo.

Kulingana na afisa wa chama cha Madaktari na Wataalamu wa Meno Kenya (KMPDU), Dkt Amos Dulo, madaktari wanapata wakati mgumu kuwahudumia wagonjwa.

“Wagonjwa hasa akina mama wanaokwenda kujifungua huambiwa wanunue maji. Vifaa vingine kama vile glavu na sirenji vimeadimika,” akasema Dkt Dulo kuhusu hali ya Homa Bay.

Kaunti ya Samburu nako hospitali za umma zinashuhudia upungufu wa vifaa muhimu vya utabibu kama vile dawa, jambo ambalo limetishia kusambaratisha shughuli za matibabu.

Vituo vilivyoathirika zaidi ni Hospitali ya Rufaa ya Samburu, inayopatikana Maralal na zahanati ya Suguta Mar Mar.

Hospitali ya Rufaa ya Samburu, ambayo ndiyo kubwa zaidi katika eneo hilo iko katika hali mbaya ya upungufu wa dawa.

Bw John Lenguroo, kibarua katika mji wa Mararal, alilalamika jinsi ilivyomlazimu kumnunulia mkewe dawa alipolazwa humo: “Mke wangu alijifungua kupitia upasuaji na nililazimika kununua dawa kutoka nje. Sijanunua dawa zote kwani huuzwa ghali katika maduka ya watu binafsi.”

Baadhi ya madaktari waliozungumza na Taifa Leo walituchorea taswira ya wagonjwa kutaabika katika wadi bila usaidizi.

Waziri wa afya wa Samburu, Bw Vincent Learaman alikubali kuwa kuna uhaba wa dawa katika hospitali za Samburu lakini akajitetea kuwa ni KEMSA ilichelewa kuwatumia dawa.

Licha ya kuwa na majengo mazuri ya kuvutia, hospitali nyingi za umma katika Kaunti ya Kisii zinatoa huduma duni.

Katika hospitali kuu ya mafunzo na rufaa ya Kisii (KTRH), baadhi ya wakazi wamekuwa wakilalamika kuwa madaktari hujikokota kuwashughulikia wagonjwa.

“Usipomjua mtu anayefanya kazi KTRH, utasubiri sana kabla ya kuhudumiwa. Dawa hazipatikani. Wagonjwa hununua dawa hizo kutoka nje,” akasema mkazi mmoja.

Hali ni sawa katika kaunti jirani ya Nyamira ambako hospitali hazina dawa za kutosha. Hospitali ya rufaa ya Hola, Kaunti ya Tana River nayo haina ICU.

Afisa wa Afya eneo hilo Javan Bonaya alikiri kuwa kaunti haina wataalamu wa ICU na kuwataka wakazi kuwa na subira, kwani itachukua muda kutatua matatizo mengi katika sekta hiyo.

“Lazima tukubali kuna matatizo ambayo bado hatujatatua, na hatuwezi kuyatatua ndani ya miaka mitatu tuliyokuwa nayo,” alisema.

Katika Kaunti za Taita Taveta, wagonjwa wanaohitaji matibabu ya oksijeni katika hospitali za umma wanahangaika baada ya mtambo wa gesi hiyo kuharibika miezi kadhaa iliyopita.

Kaunti za Kericho na Bomet, hospitali zimekumbwa na uhaba wa dawa na kusababishia wagonjwa mahangaiko makubwa.

Maduka ya kibinafsi ya kuuza dawa yanayohudumu karibu na vituo vya afya yanavuna vinono kutokana na uhaba wa dawa katika hospitali za umma.

Madaktari huwaandikia wagonjwa dawa na kuwaambia wazinunue kutoka kwa maduka ya nje.

“Ni aibu kubwa kwamba licha ya afya kugatuliwa, Bomet bado haijatilia maanani ununuzi wa dawa kutoka KEMSA,” akasema Bw Hassan Langat, mkazi wa eneobunge la Chepalungu.

Hospitali ya Rufaa ya Longisa, zile za kaunti ndogo za Tegat, Koiwo, Sigor, Ndanai, Cheptalal na Kapkoros ndizo zilizoathirika zaidi pamoja na vituo vingine vya afya katika kaunti ya Bomet.

Hospitali ya Rufaa ya Kericho, zile za kaunti ndogo za Sigowet, Kipkellion, Ainamoi, Londiani, Kapakatet miongoni mwa zingine zina upungufu mkubwa wa dawa.

Magavana Paul Chepkwony (Kericho) na Hillary Barchok (Bomet) walikiri kuwa kuna uhaba wa dawa katika hospitali zao na wakasema Kemsa ndiyo ilikuwa imechelewa kuwatumia dawa hizo.

Upungufu wa madaktari pia umesababisha baadhi ya vituo kutokuwa na mhudumu hata mmoja licha ya mamilioni ya pesa kutumiwa kujenga hospitali na zahanati katika kipindi cha miaka tisa iliyopita ya ugatuzi.

Wagonjwa wanaotafuta matibabu katika hospitali za umma mjini Nakuru hushauriwa wanunue dawa kutoka kwa vituo binafsi.

Wakazi waliohojiwa na Taifa Leo walidokeza kuwa, dawa muhimu kama zile za kuua viini, kupanga uzazi na kutuliza maumivu hazipatikani.

Hata nyembe za kufanyia upasuaji, glavu, pamba na vifaa vingineo havipatikani. Hospitali katika miji ya Naivasha, Molo, Rongai na Subukia ndizo zimeathirika mno.

Katika kaunti za Kitui na Machakos, uhaba wa dawa katika hospitali za umma umeibua manung’uniko kutoka kwa raia.

Serikali za kaunti hizo mbili zilisema matatizo haya ni kwa sababu ya utata unaoendelea katika KEMSA.

Ripoti za Benson Matheka, Steve Njuguna, George Odiwuor, Vitalis Kimutai, Eric Matara, Geofrey Ondieki, Elizabeth Ojina, Lucy Mkanyika, Pius Maundu, Stephen Oduor, Wycliffe Nyaberi na Maureen Ongala

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending