Imani potovu kikwazo kukabili kansa
MAUREEN ONGALA NA ALEX KALAMA
IMANI potovu kuhusu asili ya magonjwa imetajwa kuwa mojawapo ya vikwazo katika juhudi za kupunguza athari ya ugonjwa wa saratani katika jamii.
Wadau wa afya waliokongamana katika Kaunti ya Kilifi walibainisha kuwa jamii zinazoshikilia imani za ushirikina (kurogwa) na vilevile wanaoamini kuhusu uponyaji kupitia kwa maombi pekee katika sehemu za ibada, huwa ni vigumu kuwashawishi kwenda kutafuta matibabu hospitalini.
Kulingana na muuguzi anayesimamia kituo cha kupunguza maumivu ya wagonjwa katika Hospitali ya Kaunti ya Kilifi, Bi Lilian Said, kuna wagonjwa ambao hupatwa na saratani mapema kwa kiwango kinachoeza kutibiwa, lakini huwa hawarudi kupokea matibabu.
“Hili ni suala ambalo limetutatiza kwa muda mrefu sasa. Wanapoenda nyumbani kusema wamepatikana na saratani, jamii huwaambia wamerogwa. Baada ya kukaa muda mrefu wakijaribu kukinga uchawi bila mafanikio ndipo watarudi hospitalini na itakuwa tayari saratani ishakuwa sugu,” akaeleza.
Alitoa wito kwa serikali na wadau wengine kuongeza hamasisho kwa umma kuhusu ugonjwa huo.
Dkt Riaz Kasmani ambaye ni daktari wa saratani katika Kituo cha Matibabu ya Saratani Mombasa, alisema wanajaribu kutumia makundi mbalimbali kutatua tatizo hilo katika maeneo ya Pwani.
“Kuna watu wengi ambao huamini kuwa mtu anapougua saratani huwa
amerogwa. Sasa tunatumia wagonjwa wa saratani na wale waliopona kwa kuwapeleka mashinani kueleza jamii kuhusu ugonjwa huu. Mojawapo ya malengo yetu ni kukomesha uongo unaoenezwa kuhusu ugonjwa huu ili watu wakumbatie matibabu ya hospitalini,” akasema.
Alisema kufikia sasa, kuna makun – di aina hiyo yanayojumuisha watu kutoka Kaunti za Lamu, Tana River, Kilifi, Mombasa, Kwale na Taita-Taveta.
Msimamizi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kilifi, Dkt Eddy Nzomo, alise – ma idara ya Afya katika Kaunti inashirikiana na wadau wengine kupeleka huduma za kupima saratani kwa wakazi wa maeneo ya mashinani.
“Katika hospitali zetu na hata zile zahanati zetu ziko kule nyanjani tutapeleka huduma hizi za kupima saratani. Wagonjwa watapelekwa katika zile hospitali zilizo na vifaa vya kushughulikia magonjwa haya.
Kitengo chetu maalum kinajaribu kuhamasisha jamii kuhusu ugonjwa wa saratani ili watu waendelee kupata huu ujumbe,” akasema.
Next article
Shirika ladai kuwepo kwa jela za siri Kenya