Jenerali Badi ajikuta katika kashfa ya ardhi
Na CHARLES WASONGA
MASENETA wamemtaka Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) Luteni Jenerali Mohammed Badi afike mbele yao kujibu madai kuwa idara hiyo ilipeana ardhi ya umma kwa watu binafsi kinyume cha sheria.
Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi Moses Otieno Kajwang’ jana alisema Jenerali Badi atahitajika kufika mbele ya kamati yake kuelezea jinsi ardhi ya hospitali ya kujifungulia akina mama ya Pumwani na nyingine ya kampuni ya maji ya Nairobi mtaani Eastleigh ilipeanwa kwa watu binafsi.
Alisema kamati yake itatenga tarehe ambapo Jenerali Badi na maafisa wake watahitajika kufika mbele yao.
“Leo (jana) tumemwalika Jenerali Badi na maafisa wake wanaohusiana na masuala ya ardhi kufika hapa kujibu madai ya kwamba idara yake ilipeana ardhi ya hospitali ya Pumwani bila kufuata sheria. Amekaidi mwaliko wa kamati hii na sasa tunatoa agizo kali kwamba afike mbele yetu kujibu madai haya,” Bw Kajwang’ akasema.
Seneta huyo wa Homa Bay alikuwa ameongoza wanachama wa kamati kutembelea eneo la nyumba za wahudumu wa hospitali ya Pumwani ambalo limetwaliwa na wanyakuzi wa ardhi.
Wanachama walioandamana na Bw Kajwang’ kukagua nyumba hizo ni; Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Aaron Cheruiyot (Kericho), Agnes Kavindu Muthama (Machakos) na Seneta Maalum Millicent Omanga.
“Ikiwa madai haya ni kweli, basi Rais Uhuru Kenyatta anafaa kufahamu kwamba Luteni Jenerali Mohammed Badi anaongoza mtandao wa wahalifu ambao wanatoa ardhi ya umma jijini Nairobi kwa manufaa ya watu wachache,”akasema Bw Kajwang’.
Afisa mmoja wa cheo cha chini katika NMS aliwaambia maseneta hao kwamba Jenerali Badi hangeweza kukutana na maseneta hao katika ardhi hiyo ya hospitali ya Pumwani kwa sababu aliandamana na Rais Kenyatta katika ziara yake Dubai.
“Jenerali Badi ameonyesha waziwazi kwamba anadharau kamati hii kwa sababu afisi yake ilipokea mwaliko wetu mnamo Januari 28, kabla ya Rais kupanga safari yake ya Dubai. Ikiwa ni kweli ilikuwa lazima aandamane na Rais katika safari yake, mbona hakutuna Waziri wa Ardhi au afisa mkuu katika idara hiyo amwakilishe?” Bw Murkomen akauliza.
Baada ya kupokea malalamishi ya wakazi wa Pumwani kuhusu unyakuzi huo wa ardhi, maseneta hao walifululiza hadi katika mtaa wa Eastleigh Section 3 kukagua ardhi nyingine ambayo inadaiwa NMS ilipeana kwa watu binafsi kinyume cha sheria.
Katika eneo hilo, Bw Kajwang’ na wenzake walishuhudia jinsi ardhi ya kampuni ya Maji ya Nairobi (NCWS) ilinyakuliwa na mwekezaji kwa jina Maslah Executive Suite.
Wanachama wa kamati hiyo walisikiza shuhuda kutoka kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo kuhusu jinsi nyumba zao zilibomolewa kinyama Julai 2021 ili kutoa nafasi kwa mwekezaji huyo.
Wafanyakazi hao waliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa NCWSC Nahashon Muguna ambaye alisema juhudi zao za kukomboa ardhi hiyo zimehujumiwa na NMS.