Connect with us

General News

Jinsi magaidi watatu waliohepa jela Kamiti walivyonaswa – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Jinsi magaidi watatu waliohepa jela Kamiti walivyonaswa – Taifa Leo

Jinsi magaidi watatu waliohepa jela Kamiti walivyonaswa

Na WAANDISHI WETU

WASHUKIWA watatu wa ugaidi ambao walitoroka kutoka Gereza Kuu la Kamiti wikendi walikamatwa Alhamisi katika kijiji kimoja Kaunti ya Kitui, walipokuwa wakijitayarisha kutorokea katika Msitu wa Boni.

Watatu hao walinaswa na vikosi vya usalama saa kadhaa baada ya wenyeji kuripoti kuwaona katika Soko la Malalani, Kata ya Endau, umbali wa kilomita 100 mashariki mwa mji wa Kitui.

Walikuwa wamenunua maziwa, maji ya chupa na biskuti.

Watatu hao walionekana Jumanne katika Soko la Malalani mwendo wa saa mbili usiku, walipotokea kutoka vichaka vilivyo karibu.

Hata hivyo, walitoroka baadaye.

Tukio hilo lilizua wasiwasi katika soko hilo kwani watu wengi walidhani wafungwa hao wamejihami vikali.

Eneo hilo limekuwa likitumika kwa muda mrefu na washukiwa wa ugaidi kama maficho yao.

Nyakati za mchana, washukiwa hao walikuwa wakijificha vichakani huku wakitembea usiku ili kutogunduliwa.

Msako mkali ulianza mara moja huku wakuu wote wa idara za usalama katika eneo hilo wakiwekwa katika hali ya tahadhari.

Waliagizwa kuanza msako katika vijiji vyote vilivyo karibu ili kuwazuia kutorokea katika maeneo mengine nchini.

Duru za usalama ziliiambia ‘Taifa Leo’ kwamba kaunti hiyo yote ilikuwa imezingirwa na polisi kutoka Kitengo cha Kukabiliana na Ugaidi (ATPU).

Polisi hao walisaidiwa na Polisi wa Kukabiliana na Wizi wa Mifugo (ASTU) walio karibu na eneo la Malalani.

Kulingana na Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Kitui, Bi Leah Kithei, wafungwa hao walikamatwa katika eneo la Mwingemi walipokuwa wakijaribu kufika katika barabara ya Mwingi-Garissa kutoka Malalani.

“Ni kweli tumewakamata na wametambuliwa,” akasema Bi Kithei.

Hayo yanajiri huku walinzi watano wa Gereza la Kamiti waliokamatwa kufuatia tukio hilo wakishtakiwa na kuzuiliwa na polisi.

Mkuu wa gereza hilo, Bw Charles Mutembei, pia alishtakiwa pamoja nao katika Mahakama ya Kahawa, Kaunti ya Kiambu.

Walinzi hao ni Joseph Longorianyang’, Pamela Kiplimo, Peter Thuku, Lilian Mukasia na Nicholas Otieno.

Sita hao walipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Gigiri, Nairobi, watakakozuiliwa hadi Jumatatu, wakati mahakama itaamua ikiwa wataendelea kuzuiliwa kwa siku 30 zaidi huku uchunguzi ukiendelea au la.

Wakati huo huo, ripoti iliyozinduliwa majuzi mjini Kisumu inaonyesha kuwa kaunti za Busia, Bungoma na Kakamega katika eneo la Magharibi ndizo vitovu vipya vya ugaidi nchini.

Ripoti inasema kuwa makundi ya kigaidi kama al-Shabaab yamekuwa yakiwasajili vijana na kuwapa mafunzo yenye itikadi kali.

Maeneo mengine ni kaunti za Siaya, Nakuru, Kisumu, Vihiga, Homa Bay, Kisii, Migori na Nyamira.

Ripoti za KITAVI MUTUA, SIMON CIURI na RUSHDIE OUDIA