MAKALA MAALUM: Jinsi wakazi wa Lamu wanavyotii desturi wakiwa Ramadhani
NA KALUME KAZUNGU
MWEZI wa Ramadhani huwa wakati mgumu kwa wengi wa dini tofauti wanaosaka mahali pa kupata mlo hasa saa za mchana.
Katika kisiwa hiki ambapo dini ya Kiislamu imekita mizizi, utapata biashara nyingi, hasa zile za hoteli na mikahawa, iwe zinamilikiwa na Wailamu, Wakristo na hata wale wasiotambua dini zikisalia kufungwa mchana kutwa kipindi cha Ramadhani.
Maamuzi haya ya tangu jadi, hufanywa ili kupisha waumini wa dini ya Kiislamu kutii na kuendelea kuadhimisha saumu na masuala mengine ya kimsingi yanayofungamana na Ramadhani.
Kwa hivyo, yeyote anayeishi au kuzuru Lamu kwa mara ya kwanza, asijipata akistaajabu.
Ni vyema kufahamu kuwa ni mwiko kuonekana ukitafuna, kumenya mlo hadharani au hata kumumunya peremende waziwazi iwe ni barazani, njiani au kwenye vishoroba vya mji wa kale wa Lamu msimu huu wa Mwezi wa Ramadhani.
Taifa Leo ilizama ndani kujua ni namna gani hulka hii ilivyojiri.
Bw Abdulkadir Mau, ambaye ni kiongozi wa dini ya Kiislamu kisiwani Lamu, alieleza kuwa asili ya wakazi wote eneo hilo kutii Ramadhani kwa njia hiyo inatokana na jinsi hali ilivyokuwa miaka ya zamani, takriban 50 au 60 iliyopita.
Bw Mau ambaye pia ni mzee wa kijamii na mwanahistoria anasema ni wakati huo ambapo utawala wa Ukoloni ulikitambua kisiwa cha Lamu kuwa ngome ya Uislamu.
Kwa msingi huo, walitoa mapendekezo kwa wenyeji wote kujitahidi kuheshimu Ramadhani kwa kuhakikisha wanawapa fursa nzuri Waislamu kufunga bila ya kuwajaribu kwa vyakula vya kuuza ovyo ovyo barabarani, mahotelini au ulaji wa ovyo hadharani.
“Tangu hapo, hata baada ya Kenya kujipatia uhuru, wenyeji wa Lamu na wale wageni wanaoishi hapa wamezoea kwamba hakuna kula, kunywa wala kuuza vyakula hadharani wakati wa Ramadhani. Ni desturi ambayo kwa sasa imepokelewa vyema ni kila anayeishi au kufahamu Lamu,” akasema Bw Mau.
Mwaka huu, Ramadhani ilianza wikendi iliyopita ambapo waumini wa dini ya Kiislamu wanatakiwa kufunga kula mchana kutwa huku wakijihusisha na sala na mahitaji mengine ya kidini ikiwemo kusaidia wenzao wasiojiweza.
Bw Mohamed Abdulkadir alisema imekuwa mazoea kwa wote wanaoishi au kutembelea mji wa Lamu kukaa mchana kutwa bila kula au kunywa wakati wa Ramadhani.
Kulingana na Bw Abdulkadir, iwapo ungetaka kula, lazima uende nyumbani kwako kujitayarishia mlo kwani hoteli, mikahawa, maduka na vioski vya vyakula huwa vimefungwa.
Desturi
Anasema tangu jadi, mji wa kale wa Lamu pia umekuwa na desturi ya kipekee inayowazuia wale wanaotaka kununua vitu kama vile sigara, maji au maziwa kwa matumizi ya haraka haraka.
“Ukitaka sigara wakati huu wa Ramadhani unashurutishwa kununua boksi nzima ili ukavute nyumbani na wala si hadharani. Maji, maziwa na bidhaa nyingine pia utalazimika kununua dazani ili ukafungue na kutumia ukiwa nyumbani,” akasema Bw Abdulkadir.
Alisema desturi hiyo ipo kwa minajili ya kuvunja moyo wale wanaotaka kununua bidhaa ndogondogo na kuzitumia palepale dukani bila kuwazingatia walio kwenye saumu.
“Mambo hata hivyo hurejea kawaida punde magharibi inapowadia kwani kila mmoja huwa amefuturu,” akasema Bw Abdulkadir.
Afisa wa idara ya Turathi za Kitaifa (NMK) anayesimamia Kaunti ya Lamu, Bw Mohamed Mwenje, aliitaja hali ya watu wanaoishi kwenye mji wa kale wa Lamu kutii Ramadhani kuwa ya taadhima na inayotokana na ubinadamu au utu tu, wala sio kwamba kuna sheria rasmi kuihusu.
Bw Mwenje alisema mji wa kale wa Lamu , kiasili unatambulika kuwa na idadi kubwa ya Waislamu ikilinganishwa na madhehebu mengine yapatikanayo kisiwani humo.
Pia Lamu ni mojawapo ya vitovu vya kuenea kwa dini ya Kiislamu kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.
Bw Abdallah Shekuwe, ambaye ni mzee na pia mmiliki wa majumba ya kukodisha, anasema ili kuendeleza itikadi hiyo, wamiliki wa majengo yenye hoteli na mikahawa, pia husitisha ulishaji kodi za majumba hayo kipindi chote cha takriban siku 30 za Mwezi wa Ramadhani.
“Mimi binafsi huwa nawaambia wale waliokodi majengo yangu kwa minajili ya biashara za hoteli kwamba wasitishe biashara hizo kwanza hadi Ramadhani iishe.”
Katika kuwahimiza kufanya hivyo, huwa siitishi malipo yoyote kama kodi ya nyumba msimu wa Ramadhani,” akasema Bw Shekuwe.
Bw Mbwana Shee, mmoja wa wakongwe wa dini kisiwani Lamu alisema cha msingi kwa wale wanaositisha kufungua biashara zao au kula, kunywa na starehe nyingine wakati wa Ramadhani, hasa mchana huwa ni kwa hiari yao na wala hawalazimishwi.
Anasema wanabiashara wa kisiwa cha Lamu pia hufunga biashara zao wakati wa Ramadhani, hasa mchana, kwani wateja wao wengi ni Waislamu ambao huwa wako nyumbani wakizingatia saumu.
“Ni hiari ya mtu na pia heshima, ikizingatiwa idadi kubwa ya wanaoishi Lamu ni Waislamu. Wanaojinyima starehe kwa hiari pia hudhihirisha umoja kwa ile idadi kubwa ya wanaofunga wakati wa Ramadhani,” akasema Bw Shee.
Alieleza kuwa katika miji mingi, ikiwemo Nairobi, Nakuru, Naivasha, Kisumu na sehemu nyingine utapata biashara zikiendelea kama kawaida wakati wa Ramadhani kutokana na idadi ndogo ya Waislamu wapatikanao kwenye miji hiyo ikilinganishwa na Lamu.
Ni katika mwezi wa Ramadhani ambapo mbali na kutokula au kunywa, waumini wa kiislamu pia huhimizwa kujiepusha na maovu, kutenda mema na kuishi kwa Amani.
Waislamu pia hutumia mwezi wa Ramadhani kujikumbusha manufaa ya kujiepusha na mambo yanayokatazwa na dini kama vile hasira, kugombana, vita, kijicho, matamanio na zinaa, masimango na kusengenya na kadhalika.
Next article
Mataifa 18 yapeleka silaha vitani Ukraine