Ombaomba: Jinsi walemavu bandia walivyonaswa mjini Thika
NA LAWRENCE ONGARO
POLISI wa Thika wiki jana waliwanasa walemavu bandia ambao wamekuwa wakiomba pesa katika barabara za mji huo.
Msako huo wa wiki mbili mfululizo, ulikuwa muhimu kwa vyombo vya usalama kwa sababu walemavu hao bandia wapatao 30 walinaswa huku wakiwa na mamia ya pesa walizopokea kutoka kwa wananchi.
Idara ya watoto ya kaunti ndogo ya Thika, ikiongozwa na afisa wake Bi Linah Mwangi imekuwa ikishirikiana na polisi ili kuwaondoa barabarani kuomba pesa.
Afisa huyo alieleza kuwa wengi wa ‘walemavu’ hao ni wanawake wanaoandamana na watoto wachanga.
“Baada ya kufanya uchunguzi wetu tumegundua ya kwamba miongoni mwa walemavu hao bandia kuna baadhi wa kutoka nchi jirani ya Tanzania. Tulipowahoji zaidi walituarifu kuwa wengi wanatoka mtaa wa Kariobangi jijini Nairobi na wana kiongozi wao ambaye huwapa nauli ya kusafiri hadi mjini Thika kila siku,” alifafanua afisa huyo.
Alisema baada ya kuwahoji zaidi na kuwafanyia upekuzi baadhi yao walipatikana na pesa kati ya Sh200 na Sh1000 walizokuwa wamepokea kutoka kwa wananchi.
“Hata wengine walikiri kuwa kwa siku moja wakati wa jioni wengi hurejea nyumbani wakiwa na kati ya Sh2,000 na Sh4,000 jambo lililotushangaza,” alifafanua Bi Mwangi.
Alieleza ya kwamba baadhi ya walemavu bandia kutoka Tanzania wamekiri ya kwamba wengi wao wamekuwa hapa kwa zaidi ya miaka miwili na hata wamejenga nyumba nzuri katika nchi yao ya Tanzania kutokana na fedha hizo za kuomba.
Taifa Leo haikuthibitisha hili nchini Tanzania.
“Uombaji huo umegeuka kuwa kazi ya kawaida kwani mwishoni mwa mwezi wataweza kuchota zaidi ya Sh50,000,” akasema afisa huyo.
Afisa huyo alisema wataendelea kufanya msako huo hadi wakati watahakikisha walemavu hao bandia wanaondolewa kabisa barabarani.
Bi Sinani* kutoka nchini Tanzania ni mmoja wa walemavu bandia ambaye alisema wameajiriwa na mama mmoja kutoka Nairobi ambaye huwasafirisha mjini Thika kila siku alfajiri ili kutafuta riziki yao.
“Mimi natafutia watoto wangu wawili wadogo chakula cha kila siku. Hatuna njia nyingine ya kujikimu kimaisha,” alijitetea Bi Malonga ambaye alitembea na miguu yake miwili bila kuonyesha ulemavi wowote.
Alijitetea kuwa wazazi wake kule Tanzania walifariki na akaachwa na nyanya yake.
Naye mwanamume mmoja wa umri wa miaka 21 kutoka eneo la Donyo sabuk, Kilimambogo, Thika Mashariki, anasema shida tele ndiyo imesababisha yeye kujifanya kuwa mlemavu.
“Mimi hurauka mapema saa 10 za alfajiri ili kujitayarisha kuja mjini Thika ili kujifanya kiwete kusudi nipate pesa,” alijitetea kijana huyo.
Alieleza kuwa kwa siku moja anapokea zaidi ya Sh1,000 na ni ‘kipato’ kinachomuinua kimaisha.
Alisema iwapo ataachiliwa huru atatafuta njia ya kutafuta riziki kwa kushona viatu na pia kuuza matunda.
“Nikiachiliwa huru nitafanya juhudi kuona ya kwamba ninatafuta riziki kwa njia ya haki. Ninajua nimefanya makosa,” alijitetea kijana huyo aliyeonyesha hali ya wasiwasi usoni.