[ad_1]
MAPISHI KIKWETU: Jinsi ya kuandaa chai ya viungo ‘spiced tea’
NA MARGARET MAINA
[email protected]
CHAI ya viungo ni kinywaji kinachoweza kukuburudisha na kukutuliza msimu wa baridi au unapotaka tu kutulia nyumbani wikendi.
Chai ya viungo tofauti husaidia kwa ufya ya binadamu kwa ujumla, huongeza nguvu ya kinga ya mwili dhidi ya magonjwa, huboresha mfumo wa umeng’enyaji chakula, hupunguza maumivu, na kuongeza uwezo wa kumbukumbu. Pia husaidia kulinda moyo, kudhibiti kisukari, kuboresha ubora wa ngozi na kadhalika.
Vinavyohitajika
- Maji lita 1
- Mdalasini mzima vipande 2
- Majani ya chai kijiko cha chakula 1
- Hiliki punje 5
- Tangawizi ilioparwa kijiko cha chakula 1
- Sukari nusu kikombe cha chai
Maelekezo
Mimina maji kwenye sufuria kisha bandika motoni.
Twanga hiliki na tangawizi, kisha pamoja na mdalasini, weka kwenye maji.
Kwa moto wa wastani, wacha maji yenywe viungo ulivyotumbukiza ndani yachemke vizuri.
Baada ya kuchemka vizuri, weka majani na sukari.
Acha yachemke kidogo kama dakika tatu hivi kabla ya kuepua.
Mimina kwenye chupa halafu tumia kichujio kuchuja viungo na majani ya chai.
Unaweza kunywa na kitafunio chochote kama chapati, keki, au andazi.
Zingatia ushauri huu
Usiweke majani kama maji hayajapata moto vizuri. Hubadilisha ladha ya chai.
Usiweke majani ya chai mengi kwa sababu yanasababisha chai kuwa chungu.
Usiache chai ichemke kwa muda mrefu baada ya kuweka majani.
Next article
SHINA LA UHAI: Jinsi unavyoweza kuyatunza meno yako
[ad_2]
Source link