Joy Mwende, chipukizi anayepepea katika ushonaji na uigizaji
Na WANDERI KAMAU
HUKU serikali ikiendelea na usisitizaji kuhusu umuhimu wa Mfumo wa Elimu wa Umilisi na Utendaji (CBC), kozi za kiufundi zimeibukia kuwa maarufu na zinazokumbatiwa na vijana wengi.
Ni uhalisia huo ambao umemfanya mwanadada Joy Mwende, 21, kujitosa katika tasnia mbili—ushonaji na uigizaji.
Joy, maarufu kama ‘Designer Quirpo’ ni mzaliwa wa Kaunti ya Makueni, ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa mwaka wa nne katika masuala ya ushonaji katika Chuo Kikuu cha Kirinyaga, Kaunti ya Kirinyaga.
Kwa mwaka mmoja sasa, amejizolea umaarufu mkubwa kutokana na ujuzi wake wa kipekee katika kushona mavazi ya miundo tofauti.
Kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’, mwanadada huyo alisema kuwa ingawa amekuwa kwenye fani hiyo kwa mwaka mmoja na miezi miwili pekee, amepiga hatua kubwa ambazo hakudhani angeweza kuzifikia.
“Baada ya serikali kutangaza janga la corona kufika nchini mnamo Machi 2020, watu wengi walibaki majumbani mwao. Ikizingatiwa mimi ni mwanafunzi, shughuli za masomo pia zilivurugika pakubwa baada ya vyuo vikuu kufungwa. Hata hivyo, nilitumia muda niliokuwa nao kuboresha na kuimarisha ujuzi wangu kwenye fani ya ushonaji,” akasema Joy.
Ijapokuwa hajaanza rasmi kuuza baadhi ya mavazi anayotengeneza, anasema analenga kujitosa kwenye biashara ya mavazi mara tu baada ya kumaliza masomo yake.
“Niko katika mwaka wa nne. Kufikia sasa, nimejua mwelekeo nitakaouchukua, kwani baadhi ya wateja wangu wamekuwa marafiki wa karibu. Hata hivyo, sijajitosa rasmi kwenye biashara ya uuzaji wa mavazi. Mara tu baada ya kumaliza shahada yangu, huo ndio mkondo nitakaofuata kwani imenidhihirikia watu wanafurahia kazi yangu,” akasema.
Kijumla, ushonaji si fani rahisi kama wengi wanavyodhania.
Anasema kuwa ili vazi kukamilika na kupendeka na mteja, huwa linahusisha hatua nyingi ambazo lazima zimridhishe.
Hatua ya kwanza ni kuelewa aina ya muundo wa vazi lenyewe. Hatua ya pili ni kufahamu ubora wa kitambaa ambacho vazi litaundwa nacho ili kuwa bora zaidi.
Kwa sasa, huwa anajitosa na ushonaji wa mavazi ya wanawake (hasa mabinti), ijapokuwa anasema ataanza kutengeneza mavazi ya jinsia zote baada ya kumaliza masomo.
Ili kutangaza kazi yake, huwa anatumia mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, YouTube na Tik Tok ili kuwafikia mashabiki wake.
“Katika mtandao wa YouTube, huwa ninaweka video zangu ambazo huwa narekodi nikitengeneza mavazi ili kuwaonyesha wale wanaonifuata pale nilipofikisha ujuzi wangu. Huwa nafanya vivyo hivyo kwenye mitandao hiyo mingine. Huwa naegemea matumizi ya mitandao kwani ndiko dunia inakoelekea. Lazima mfanyabiashara yeyote anayetaka kukuza biashara yake kutambua kuwa mitandao ya kijamii ni nguzo kuu ya kuwafikia maelfu ya wateja wake,” anaeleza.
Baadhi ya washonaji au wanafasheni anaiwaangalia sana ni Judy Gao Culture na Gabriel Union kutoka ughaibuni.
Kando na ushonaji, mwanadada huyu ni mwigizaji chipukizi.
Video zake zimekuwa zikizua msisimko kwenye mitandao ya kijamii, kutokana na weledi wake mkubwa kwenye fani hiyo.
Kama ushonaji, anasema kuwa bado anajikuza kwa kushirikiana na waigizaji wengine chipukizi katika chuo anakosomea na maeneo mengine nchini.
Baadhi ya waigizaji chipukizi ambao amekuwa akishirikiana nao ni CEO Bruce, Mbilimbili kati ya wengine.
Waigizaji ambao amekuwa akiwaangalia ili kukuza talanta yake ni Foi Wambui, Jacky Matubia, Jacky Vicke (Papa Shirandula) kati ya wengine.