Connect with us

General News

Jubilee yageuka sumaku kwa wanaolenga ubunge – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Jubilee yageuka sumaku kwa wanaolenga ubunge – Taifa Leo

Jubilee yageuka sumaku kwa wanaolenga ubunge

CHARLES WASONGA na LEONARD ONYANGO

CHAMA cha Jubilee kimeongoza kwa kuvuna idadi kubwa ya wanasiasa ndani ya wiki moja iliyopita huku mlango wa kuhama vyama vya kisiasa ukifungwa leo Jumamosi.

Jana Ijumaa, makao makuu ya Jubilee yalikuwa na shughuli nyingi huku viongozi wake wakipokea idadi kubwa ya wanasiasa kutoka vyama vingine wanaotaka kutumia tiketi yake kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Aliyekuwa Seneta wa Kitui, David Musila alijiunga na chama hicho baada ya kugura Wiper Democratic Movement chake makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka.

Bw Musila alipokelewa chamani katika hafla iliyoongozwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho, Kanini Kega katika makao makuu yaliyoko mtaani Pangani, Nairobi.

“Sasa Mheshimiwa Musila atawania ugavana wa Kitui kwa tiketi ya chama tawala cha Jubilee,” Bw Kega akasema.

Hatua ya Bw Musila kugura chama cha Wiper ni pigo kwa chama hicho ikizingatiwa kuwa, yeye ndiye alikuwa akitegemewa na Bw Musyoka kumwangusha Gavana Charity Ngilu katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Bw Musyoka amekuwa akitamani kaunti ya Kitui kuongozwa na Gavana wa Wiper ikizingatiwa kuwa hiyo ndio kaunti yake ya nyumbani.

Jana Ijumaa, uvumi ulikuwa umetanda kwamba Mbunge Mwakilishi wa Kirinyaga Wangui Ngirici pia angehamia Jubilee.

Hata hivyo, hadi tulipoenda mitamboni, mwanasiasa huyo hakuwa amechukua hatua hiyo.

Bi Ngirici alikuwa ametangaza kuwa atawania Ugavana wa Kirinyaga kama mgombeaji wa kujitegemea baada ya kugura chama cha United Democratic Alliance (UDA) mwishoni mwa mwaka 2021.

Miongoni mwa wengine ambao wamejiunga na Jubilee katika siku za hivi karibu ni; aliyekuwa Mbunge wa Mugirango Kusini, Omingo Magara na Mbunge wa Sirisia John Waluke ambao waligura United Democratic Alliance (UDA) inayoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Wengine walikuwa aliyekuwa Mbunge wa Kigumo, Jamlek Kamau aliyetangaza kuwania ugavana wa Murang’a kwa tiketi ya Kanu, na wabunge Joyce Emanikor (Mwakilishi wa Kike, Turkana), Mohamed Lokiru (Turkana Mashariki) na James Lomenen (Turkana Mashariki).

“Huu ni ushindi mkubwa kwa chama chetu na mwaniaji urais tunayemuunga mkono Raila Odinga. Chama chetu kinaheshimu demokrasia na kiko tayari kupokea kila mtu,” akasema Bw Kega ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Kitaifa.

Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni jana Ijumaa aliambia Taifa Leo kuwa, chama hicho kinatarajiwa kupokea idadi kubwa ya wanasiasa wanaogura vyama vingine.

Jana Ijumaa, ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kwa wanasiasa wanaotaka kuwania viti kupitia tiketi ya Jubilee kuwasilisha maombi yao.

Mlango wa wanasiasa kuhama vyama unatarajiwa kufungwa leo kabla ya madaftari ya wanachama wa vyama mbalimbali kupelekwa kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa Bi Ann Nderitu kukaguliwa.

Wanasiasa watakaoangushwa katika kura za mchujo watakuwa huru kuhama na kuwania kama wagombea wa kujitegemea. Wanaolenga kugura vyama wanahitajika kufanya hivyo kufikia Mei 2.

Wiki jana, Katibu katika Wizara ya Usalama Karanja Kibicho aliwapokea zaidi ya wanasiasa 50 wa chama cha UDA ambao walijiunga na Jubilee.