Connect with us

General News

Jumwa abanwa katikati ya ndume – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Jumwa abanwa katikati ya ndume – Taifa Leo

Jumwa abanwa katikati ya ndume

VALENTINE OBARA NA ALEX KALAMA

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, anatarajiwa kuwa miongoni mwa wanawake wachache nchini ambao watajitosa katika kinyang’anyiro cha ugavana dhidi ya wanaume tupu katika kaunti zao.

Kufikia sasa, Bi Jumwa pekee ndiye mwanamke ambaye amejitokeza kwa ukakamavu kujipigia debe kwa kiti hicho kitakachobaki wazi wakati Gavana Amason Kingi atakapokamilisha kipindi chake cha pili Agosti.

Wanasiasa wengine wanaomezea mate wadhifa huo ni Naibu Gavana Gideon Saburi, aliyekuwa waziri msaidizi wa Ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro, wakili George Kithi, na Spika wa Bunge la Kilifi, Bw Jimmy Kahindi.

Isipokuwa Bw Kithi ambaye ni mwanachama wa Pamoja African Alliance (PAA), wengine waliosalia ni wa ODM.

Bi Jumwa, ambaye anaegemea chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto, alijipiga kifua na kupuuzilia mbali swala kuhusu ikiwa atafanikiwa kuwashinda na kuwa gavana wa kwanza wa kike kaunti hiyo.

Kulingana naye, huu ni wakati mwafaka kwa wananchi kumpa nafasi mwanamke aongoze ili kutatua changamoto sugu za kaunti hiyo kama vile uhaba wa chakula, maji, ukosefu wa ajira, miongoni mwa nyingine.

“Mama akiwa pale kila mtu atakuwa anapata haki yake. Kutakuwa na shibe kimaendeleo. Mimi Aisha Jumwa ndiye Mama Lao. Hao waume wanaotafuta ugavana waambie nafasi yao ni 2032,” akasema akiwa Kilifi wikendi.

Kitaifa, kiti cha ugavana kimekuwa kikivutia zaidi wanaume tangu mwaka wa 2013, na idadi kubwa ya waliochaguliwa katika chaguzi mbili zilizopita walikuwa wanaume. Eneo zima la Pwani halijawahi kuwa na gavana wa kike.

Katika uchaguzi uliopita, magavana wanawake waliochaguliwa ni Charity Ngilu wa Kaunti ya Kitui, Anne Waiguru (Kirinyaga) na marehemu Joyce Laboso (Bomet).

Mwaka huu, inatarajiwa idadi ya wanawake watakaojitosa katika kinyang’anyiro cha ugavana itaongezeka ingawa kuna kaunti ambapo hakuna hata mwanamke mmoja aliyejitokeza kufikia sasa, huku kaunti nyingine zikiwa na mwanamke mmoja au wawili pekee wanaotaka wadhifa huo.

“Wakisema wataungana dhidi ya Aisha Jumwa, hawajui mimi ndiye ‘anaconda’,” akasema, akipuuza mipango ya baadhi ya wagombeaji kuungana ili kuachia mmoja wao nafasi katika debe.

Akiwa katika hafla tofauti, Mwenyekiti wa shirika la Maendeleo ya Wanawake tawi la Kaunti ya Kilifi, Bi Witness Tsuma, alisema hamasisho zinaendelezwa katika kaunti hiyo ili kuongeza idadi ya wanawake wanaoingia uongozini kisiasa.

“Najua wengi wanaogopa kwa kuwa hawana pesa, lakini ninayo mikakati ambayo ninajaribu kuipanga katika kila wadi. Nitahakikisha naandaa kina mama ambao ifikapo 2027 mwenyezi Mungu akipenda, idadi kubwa ya madiwani watakuwa kina mama na vijana,” akasema Bi Tsuma.

Baadhi ya masuala ambayo hutajwa kuchangia kwa idadi ndogo ya wanawake wanaojitosa katika siasa ni kama vile wengi wao kutopenda kupakwa tope ilivyo desturi katika siasa za nchi nyingi ulimwenguni, mbali na ghasia za uchaguzi na gharama kubwa za kampeni.

Masuala mengine ambayo huibuka na kutatiza wanawake wanaotaka kujitosa katika siasa ni itikadi za kijamii na kidini kuhusu uongozi ambapo kipaumbele huendea wanaume.

Mbali na Bi Jumwa, mwanaharakati wa masuala ya afya katika Kaunti ya Lamu, Bi Umra Omar, pia huenda akawa mgombeaji pekee wa kike wa ugavana kaunti hiyo kwani kufikia sasa hakuna mwanamke mwingine aliyejitokeza.

Katika Kaunti ya Kwale, Naibu Gavana Fatuma Achani na seneta maalumu wa ODM, Bi Agnes Zani, wametangaza azimio la kuwania ugavana.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending