Connect with us

General News

Kabogo awarai wakazi wa Ruiru wamchague arudi kuwa gavana Kiambu – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kabogo awarai wakazi wa Ruiru wamchague arudi kuwa gavana Kiambu – Taifa Leo

Kabogo awarai wakazi wa Ruiru wamchague arudi kuwa gavana Kiambu

Na SAMMY WAWERU

ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu, William Kabogo ameendeleza kampeni yake kurai wapiga kura wa kaunti hiyo kumchagua tena katika uchaguzi mkuu ifikapo Agosti 9, 2022.

Bw Kabogo aliwania kuhifadhi kiti chake 2017 kama mgombea wa kujitegemea, japo alibwagwa na Ferdinand Waititu (Jubilee).

Hata hivyo, Bw Waititu naye alivuliwa taji la ugavana Januari 2020 na seneti baada ya bunge la Kaunti ya Kiambu kupitisha mswada wa kumng’atua mwishoni mwa 2020, kufuatia madai ya ufisadi, ubadhirifu wa mali ya umma na matumizi mabaya ya ofisi.

Aliyekuwa naibu wake, James Nyoro ndiye alimrithi kwa mujibu wa matakwa ya Katiba.

Kabogo ametangaza nia kurejea gavana, akihoji amepata msukumo kutoka kwa wakazi wa Kiambu.

“Msinirudishe na kura nusu, mnirejeshe na zote,” akasema akizungumza eneo la Ruiru.

Matamshi yake yakionekana kulenga waliorithi wadhifa wake, Bw Kabogo aidha alisema wenyeji Kiambu wamechoshwa na uongozi mbaya.

“Ninajua mmechoka kujaribu, mnirejeshe tena na hamtajuta,” akasema.

Gavana huyo wa zamani anayemezea mate kiti hicho kupitia Tujibebe Wakenya Party, aliahidi wakazi wa Ruiru kwamba atafufua miradi aliyoanzisha akiwa madarakani.

Alielezea kusikitishwa kwake na warithi wake kusambaratisha mipango na miradi aliyoasisi, akiwasuta kama “viongozi wanaoongozwa na tamaa za ubinafsi badala ya maslahi ya wananchi”.

“Mkinirejesha, nitang’oa zulia la Ruiru Stadium nililoweka na ambalo sasa limechakaa, niwawekee jingine,” akaahidi.

Kabogo anashirikiana kwa karibu na kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi ambaye amejiunga na vuguvugu la Tangatanga linaloongozwa na Naibu wa Rais, Dkt William Ruto.

Katika ziara yake Ruiru, Kabogo alisema endapo atachaguliwa gavana wapiga kura mwaka wa 2027 ndio wataamua ikiwa anapaswa kurejea au la kutokana na rekodi yake ya utendakazi.

“Ninahitaji muhula mmoja tu kuwathibitishia. Nyinyi ndio mtaamua iwapo mtataka nirejee au nistaafu,” akaelezea.

“Ama pia mnaweza kunipandisha madaraka niwe rais. Mniambie ni kitu gani sina, Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake wanacho?” Bw Kabogo akataka kujua.

Alisema uhusiano wake na Rais Kenyatta ni wa karibu, na atahakikisha ahadi alizotoa kwa wakazi wa Ruiru zimeafikiwa kikamilifu kabla kiongozi wa nchi astaafu.