Connect with us

General News

Kampuni yazindua kiwanda cha kuongeza thamani mazao mabichi ya kilimo – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Na SAMMY WAWERU

KERO ya soko hasa kwa mazao mabichi ya kilimo ni jambo ambalo huhangaisha wakulima wengi nchini.

Endapo hawana vifaa vya kuyahifadhi au mikakati faafu, hukabiliwa na kibarua kigumu kuyawasilisha sokoni.

Ni changamoto zinazowapa mwanya mawakala kuwakandamiza kibiashara, wafanyabiashara hao wakisalia na vinono mfukoni.

Isitoshe, huchukua mazao ya hadhi ya juu, yaliyosalia ingawa bora, mkulima anaachwa ajipange nayo.

Mahangaiko ya aina hiyo, yanapaswa kutathminiwa kwa msingi wa uongezaji thamani.

Mojawapo ya Ajenda Nne Kuu za Rais Uhuru Kenyatta, ni kuboresha sekta ya viwanda, ambayo kwa kiasi kikubwa inafanikishwa na kilimo.

Kusaidia kuafikia hilo, kampuni moja jijini Nairobi imezindua kiwanda cha kuongeza thamani mazao mabichi ya kilimo, hasa yanayotajwa kuwa ya hadhi ya chini na yanayokataliwa sokoni.

Kiwanda cha NatureLock kinalenga kuokoa mazao ya shambani yanayopotea baada ya mavuno.

“Tunaleta pamoja mazao ambayo yangeoza, kwa kuyafunga yadumu muda mrefu. Tunayaongeza thamani kwa kutumia malighafihai,” anasema Afisa Mkuu Mtendaji NatureLock, Bi Tei Mukunya.

Bi Tei anasema wamekumbatia mifumo ya Kisayansi kuyakausha.

“Shabaha yetu ni kuokoa mazao yanayokataliwa shambani ilhali ni bora. Kwa mfano, karoti zilizovunjika, vitunguu vinavyoonekana kutokuwa na umbo la kuvutia (maumbile), nyanya, viazi, kati ya mazao mengineyo, ambayo hayapati soko la haraka,” anafafanua.

Huku kila mkulima akiwa na bakisho la zao lililokataliwa na hatimaye kuharibika, NatureLock inasema asilimia 75 ya mazao inayolenga yatatoka katika utandazi huo.

Kwa ushirikiano na Farm to Feed, kampuni hiyo imeanza kusindika ndengu, bidhaa inayotokana ikitumika kutengeneza mchuuzi.

Nafaka hiyo inaongezwa unga wa mihogo, vitunguu vyekundu, nyanya, karoti, mafuta ya halizeti, mafuta ya mnazi, pilipili hoho (pilipili kali au pilipili kichaa), vitunguu saumu, tangawizi, na giligilani (dania).

“Tulitangulia na ndengu kwa sababu ni nafaka yenye madini na virutubisho faafu, katika familia ya Legumi. Mimea itakayofuata itakuwa sukuma wiki, spinachi, mboga za kienyeji na kabichi, kwa sababu huwa katika hatari ya kuoza msimu wa mavuno,” Tei akasema wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho Mombasa Road, Nairobi.

Uholanzi, serikali ya nchi hiyo imeweka mikakati maalum kuimarisha sekta ya viwanda, kupitia uongezaji thamani mazao ya kilimo.

“Maendeleo yanadhihirika kupitia uzalishaji wa chakula, ambapo hakuna kinachopaswa kupotea na watu wote wapate,” akasema Balozi wa Uholanzi nchini Kenya, Bw Marteen Brouwer, akisifia hatua ya NatureLock kuzindua kiwanda hicho.

Kampuni yazindua kiwanda cha kuongeza thamani mazao mabichi ya kilimo – Taifa Leo
Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya NatureLock, Bi Tei Mukunya (kulia) akiarifu Balozi wa Uholanzi hapa Kenya, Bw Marteen Brouwer (pili kutoka kulia) kiwanda cha kampuni hiyo kuongeza thamani kinavyofanya kazi. Picha/ Sammy Waweru

Ulimwenguni, thuluthi moja ya chakula hupotea, watu wengi wakiendelea kusalia njaa.

Kulingana na Bw Brouwer, haja ipo sekta ya kilimo na biashara kuwa na miakati bora, ili kudhibiti vyakula kuharibika.

“Serikali inahitaji kuweka mipango na mikakati maalum,” Balozi huyo akahimiza, akiahidi kwamba serikali ya Uholanzi itashirikiana na NatureLock.

Kiwanda hicho kiligharimu zaidi ya Sh40 milioni, Bi Tei akifichua Hooge Raedt Social Venture (HRSV) ndio mwekezaji mkuu. Aidha, kwa sasa kina wafanyakazi 28.

“Tunapanga kuwa na viwanda vitano kufikia mwaka ujao. Vile vile, tunalenga programu za kulisha shule,” afisa huyo akasema.

Alisema kufikia sasa wana vituo sita vya kukusanya mazao.

“Tunashirikiana kwa karibu na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (KARLO), wakulima wa ndengu waboreshe mazao yao,” akaelezea.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Trending