Connect with us

General News

Kampuni za maziwa zapata hasara – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kampuni za maziwa zapata hasara – Taifa Leo

Kiangazi: Kampuni za maziwa zapata hasara

NA BARNABAS BII

KAMPUNI zinazomiliki viwanda vya kuhifadhi maziwa zinaendelea kupata hasara za mamilioni ya pesa kutokana na ukame unaondelea kushuhudiwa ambao umeathiri ufugaji.

Kiwango cha maziwa ambacho kimekuwa kikiwasilishwa na wakulima katika viwanda hivyo kimepungua kwa nusu, hali hiyo ikitokana na ukosefu wa lishe ya mifugo.

Kwa sasa kampuni hizo zimepunguza idadi ya wafanyakazi kwenye viwanda hivyo ndipo zisilemewe na gharama za kuendesha shughuli zao.

“Ukame unaoendelea umekuwa na mchango hasi kwa kilimo cha ufugaji hasa ng’ombe wa maziwa. Hatupokei tena maziwa kwa wingi kama hapo awali kutoka kwa wakulima na hilo limeathiri shughuli zetu,” akasema David Kiptoo ambaye anamiliki kiwanda cha maziwa cha Lelgaa katika Kaunti ya Nandi.

Kwa kawaida kiwanda hicho kilikuwa kikipokea lita 10,000. Hata hivyo, kiwango hicho sasa kimepungua hadi lita 2,000 pekee huku wakulima nao wakilalamikia ukosefu wa lishe na bei ya juu inayotozwa.

“Lazima tugharimie lishe, tuwalipe wafanyakazi wetu na pia bili ya umeme. Kupungua kwa uzalishaji kumetuathiri kwa sababu hata sisi tuna mikopo na lazima tuzungumze na wanaotudai ili wasichukue mali yetu,” akasema Bw Kiptoo.

Kauli yake iliungwa mkono na Reuben Kosgei wa chama cha ushirika cha wakulima katika Kaunti ya Nandi.

“Kiasi cha maziwa kinachowasilishwa viwandani kimepungua kutokana na ukame na kuathiri sana fedha tunazopata pamoja na malipo ya madeni yetu. Pia sasa wakulima hawawezi kuchukua mikopo kununua mifugo na lishe bora kama hapo awali,” akasema Bw Kosgei.

Bei ya maziwa sasa imepanda kwa Sh12 kwa kuwa hapo awali yalikuwa yakiuzwa Sh48 na sasa yanauzwa Sh60 kwa lita. Familia nyingi zimelazimika kugharimika zaidi ili kununua maziwa hayo.

Vilevile maduka mengi Kaskazini mwa Bonde la Ufa sasa yanakabiliwa na uhaba wa maziwa nao wanaofika katika maduka ya jumla wanatakiwa kutobeba zaidi ya pakiti mbili.

Hata hivyo, wakulima wanaowafuga ng’ombe wa maziwa ambao walihifadhi lishe la kutosha hawajaathirika sana wakati huu ambapo ukame unaendelea kuathiriki kilimo.

“Niliweka akiba sehemu ya mavuno yangu ya mahindi na kuitumia kutengeneza lishe kwa mifugo yangu. Sasa sijaathirika na uhaba wa lishe kama wakulima wengine,” akasema Willy Koskei, kutoka Chepkanga, Kaunti ya Uasin Gishu.

Vilevile, wafanyabiashara wameongeza lishe ya mifugo ambayo sasa inauzwa kwa Sh1,800 kutoka Sh1,600 kwa kila gunia.

Idadi ya ng’ombe wa maziwa Kaskazini mwa Bonde la Ufa huwa ni milioni 1.2 huku wale wanaofugwa kuchinjwa kisha nyama yao kuuzwa wakiwa kati ya 400,000 -500,000.