Connect with us

General News

Kananu kurithi kiti dhaifu cha ugavana jijini – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kananu kurithi kiti dhaifu cha ugavana jijini – Taifa Leo

Kananu kurithi kiti dhaifu cha ugavana jijini

Na BENSON MATHEKA

NAIBU GAVANA WA Nairobi, Bi Ann Kananu Mwenda anayetarajiwa kuapishwa wakati wowote wiki hii kuwa Gavana wa tatu wa Nairobi, hatakuwa na nguvu kama magavana wengine.

Hii ni kwa kuwa mtangulizi wake Mike Sonko alikuwa amehamishia majukumu muhimu kwa Serikali ya kitaifa, yanayotekelezwa na Shirika la Huduma la Nairobi (NMS).Mkataba wa kuhamisha majukumu uliopelekea Rais Uhuru Kenyatta kubuni NMS inayosimamiwa na Luteni Jemedari Mohamed Badi, utakamilika Februari 25, 2022.

Mkataba huo unaweza kuongezwa muda na iwapo hilo litafanyika, Bi Kananu ataendelea kukosa makali ya kusimamia Kaunti ya Nairobi kwa kipindi cha takriban miezi 10 atakayokuwa ofisini. Mnamo Jumatatu wiki hii, Mahakama ya Juu ilitupilia mbali kesi iliyozuia Bi Kananu kuapishwa kuwa gavana wa tatu na wa kwanza mwanamke wa Nairobi.

Kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa na Bw Sonko ambaye licha ya kumteua kushikilia wadhifa wa naibu gavana 2020, hakuweza kuidhinishwa na bunge la Kaunti baada ya kesi kuwasilishwa kortini kuzuia madiwani kumpiga msasa.Desemba 18, 2020, Sonko aliondolewa ofisini nayo mahakama ikaondoa agizo la kuzuia kupigwa msasa na bunge la Kaunti.

Sonko aliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu na kupata agizo la kuzuia kuapishwa kwa Bi Kananu kuwa gavana; na Juni mwaka huu majaji Said Chitembwe, Weldon Korir na Wilfrida Okwany walitupa kesi hiyo.

Sonko aliwasilisha kesi katika Mahakama ya Juu ambayo wiki hii ilitupa tena na kufungua milango kwa Bi Kananu kuapishwa.Hata hivyo, japo amekuwa kaimu gavana tangu mwaka jana, ni NMS ambayo imekuwa ikisimamia majukumu yote yaliyohamishiwa serikali ya kitaifa kupitia mkataba ambao Sonko alitia katika ikulu ya Nairobi mnamo Februari 25.

Katika mkataba huo, Bw Sonko alihamisha Huduma za Afya, Huduma za Umma, Huduma za Uchukuzi na Mipango ya Maendeleo ya Kaunti.Bw Sonko pia alihamisha huduma za mazingira na ukusanyaji ushuru.

NMS kwa ushirikiano na asasi nyingine za serikali imeweka mifumo mipya ya ukusanyaji ushuru na imekuwa ikiungwa na bunge la Kaunti. “Hii itaacha Bi Kananu kuwa gavana asiye na nguvu sawa na Sonko alivyokuwa baada ya kuhamisha majukumu.

Kazi yake itakuwa ni kuidhinisha maamuzi na pesa kwa NMS kwa kuwa hana mamlaka ya kukatiza mkataba wa mtangulizi wake na serikali ya kitaifa iliyobuni NMS,” asema mchanganuzi wa masuala ya utawala Peter Keli.

Anasema japo mkataba wa kuhamisha majukumu ya serikali ya kaunti hadi serikali ya kitaifa utaisha mwaka ujao, ishara ni kwamba NMS inayosimamiwa na maafisa wa jeshi la Kenya litadumu. “Mkataba huo utaongezwa muda mradi tu Rais Kenyatta awe mamlakani.

Kwa sababu hii, Bi Kananu akiapishwa kuwa gavana, ataendelea kushirikiana na NMS. Kumbuka ni serikali ya Jubilee iliyomsaidia kupata wadhifa wa naibu gavana,” asema.