Connect with us

General News

Karata ya kuteua manaibu gavana sasa yafichuka – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Karata ya kuteua manaibu gavana sasa yafichuka – Taifa Leo

Karata ya kuteua manaibu gavana sasa yafichuka

NA MWANDISHI WETU

SIASA za urithi wa Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, zimechukua mkondo mpya baada ya kufichuka kwamba wanaotaka tikiti ya ODM kuwania wadhifa huo wanashindana kuteua wagombea wenza watakaovutia idadi kubwa ya kura.

Kufikia sasa, wanasiasa wanaotaka kuwania ugavana Mombasa kupitia ODM ni mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, Naibu Gavana, Dkt William Kingi, na mfanyabiashara, Bw Suleiman Shahbal.

Duru katika Chama cha ODM zimeambia Taifa Leo kuwa, kufikia sasa wagombeaji watarajiwa wanazingatia sana kuteua wanawake kutoka jamii za asili ya Pwani kuwa wagombea wenza kama mkakati wa kuimarisha kampeni zao.

Miongoni mwa waliotajwa kulengwa kuwa wagombea wenza ni Bi Barbara Ngome, ambaye ni afisa mkuu katika af isi ya gavana.

Bi Ngome amekuwa akifanya kazi na Bw Joho tangu mwaka wa 2013 na amewahi kuhusika katika masuala ya kuleta vijana pamoja.

Mwanafunzi huyo wa chuo kikuu alikuwa kwenye kampeni za Bw Joho mwaka 2013, na uteuzi wake kuwa mgombea mwenza unatarajiwa kuvutia pia kura za vijana.

Licha ya wanachama wa ngazi za juu katika ODM kusema Ngome anazingatiwa kuwa mgombea mwenza wa mmoja wa wanasiasa wanaotaka ugavana, alikataa kuthibitishia Taifa Leo alipohojiwa.

“Siwezi kujibu hili swali kwa sasa,” akasema Bi Ngome.

Mbali na yeye, imebainika mwanamke mwingine anayezingatiwa kuwa naibu gavana ni dada ya mwanasiasa maarufu wa zamani wa Mombasa, aliyewahi kuwa mbunge wa Kisauni.

Uteuzi wa mwanamke huyo, ambaye tumebana jina, unatarajiwa kuvutia kura za wanawake na jamii ya Wamijikenda kwa jumla.

Awali Bw Shahbal na Bw Nassir walikuwa wakimvizia mwanahabari Francis Thoya, ambaye alikuwa katibu wa kaunti kwa miaka kadhaa katika serikali ya Bw Joho.

Hata hivyo, katika mahojiano, Bw Thoya alisema hana azimio la kuwa naibu gavana.

Bw Thoya alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakisakwa na Bw Joho kuwa naibu wake kwenye kinyang’anyiro cha 2017 baada ya gavana huyo kukosana na Bi Hazel Katana aliyekuwa naibu wake tangu 2013.

Wachanganuzi wa masuala kisiasa, Bi Maimuna Mwidau na mwenzake Grace Oloo wamesema wagombea wote wa ugavana hawana budi kuchagua wanamke kuwa wagombeawenza.

Hata hivyo, wamesisitiza kwamba ni sharti mwanamke anayeteuliwa awe na uwezo na tajriba.

“Wasichague mwanamke tu kwa sababu wanataka kujaza pengo la kijinsia. Tunataka kiongozi mwanamke ambaye ni kiongozi. Tunataka mwanamke ambaye ataweza kuhakikisha masuala ya wanawake yanapewa kipaumbele,” akasema Bi Oloo.