Connect with us

General News

Kasi ya Ruto yatoa jasho Mudavadi, Wetang’ula – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kasi ya Ruto yatoa jasho Mudavadi, Wetang’ula – Taifa Leo

Kasi ya Ruto yatoa jasho Mudavadi, Wetang’ula

NA LEONARD ONYANGO

KINARA wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula watalazimika kuzoea kasi ya Naibu wa Rais Wiliam Ruto ya kuhutubia mikutano mingi kwa siku na kuketi juu ya gari kwa muda mrefu.

Tangu Mabw Mudavadi na Wetang’ula watangaze kujiunga na Dkt Ruto siku 21 zilizopita na kuunda muungano wa Kenya Kwanza, vigogo hao wamehutubia mikutano ya kisiasa katika kaunti 20.

Tofauti na awali wawili hao walipokuwa katika muungano wa One Kenya Alliance (OKA) ambapo walihutubia mkutano mmoja na kupumzika kwa wiki moja, sasa wanalazimika kuhutubia mikutano kila siku.

Viongozi wa Kenya Kwanza wakiongozwa na Naibu wa Rais wamezuru baadhi ya kaunti mara mbili tangu kuwanasa Mabw Mudavadi na Wetang’ula mnamo Januari 23, mwaka huu.

Mkutano wa kwanza uliojumuisha viongozi hao watatu uliandaliwa katika Uwanja wa

Maonyesho wa Nakuru Januari 26. Lakini kabla ya kufika Nakuru, walihutubia wakazi wa El – dama Ravine, Kaunti ya Baringo.

Naibu wa Rais alipokuwa nje ya nchi kati ya Februari 1 na Februari, Bw Mudavadi aliongoza kampeni za Kenya Kwanza mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru.

Jana, viongozi wa Kenya Kwanza, wakiongozwa na Dkt Ruto walikita kambi katika Kaunti ya Nakuru ambapo walihutubia mikutano ya kisiasa katika maeneo ya Njoro, Kuresoi na Gilgil kujipigia debe.

Dkt Ruto alielekea Gilgil siku moja baada ya kumnasa mbunge wa eneo hilo Martha Wangari aliyegura Jubilee na kujiunga na United Democratic Alliance (UDA).

Alhamisi, viongozi wa Kenya Kwanza walihutubia mikutano mitano katika Kaunti za Kisii na Nyamira. Dkt Ruto na Mabw Mudavadi na Wetang’ula leo wanarejea katika Kaunti ya Kakamega ambapo watafanya mkutano kwenye uwanja wa Amalemba.

Viongozi wa Kenya Kwanza wanarejea Kakamega siku tatu baada ya kutoka huko ambapo waliandaa mikutano ya kisiasa katika maeneo ya Mumias, Khwisero, Matungu, Likuyani, Lumakanda na Shinyalu.

Kenya Kwanza pia walihutubia mikutano kadha katika Kaunti za Busia, Trans Nzoia, Vihiga na Bungoma. Dkt Ruto analenga kuvuna mamilioni ya kura katika eneo la Magharibi baada ya kuungana na Mabw Mudavadi na

Wetang’ula wanaochukuliwa kuwa vinara wa eneo hilo.

Dkt Ruto alielekea Magharibi baada ya kutoka Pwani ambapo walifanya mikutano ya kisiasa katika Kaunti za Taita Taveta, Kwale, Mombasa na Kilifi.

Ni katika ziara hiyo ya Pwani ambapo Dkt Ruto aliteua Gavana wa Kwale Salim Mvurya kuwa kwenye kikosi chake cha kampeni za urais. “Nawashukuru wakazi wa Kwale kwa kuruhusu Gavana Mvurya kuwa kwenye kikosi cha kampeni za muungano wa Kenya Kwanza,” alisema Dkt Ruto.

Viongozi hao pia wamefanya mikutano ya kisiasa katika Kaunti za Nairobi, Embu, Kirinyaga, Kajiado na Kiambu.

Alipokuwa katika Kaunti ya Makueni mwezi jana, Dkt Ruto alifichua siri yake ya kuzuru eneo fulani mara nyingi huku akisema uwepo wake mara kwa mara unafanya wakazi kumzoea. “Napenda kuwaomba radhi wakazi wa Makueni sijakuwa nikija hapa mara kwa mara ndiyo maana mnapenda yule jamaa yule wa vitendawili. Kuanzia sasa nitakuwa nikija hapa mara kwa mara,” alisema Dkt Ruto huku akimrejelea kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga.

Mbali na kuwekwa kwenye msururu wa kampeni, wadadisi wanasema Dkt Ruto amewapa Mabw Mudavadi na Wetang’ula jukumu la kumshambulia Bw Odinga, Rais Uhuru Kenyatta na kufichua maovu ya serikali ya Jubilee.