CHARLES WASONGA: Kauli za Moses Kuria na wengine zipuuzwe kwani zimepitwa na wakati
NA CHARLES WASONGA
KIPENGELE cha 33 cha Katiba ya sasa kinasema kila mtu ana uhuru kujieleza, kupokea na kupitisha habari.
Lakini uhuru huo haujumuishi uenezaji wa matamshi ya chuki au uchochezi wa uhasama wa yoyote ile ukiwemo wa kikabila au kidini.
Hii ndio maana Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kwa ushirikiano na Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kuwaandamana watu, husasan wanasiasa, wenye mazoea ya kutoa matamshi ya chuki.
Kwa misingi hii, nalaani vikali matamshi ambayo Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria alitoa Ijumaa wiki jana wakati wa kampeni ya kumpigia debe Naibu Rais William Ruto katika eneo hilo.
Alionya Rais Uhuru Kenyatta na jamii ya Wakikuyu, kwa ujumla, kuwa watalaaniwa ikiwa watamuunga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais Agosti 9.
Kulingana na Bw Kuria, laana hiyo itaifika jamii hiyo kwa sababu ya kwenda kinyume na kiapo 1960s kilichowakataza kumpigia kura mtu ambaye hajapashwa tohara.
Kauli kama hii ni hatari kwa sababu inaweza kuchochea uhasama wa kikabila baina ya jamii ya Wakikuyu na jamii zingine ambazo haziendeshi utamaduni wa upashaji tohara. Inapanda mbegu ya utengano miongoni mwa jamii mbalimbali nchini kwa misingi ya utamaduni kama huu.
Ni kinyume cha Katiba ya sasa inayosema kuwa Wakenya wote wana haki ya kufurahia haki zote bila kubaguliwa kwa misingi masuala mengi ikiwemo mila na tamaduni zao.
Kenya ina zaidi ya makabila 44 yenye tamaduni, mila na kaida tofauti lakini yameungana kuunda nchi moja. Ni kwa kutambua utofauti huu ambapo Wimbo wetu wa Kitaifa unahimiza wananchi kuishi kwa umoja, amani na uhuru ili kuistawisha Kenya.
Nahimiza kizazi cha sasa kupuuzilia mbali kauli ya Bw Kuria, na watu wengine wenye fikra sawa na hizo.
kwa sababu haina msingi wowote katika maisha ya sasa. Hii ni kwa sababu Mbunge huyo hana ithibati yoyote kwamba mgombea urais ambaye anaonya jamii yake dhidi ya kumpigia kura, kwa kweli hajapashwa tohara.
Nawaomba wapiga kura kutoka jamii ya Agikuyu kufanya maamuzi yao kuhusu ni nani watampigia kura za urais, kwa misingi ya sera mwaniaji huyo wala sio viapo ambavyo mababu zao walilishwa katika miaka ya 1960s.
Next article
Mradi wa Buxton wapata pigo tena