Kenya Seed yazindua aina mbili za mbegu za mahindi yanayostahimili kiangazi na magonjwa
NA SAMMY WAWERU
KAMPUNI ya Kenya Seed (KSC), imezindua aina mbili za mbegu za mahindi zenye mazao bora yanayostahimili athari za kiangazi na magonjwa.
Kulingana na shirika hilo, mbegu aina ya H519 ina mazao ya kuridhisha na maganda bora, huku H532 ikiwa na ustahimilivu wa hali ya juu kwa kiangazi na ugonjwa unaoathiri majani – Gray Leaf Spot.
Uzinduzi huo ni afueni kwa wakulima wa mahindi nchini.
Kaunti ya Uasin Gishu na Trans Nzoia, ndizo zinaongoza katika uzalishaji wa mahindi Kenya.
Athari za mabadiliko ya tabianchi nchi yakiendelea kushuhudiwa na kiwango cha joto kupanda kupita kiasi, Kenya imetajwa kuwa miongoniwa nchi katika Upembe wa Afrika zilizoathirika kwa kiwango kikubwa kutokana na ukame unaoshuhudiwa.
Mataifa mengine kulingana na Shirika la Chakula na Kilimo, FAO – UN, ni Ethiopia na Somalia.
Akisifia uvumbuzi wa mbegu hizo za mahindi, Meneja Mkurugunzi Kenya Seed, Bw Fred Oloibe amesema hatua hiyo inaenda sambamba na malengo ya kampuni hiyo kupiga jeki Ajenda Nne Kuu za Kiongozi wa Nchi kati ya 2017 – 2022.
Mwaka wa 2017, baada ya kuchaguliwa kuhudumu awamu yake ya pili na ya mwisho, Rais Uhuru Kenyatta aliahidi kuwa shabaha yake ni kuhakikisha Kenya inakuwa salama katika masuala ya chakula.
“Tutaendelea kufanya utafiti na uvumbuzi wa mbegu zinatakazolifaa taifa, kuwa na chakula cha kutosha na kudumisha usalama wa mlo,” Bw Oloibe akasema, akiahidi kujitolea kwa KSC kusaidia kuboresha sekta ya kilimo nchini.
Afisa wa kampuni moja ya pembejeo nchini inayotengeneza mbegu za nafaka, akionyesha pakiti yenye mbegu za mahindi. PICHA | SAMMY WAWERU
Afisa huyo alisisitiza janga la njaa litakabiliwa kupitia ushirikiano wa kampuni na mashirika ya pembejeo na wadauhusika katika sekta.
Katika Maonyesho ya Kilimo, Ufugaji na Mashine yaliyofanyika majuzi Eldoret, Kenya Seed Company ilitumia jukwaa hilo kuvumisha mbegu hizo mpya.
Yalihudhuriwa na mamia na maelfu ya wakulima na wafugaji, kutoka sehemu mbalimbali za nchi, wanaochangia katika mtandao wa uzalishaji wa chakula na mazao.
“Kama kampuni, tunafanya kila tuwezalo kuhamasisha wakulima kupata mbegu bora na faafu, zitakazoweza kustahimili changamoto za hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi,” Oloibe akaelezea.
Huku sekta ya kilimo ikiwa kati ya nguzo kuu kufanikisha malengo ya Ruwaza 2030, imekumbwa na changamoto tele ongezeko la juu la bei ya fatalaiza likitishia jitihada za wakulima nchini.
Mfuko wa kilo 50 sasa unagharimu zaidi ya Sh6,000 kutoka Sh3,000, wadauhusika katika sekta wakidai mfumko huo unatokana na upungufu wa malighafi kutengeza mbolea.
Kenya huagiza nje malighafi kutengeneza fatalaiza, janga la corona vilevile likitajwa kuchangia hali kuwa mbaya zaidi.