Connect with us

General News

Kenya yaadhimisha miaka 10 tangu kukumbatia mfumo wa Bayoteknolojia kuboresha kilimo na ufugaji – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kenya yaadhimisha miaka 10 tangu kukumbatia mfumo wa Bayoteknolojia kuboresha kilimo na ufugaji – Taifa Leo

Kenya yaadhimisha miaka 10 tangu kukumbatia mfumo wa Bayoteknolojia kuboresha kilimo na ufugaji

Na SAMMY WAWERU

KENYA inaadhimisha miaka 10 baada ya kukumbatia mfumo wa bayoteknolojia katika kuendeleza kilimo, hatua ambayo Wanasayansi na wataalamu wanasema itasaidia pakubwa kuangazia changamoto zinazozingira sekta ya kilimo.

Mfumo huu unajumumuisha bunifu za Kisayansi na teknolojia, ikiwemo kuongeza jeni, kuboresha mimea na mifugo ili kupata spishi zilizoboreka (GMO)S kusaidia kupambana na kero ya wadudu na magonjwa.

Isitoshe, unasaidia kuafikia usalama wa mazao kwa kupunguza matumizi ya kemikali na gharama ya uzalishaji.Kulingana na wataalamu, ukumbatiaji wa bayoteknolojia nchini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita umeashiria kuzaa matunda.

Desemba 2019, serikali iliidhinisha upanzi wa pamba iliyoimarishwa kupitia teknolojia hii, baada ya kufanyiwa ukaguzi, utafiti na jaribio. Juni mwaka uliopita, Kenya ilipiga hatua nyingine mbele baada ya kuidhinisha upanzi wa muhogo ulioboreshwa.

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (Karlo), pia imekamilisha jaribio la mahindi yaliyoboreshwa na kuwa na ustahimilivu dhidi ya mdudu anayeshambulia matawi (stem borer), yakisubiri idhini ya Baraza la Mawaziri kuanza kukuzwa.

Prof. Dorington O. Ogoyi, Afisa Mkuu Mtendaji Mamlaka ya Kitaifa Kuhusu Usalama wa Bayoteknolojia.

“Ni maendeleo ya kuridhisha, hasa ikizingatiwa Kenya ni miongoni mwa mataifa ya kwanza ulimwenguni kukumbatia mhogo-GM, ulioboreshwa. “Bayoteknolojia inasaidia kuangazia changamoto zinazozingira sekta ya kilimo,” akasema Prof. Dorington O. Ogoyi, Afisa Mkuu Mtendaji Mamlaka ya Kitaifa Kuhusu Usalama wa Bayoteknolojia, akizungumza katika hafla ya Shirika la Kuhamasisha Matumizi ya Bayoteknolojia (OFAB) tawi la Kenya kutuza wanahabari jijini Nairobi.

Aidha, wanahabari waliozawadiwa ni walioibuka bora katika uandishi wa makala ya Bayoteknolojia, Sayansi na Ubunifu, katika sekta ya kilimo 2021, baada ya droo kufanywa. Prof. Dorington alipongeza vyombo vya habari kufuatia jitihada zake kueneza na kusambaza manufaa ya bayoteknolojia.

“Athari za mabadiliko ya tabianchi (climate change), wadudu na magonjwa, yataangaziwa na kudhibitiwa kupitia teknolojia, Sayansi na ubunifu,” akaelezea. Dkt Margaret Karembu, mwenyekiti wa OFAB-Kenya, alifichua kwamba kufikia Desemba 2020 mimea iliyoboreshwa kupitia mfumo huu ilikuzwa kwenye hektari milioni 190.4 za mashamba katika mataifa 29 duniani.

“Asilimia 95 ya kiwango hicho ni kutoka mataifa yanayoendelea kukua,” Dkt Karembu akasema. Wizara ya Kilimo, Mifugo na Samaki imeahidi kutumia mifumo yote faafu kuboresha sekta ya kilimo.“Mfumo wa bayoteknolojia ni mojawapo na tutaupiga jeki kutekelezwa nchini,” akasema Dkt Oscar Magenya, mtafiti wa masuala ya kilimo katika wizara.

“Mataifa yote yaliyoimarika kiuchumi na kimaendeleo, yamekumbatia na kuwekeza pakubwa katika Sayansi, teknolojia na ubunifu. Tukiiga nyayo zao, tutaweza kuwa na chakula cha kutosha na salama,” akafafnua afisa huyo.

Australia ni kati ya mataifa yanayoendeleza na kuridhia mfumo wa bayoteknolojia katika kilimo na ufugaji, na Balozi wa nchi hiyo Bw Luke Williams, alisema Kenya ikiukumbatia kikamilifu usalama wa chakula utaangaziwa.

“Kando na kushusha gharama ya uzalishaji, athari za mabadiliko ya tabianchi, wadudu na magonjwa zitapungua,” Bw Wlliams akasema. Kiangazi kinachoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo nchini, athari za mabadiliko ya tabianchi zimetajwa kuchangia pakubwa.

Zaidi ya kaunti 23 hususan zile kame (ASAL), zinaendelea kusakamwa na baa la njaa, mimea ikikauka na mifugo kufariki. Barani Afrika, nchi zilizokumbatia bayoteknolojia ni pamoja na Eswatini, Ethiopia, Kenya, Malawi, Nigeria, Sudan na Afrika Kusini.

Novemba 4 hadi 5, Kenya itaadhimisha miaka 10 baada ya kukumbatia mfumo huu faafu.