Kero ya dimbwi la majitaka karibu na majumba ya makazi mtaani Zimmerman
NA SAMMY WAWERU
SUALA la majitaka katika mtaa wa Zimmerman, Kaunti ya Nairobi limegeuka kuwa kero kuu, maji machafu yakielekea kwenye nyumba za wakazi.
Changamoto hiyo imetokana na miundomsingi mbovu ya mikondo ya majitaka.
Aidha, mkondo mkuu wa majitaka yanayotoka kwenye majengo mengi Zimmerman, umeelekezwa katika dimbwi lililoko katika barabara ya Karii, inayounganisha Thika Superhighway na Kamiti Road.
“Maji machafu sasa yanatukuta kwenye kaya zetu,” Antony Kiragu, mmoja wa wakazi akaambia Taifa Leo akilalamikia hali hiyo.
Kero ya majitaka eneo hilo, inaendelea kushuhudiwa licha ya Shirika la Kuboresha Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) kwa ushirikiano na serikali ya kaunti kufanya ukarabati wa barabara ya Karii.
Wakati wa shughuli hiyo, mtaro mkubwa wa majitaka ulichimbwa na kuwekwa mifereji.
Huku viongozi waliochaguliwa eneo hilo, kuanzia diwani (MCA) wakiendeleza kampeni na siasa kuhifadhi viti vyao, wenyeji wanaomba kero ya majitaka kuangaziwa na kutatuliwa.
“Tunaona magari yao yakipita na vipaza sauti wakiomba kura, kwanza watusuluhishie suala la majitaka,” akahimiza mkazi mwingine.
Miundomsingi duni ya majitaka inatishia usalama wao kiafya, wakihofia mkurupuko wa maradhi yanayohusishwa na uchafu.