Kibaki alishindwa kumng’oa Daniel Moi mamlakani 1992, 1997
NA RICHARD MUNGUTI
JITIHADA za Mwai Kibaki kumng’oa mamlakani Daniel arap Moi baada ya chaguzi kuu za 1992 na 1997 ziligonga mwamba baada ya kesi alizoshtaki kutupiliwa mbali na mahakama ya rufaa.
Majaji wa mahakama kuu na mahakama ya rufaa walitupilia kesi za Kibaki kwa madai “hakumkabidhi mwenyewe (Moi) nakala za kesi hiyo.”
Kupitia kwa mawakili Kihara Mutu (marehemu) na Pheroz Nowrojee, Kibaki aliwasilisha kesi akilalamika hayati Moi hakushinda chaguzi hizo kwa njia halali.
Katika uchguzi wa 1992 hayati Moi aliwashinda wawaniaji urais miongoni mwao hayati Kibaki, Jaramogi Oginga Odinga.
Vile vile Moi aliwashinda tena waliompinga mnamo 1997 kisha wakamshtaki wakidai ushindi wake ulikumbwa na kasoro kadhaa.
Kupitia kwa wakili Mutula Kilonzo (marehemu) mahakama kuu iliombwa itupilie mbali kesi za kupinga ushindi wa hayati Moi.
Wakati wa uchaguzi mkuu wa 1997 Moi alimpiku Kibaki ambaye wakati huo ndiye alikuwa kiongozi wa upinzani.
Moi alishinda uchaguzi huo kwa kuzoa kura 2,445,801 huku Kibaki akiwai kura 1,895,527.
Ijapokuwa Moi alimshinda Kibaki kwa zaidi ya kura 500,000 bado rais huyu watatu kuongoza Kenya aliwasilisha kesi akilalamika uchaguzi huo ulikumbwa na kasoro tele.
Alidai wapiga kura walihongwa na maafisa kutoka tume ya uchaguzi walimpendelea Moi.
Kibaki alidai kutofuatwa kwa sheria za uchaguzi kulimnyima ushindi.
Kesi za uchaguzi dhidi ya Moi zilikuwa changamoto kubwa idara ya mahakama lakini makosa ya Kibaki yalikuwa, aliwasilisha kesi dhidi Moi kama amechelewa kwa siku 17.
Ushindi wa Moi tayari ulikuwa umechapishwa katika Gazeti rasmi la Serikali mnamo Januari 5, 1998.
Kibaki aliwasilisha kesi hiyo mnamo Januari 22, 1998.
Wiki moja baada ya kuwasilisha kesi hiyo Kibaki , aliichapisha kesi hiyo katika Gazeti rasmi la Serikali.
Kibaki alimjulisha aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi (ECK) Samuel Kivuitu (marehemu) kwamba amewashtaki pamoja na Moi na kwamba wachukue nakala za kesi hiyo katika idara ya usajili wa mahakama kuu.
Lakini kesi hiyo iliposikizwa na Majaji Emmanuel O’Kubasu (mstaafu), Mbogholi Msagha na Moijo ole Keiwua (marehemu), Moi aliipinga akisema hakushtakiwa siku 28 baada ya matokeo ya kura za urais kutangazwa.
Majaji hao walitupilia mbali kesi hiyo ya Kibaki.
Alikata rufaa iliyosikilizwa na aliyekuwa Jaji Mkuu Bernard Chunga na majaji wastaafu Riaga Omolo, AB Shah, Abdul A Lakha (marehemu) na Effie Owuor.
Majaji hao waliamua lazima rais akabidhiwe mwenyewe nakala za kesi inayopinga ushindi wake.