Kibaki kuzikwa Jumamosi
NA CECIL ODONGO
RAIS wa tatu wa Kenya Mwai Kibaki aliyefariki Ijumaa, atazikwa Jumamosi ijayo nyumbani kwake Othaya, Kaunti ya Nyeri.
Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i alitangaza Jumamosi kuwa Mzee Kibaki atafanyiwa mazishi ya kiserikali.
Dkt Matiang’i akiwa ameandamana na wanakamati wengine wa mazishi ya kiserikali na familia ya Kibaki katika jumba la Harambee, alisema kuwa kutakuwa na ibada ya kitaifa ya kumuaga Mzee Kibaki katika uwanja wa kimataifa wa Nyayo mnamo Ijumaa.
Kuanzia kesho, Wakenya watakuwa na nafasi ya kumpa Mzee Kibaki heshima zao za mwisho kwenye Majengo ya Bunge ambako mwili wake utalazwa hadi Jumatano.
“Taifa bado lipo katika hali ya maombolezo. Tunaendelea na mikutano na leo (jana Jumamosi) asubuhi tumekutana na familia ya marehemu Mzee Kibaki kuhusu mipango hiyo. Kabla ya mazishi yake Jumamosi, Wakenya na viongozi watampa heshima zao za mwisho katika Majengo ya Bunge kwa siku tatu mfululizo. Tutatoa ratiba ya kina leo ya shughuli zote,” akasema Dkt Matiang’i.
Kwa Wakenya ambao wangependa kutembelea familia ya Mzee Kibaki hasa viongozi na mabalozi, watafanya hivyo mnamo Jumanne na Jumatano katika afisi za marehemu zilizoko Nyari, Nairobi.
Kwa wakazi wa eneobunge la Othaya ambalo Mzee Kibaki aliwakilisha kwa muda wa miaka 39, watatoa rambirambi zao kwa kuandika kwenye kitabu katika afisi ya Hazina ya Ustawi wa Eneobunge hilo kuanzia leo Jumapili. Vitabu hivyo, pia vitakuwa katika afisi za wizara na makao makuu ya kaunti zote 47 ambako Wakenya watafika kuandika rambirambi zao.
“Tuendelee kuombea nchi wakati huu mgumu hasa kwa familia ya Mzee Kibaki ili Mungu awape stahamala, subira na uvumilivu wakati huu wa majonzi. Nasisitiza kuwa Rais Kibaki atapewa mazishi ya heshima ya kitaifa kutokana na huduma alizotoa kwa nchi hii jinsi alivyotangaza Rais Uhuru Kenyatta mnamo Ijumaa,” akaongeza Dkt Matiang’i.
Dkt Matiang’i aliandamana na wanawawe marehemu, Jimmy na Judy Kibaki pamoja na wanachama wengine wa kamati hiyo akiwemo Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua.
Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kifo cha Mzee Kibaki mnamo Ijumaa na kusema kuwa taifa litaendelea kumwomboleza hadi siku ya kuzikwa kwake.