Connect with us

General News

Kijana, 33, aapa kumtoa jasho Omar kumrithi Joho – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kijana, 33, aapa kumtoa jasho Omar kumrithi Joho – Taifa Leo

Kijana, 33, aapa kumtoa jasho Omar kumrithi Joho

Na VALENTINE OBARA

MASHINDANO ya tikiti ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kwa wanasiasa wanaopanga kuwania ugavana Mombasa mwaka ujao, sasa yameanza kushika kasi.

Aliyekuwa Seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, anatarajiwa kupata ushindani kutoka kwa Dkt Mohamed Bahaidar, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya saikolojia.

Wanasiasa wengine wanaosemekana waliwasilisha ombi kutaka kushindania tikiti hiyo, hawajajitokeza wazi.

Baada ya kimya cha muda mrefu, Bw Omar alianzisha ziara zake za kampeni wikendi ambapo alikutana na wakazi wa maeneobunge ya Mvita, Nyali na Kisauni.

Katika ziara hizo, seneta huyo wa zamani alitilia mkazo injili ya UDA kuhusu hitaji la kufufua uchumi wa nchi kwa kustawisha biashara ndogondogo.

“Tuna hakika kuwa mfumo wa kiuchumi wa ‘hasla’ utastawisha biashara za Wakenya walio mashinani na kuwapa uwezo wa kifedha ili nchi ipate ushuru wa kutosha kuimarisha uchumi,” akasema Bw Omar.

Baadhi ya wafuasi wa UDA walikuwa wamepinga azimio la Bw Omar wakitaka Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali ndiye apewe tikiti hiyo. Hata hivyo, Bw Ali alikataa kuwania ugavana.

Ijapokuwa Bw Omar awali alionekana kupigwa jeki katika azimio lake alipoandamana na Naibu Rais William Ruto katika kampeni zake Pwani, Dkt Bahaidar ameapa kumtoa kijasho katika kinyang’anyiro cha kutafuta tikiti ya UDA.

Katika mahojiano na Taifa Leo, msomi huyo aliye na umri wa miaka 33, alisema changamoto zinazokumba wakazi wa Mombasa zinahitaji kiongozi atakayeibuka na mawazo mapya ya kuendeleza jamii.

Alifananisha maisha ya wakazi wa Mombasa wanaotaabika kuwa ya kusikitisha kama yale ya chura aliyekuwa akifurahia joto la maji ndani ya sufuria, lakini maji yalipotokota chura akafa kwa kushindwa kujiokoa.

“Tumefikia kiwango ambapo twategemea maji ya chumvi kukata kiu, biashara zimekufa, shule ziko tele lakini hakuna elimu, na matibabu ni duni. Kuna shida nyingi ambazo tusipotatua hatujui hatima ya watoto wetu. Imefika mahali ambapo hata choo wengine wetu wanalipa,” akasema Dkt Bahaidar.

Alisisitiza kuwa anaamini UDA itaandaa kura ya mchujo kwa njia huru na haki kufuatia ahadi iliyotolewa na Dkt Ruto.

“Kile ambacho Naibu Rais alifanya ni kumshika mkono Sarai (Bw Omar) kwa vile wao ni marafiki na wakati huo hakuwa na mpinzani. Tulihakikishiwa wajumbe wa UDA watapiga kura kuamua atakayepeperusha tikiti ya chama kwa ugavana na tunaamini itafanywa kwa njia ya haki,” akasema.

Kufikia sasa, kiti cha Gavana Hassan Joho kitakachobaki wazi akistaafu ugavana mwaka ujao kimevutia wanasiasa wengine wengi kutoka vyama mbalimbali.

Katika ODM, kiti hicho kinamezewa mate na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir na mfanyabiashara Suleiman Shahbal, ambao wanashindania tikiti ya chama hicho.

Wengine wanaotarajiwa kuwania nafasi hiyo ni Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo wa Chama cha Wiper na aliyekuwa Mbunge wa Nyali, Bw Hezron Awiti wa Vision Democratic Party.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending