Kilio cha mama mwenye mtoto aliye na tatizo la uti wa mgongo
Na SAMMY WAWERU
KATIKA barabara ya Nairobi – Nakuru, eneo la Kamandura ndiko Catherine Minayo, mama wa watoto watano anaishi.
Pembezoni mwa barabara inayopitia Mai Mahiu kuelekea Naivasha, Bi Catherine amepewa makazi na kanisa moja eneo hilo. Ni singo-matha, hali ya upweke aliyojipata baada ya kuachwa na mume wake 2012 alipojifungua mtoto wa tano. Akiwa mama mchangamfu na mkwasi wa ukarimu unapomtembelea, moyoni anauguza majeraha. Mosi, jeraha la kupewa talaka na mume wake kipindi ambacho alimhitaji kwa hisia, hali na mali, wanawe wakiwa wangali wachanga kiumri.
Pili, ni hili jeraha la kifunga mimba wake kuwa na ulemavu, linalomkosesha amani na usingizi. “Nilipojifungua, nilifanyiwa upasuaji (ndiyo Cesarean Section – CS) na ikabainika mwanangu mdogo ana shida ya uti wa mgongo,” Catherine afichua. Ni tatizo ambalo limemuongezea mahangaiko juu ya mahangaiko, akisema amejaribu kutafuta huduma za matibabu bila mafanikio. Anasema kikwazo kikuu ni ukosefu wa fedha.
“Haijakuwa rahisi. Hii miguu yangu unayoiona hapa, imeingia vituo vingi vya afya na hospitali – lengo likiwa mtoto wangu atibiwe aweze kutembea kama wenzake ila sina uwezo,” akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano, kwenye chumba chake eneo la Kamandura akilengwa na machozi kufuatia changamoto anazopitia.
Tatizo la uti wa mgongo husababisha mwathiriwa kutoweza kutembea, wengi wakijipata katika hali hii baada ya kuhusika kwenye ajali. Huishia kutumia kiti chenye magurudumu kuwawezesha kusafiri. Uti wa mgongo unapoathirika, hujiri na uchungu mgongoni, kwenye shingo na vilevile kuathiri utendakazi wa viungo vingine vya mwili.
Bi Catherine Minayo kwenye chumba alichopewa na kanisa moja eneo la Kamandura kuishi…Picha/ SAMMY WAWERU
Kulingana na tovuti ya www.healthline.com, uti wa mgongo ni tatizo hatari katika mwili wa binadamu, linaloweza kuathiri mkondo wa maisha wa mwathiriwa kwa kiasi kikubwa. “Uti wa mgongo umeunganishwa na viungo vingi vya mwili, kuanzia mishipa, ubongo, mgongo wenyewe na hadi karibu na makalio,” mtandao huo unaelezea.
Aidha, uti wa mgongo unawajibika kutuma ‘ujumbe – jumbe’ kutoka bongoni hadi kwenye viungo vingine vyote vya mwili. “Vilevile, hutuma jumbe kutoka viungo vya mwili hadi kwenye ubongo. Uchungu na kushindwa kutembea kwa mwathiriwa hujiri kwa sababu ya jumbe kukosa kusambazwa,” tovuti hiyo inafafanua. Inaendelea kueleza: “Uti wa mgongo unapopata jeraha au majeraha, baadhi ya viungo au vyote vinakosa kufanya kazi. Jeraha karibu na shingo huathiri viungo vingi mwili, ikilinganishwa na karibu na makalio.”
Wengi wa manusura wa ajali wanaojipata kuathirika uti wa mgongo, hutumia maelfu na mamilioni ya pesa kutafuta matibabu. Gharama ya matibabu nchini ingali ghali, licha ya Rais Uhuru Kenyatta kuahidi kuhakikisha kila Mkenya anapata matibabu bora na kwa bei nafuu kabla kukamilisha hatamu yake ya pili na ya mwisho.
Alipochaguliwa 2017, alizindua Ajenda Nne Kuu, mojapo ikiwa utoaji wa huduma za matibabu bora na bei nafuu. Idadi kubwa ya Wakenya hawana uwezo kumudu gharama ya afya. Rais Kenyatta aidha amekuwa akihimiza wananchi kuchukua bima ya afya, kupitia mpango wa Afya Bora Kwa Wote (UHC). Kwa Catherine anaomba wahisani na wasamaria wema kujitokeza, kumpa tabasamu tena maishani na zaidi ya yote kumsaidia kupata matibabu.
“Kwa unyenyekevu, ninaomba wasamaria wema wanisaidie mwanangu apate matibabu,” Catherine anaomba. Hana ajira, hutegemea vibarua vya hapa na pale vikiwemo kulimia watu mashamba na kufua nguo. Isitoshe, hali ya mwanawe anapozidiwa na uchungu humshinikiza kusalia naye nyumbani, hivyo basi kukosa kuenda vibarua ambavyo kuvipata ni nadra.
“Kukithi familia yangu riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi imekuwa ngumu. Ninajikaza kulipia watoto karo,” aelezea, akiwa mwingi wa matumaini “ipo siku mambo yatageuka na kuwa bora”. Anasema watoto wake wana hamu kukata kiu cha masomo. “Urithi mkuu kwao kutoka kwangu ni kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu ya kimsingi, yakiwemo chakula, afya na elimu.”
Na kwa yeyote aliye na kazi, Catherine Minayo anasema yuko tayari kuifanya angalau aweze kusukuma gurudumu la maisha. Hali ya chumba anachoishi, inaashiria mahangaiko chungu nzima anayopitia.
Bi Catherine Minayo na wanawe, nyumbani kwake eneo la Kamandura, katika barabara ya kuelekea Mai Mahiu….Picha/ SAMMY WAWERU