Connect with us

General News

Kinundu mmoja anaharibia watu futari zao kwa mavamizi ya chakula – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kinundu mmoja anaharibia watu futari zao kwa mavamizi ya chakula – Taifa Leo

HUKU USWAHILINI: Kinundu mmoja anaharibia watu futari zao kwa mavamizi ya chakula

NA SIZARINA HAMISI

KAMA ilivyo sehemu nyingine ulimwenguni, huku kwetu Uswahili tupo katika mfungo wa mwezi mtukufu, kwa wale ambao imani inahusu jambo hili muhimu la kidini.

Na hii saumu nayo huwa inakuja na jinsi zake tofauti, wale tunaoishi huku kwetu tunaelewa.

Kawaida muda huu waumini huwa tunatilia maanani suala zima la futari na hata daku.

Nako huku kwetu suala la futari huwa linakuja kwa hatua zake, zilizo njema kabisa. Hivyo ni kawaida kutupata huku kwetu tukitayarisha futari kuanzia mchana, kwani huwa inahusu mchanganyiko wa aina mbalimbali ya vyakula pamoja na mapishi pia.

Lakini pia baada ya futari huwa tunakuwa na daku, ambayo huliwa usiku kabla ya kuanza mfungo wa siku inayofuata. Mfungo huu sio wa chakula pekee, bali unahusu pia mambo mbalimbali ambayo tunaweza kujinyima kipindi hiki.

Kama kawaida hawakosekani wale vivuruge ambao wakati mwingine nia na madhumuni inaweza ikawa sio mbaya, lakini vitendo vyao vikakukwaza ukahisi kama utaharibiwa saumu yako.

Hawa ni wale wavamizi wa futari waliokubuhu. Kawaida huku kwetu unapowadia muda wa kufuturu, tuna kawaida ya kutandika mkeka upenuni na kuketi na kujumuika futari kwa pamoja.

Na vivyo hivyo, kuna huyu jamaa ambaye siku sio nyingi tunaona tutamweleza ukweli kwa hii tabia yake isiyokuwa na heshima.

Kinundu huyu wa mtaani, amekuwa na mazoea ya kujikaribisha muda ule ambao watu tunafungulia na bora angejikaribisha kwa heshima, bali hufanya hivyo kwa mtindo wa uvamizi.

Uvamizi wake unatutia mashaka kwani, akikuta watu tumejumuika kupata mlo, hujiketisha chini bila kunawa na kuweka mkono wake mkubwa mfano wa sepetu kwenye chakula na kuchota matonge makubwa ya chakula kama anakimbizwa. Na safari yake haishii hapo, akishachota kiasi cha chakula anachotaka, anaondoka bila kuaga na kwenda kuvamia tena mlo wa wengine mtaa wa pili.

Hatuna ubaya kujumuika na wenzetu wakati wa mlo huu muhimu, lakini huku kwetu kuna watu tabia zao ni zaidi ya kushangaza.

Ndiposa watu hapa mtaani tumeamua tumweleze, kwani siku chache zilizopita kuna waliougua tumbo na tunahisi ni mikono yake huyu Kinundu ambayo huvamia chakula bila kunawa.

Iwapo bado unashangaa, huku kwetu tunakula kwa kutumia mikono yetu, suala la vijiko na visu huwa ni anasa tena hatujazoea.

Na ndio maana kabla hatujamaliza mfungo, tunataka tumweleze ukweli huyu Kinundu kabla hajatuletea majanga zaidi ya kuugua matumbo.

[email protected]