Connect with us

General News

Kivumbi ndani ya Azimio jijini – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kivumbi ndani ya Azimio jijini – Taifa Leo

Kivumbi ndani ya Azimio jijini

Na COLLINS OMULO

USHINDANI mkali unatarajiwa kushuhudiwa baina ya wawaniaji mbalimbali ambao wametangaza azma za kuwania nyadhifa tofauti za kisiasa katika Kaunti ya Nairobi kupitia vuguvugu la Azimio la Umoja.

Hili linajiri baada ya kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kutangaza kuwa vyama washirika katika vuguvugu hilo, vitafanya zoezi la mchujo kwa pamoja.

Bw Odinga ndiye mgombea urais wa vuguvugu hilo kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti.

Ushindani huo unatarajiwa kujitokeza kwenye nyadhifa za ugavana, useneta na nafasi ya Mwakilishi wa Kike.

Nyadhifa hizo ndizo zimewavutia wawaniaji wengi zaidi ikilinganishwa na zile zingine kama ubunge na udiwani.

Tayari, mbunge wa Westlands, Tim Wanyonyi, ametangaza azma ya kuwania ugavana akilenga kukabiliana na Gavana Anne Kananu, anayetarajiwa kutetea wadhifa huo.

Mfanyabiashara Agnes Kagure vile vile ametangaza rasmi azma ya kuwania nafasi hiyo.

Bi Kagure anatarajiwa kukabiliana na kiongozi wa Chama cha Wenye Biashara na Viwanda (KNCCI), Bw Richard Ngatia.

Kwenye kinyang’anyiro cha useneta, Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna anatarajiwa kukabiliana na Mbunge Maalum Maina Kamanda, mwanamuziki Roy Smith Mwatia (maarufu kama Rufftone) na mfanyabiashara George Kamano.

Kwenye kinyang’anyiro cha nafasi ya Mwakilishi wa Kike, Bi Esther Passaris anatarajiwa kumenyana na Naibu Waziri wa Jinsia, Bi Rachel Shebesh na Bi Wangui Ng’ang’a, aliyehudumu kama diwani hapo awali.

Wiki iliyopita, Bi Passaris alizua hisia alipopendekeza kuwa vuguvugu hilo linapaswa kuandaa tafiti kubaini mgombea maarufu zaidi miongoni mwa wale wote ambao wamejitokeza kuwania nafasi fulani.

“Wapigakura wanapaswa kupewa nafasi kuamua mgombea wanayempendelea zaidi kupitia kura za maoni,” akasema Bi Passaris.

Vile vile, alidai kuna njama za vyama vya ODM na Jubilee kumsimamisha mgombea tofauti kuwania ugavana, hivyo kumwacha nje Bw Wanyonyi.

“Kuna wale wanaoshikilia kuwa lazima nafasi hii ishikiliwe na jamii moja. Kwangu, huo ni ukabila ambao unakinzana na kauli ya umoja wanayoendesha Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta,” akasema.

Bi Passaris alikuwa akijibu tetesi kwamba huenda Bw Ngatia ndiye mwaniaji anayependekezwa na vyama vya Jubilee na ODM.

“Kati ya wabunge wote katika Kaunti ya Nairobi, nimeona kazi ambayo ameifanya Bw Wanyonyi. Amewatumikia wenyeji wa Westlands vizuri. Vivyo hivyo, anataka kuwafanyia kazi wakazi wa kaunti hii,” akasema.

Hata hivyo, Bi Ng’ang’a alisema Bi Passaris anatoa kauli hiyo kwani anahofia huenda akashindwa kwenye zoezi la mchujo.

Alisema zoezi hilo haliwezi kuendeshwa kwa kutegemea “tafiti ambazo haziaminiki.”

“Bi Passaris hapaswi kuhofishwa na jinsi zoezi la mchujo litaendeshwa katika vuguvugu hili. Anapaswa kuwaeleza wakazi wa Nairobi kuhusu aliyowafanyia kwa muda wa miaka mitano iliyopita,” akasema.