Connect with us

General News

Knut yaongeza umri wa kustaafu kutoka miaka 60 hadi 65 – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Knut yaongeza umri wa kustaafu kutoka miaka 60 hadi 65 – Taifa Leo

Knut yaongeza umri wa kustaafu kutoka miaka 60 hadi 65

VITALIS KIMUTAI na CHARLES WASONGA

WANACHAMA wa Baraza la Ushauri la Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut), wameamua kuongeza umri wa kustaafu kwa maafisa wa chama hicho kutoka miaka 60 hadi 65.

Hatua hiyo imetoa afueni kwa mamia ya maafisa wa Knut katika ngazi za kitaifa na matawi ambao muda wao wa kuhudumu ulikaribia kukamilika kwani sasa wataendelea kuhudumu kwa miaka mitano zaidi.

Baraza hilo pia lilipitisha uamuzi kwamba wabunge, maseneta na madiwani waliochaguliwa wakome kushikilia nyadhifa katika chama hicho cha Knut.

Kulingana na uamuzi huo ambao ulipitishwa katika mkutano wa baraza hilo la Knut lililofanyika katika uwanja wa Nyayo, Nairobi, maafisa wa chama hicho pia wamepigwa marufuku kushikilia nyadhifa za mawaziri katika serikali za kaunti (CEC).

“Jumla ya wanachama 510 wa baraza la ushauri (NAC) wamepitisha mageuzi katika katiba yetu ili kufutilia mbali matawi 63 nchini na kudumisha matawi 47 pekee. Hatua hii inaafiki katiba ya sasa inayotambua serikali za kaunti 47 pekee,” akasema Katibu Mkuu Collins Oyuu.

Bw Oyuu alipuuzilia mbali madai kuwa kubadilishwa kwa umri wa kustaafu ni njama ya maafisa wakuu wa Knut kuendeleza muda wao wa kusalia afisini ikizingatiwa kuwa baadhi yao wamekaribia kufikisha umri wa miaka 60.

Kulingana na kanuni za Tume ya Huduma za Walimu (TSC) walimu wanapaswa kustaafu wakifikisha umri wa miaka 60.

“Hayo ni masuala madogo. Hatuna nia ya kusalia afisini kwa miaka mingi kupita kiasi. Kile ambacho tumefanya ni kuoanisha shughuli zetu na taratibu bora ulimwenguni ili kurejesha hadhi ya chama chetu cha Knut katika ukanda huu wa Afrika,” Bw Oyuu akasema.

Mageuzi mengine makuu katika Katiba hiyo mpya ni kwamba wanachama wa Knut ambao sio wanachama wa baraza hilo la ushauri watazuiwa kuwania nyadhifa za juu katika chama hicho cha kutetea masilahi ya walimu.

Wanachama wa NAC ni pamoja katibu wa tawi, mwenyekiti, mweka hazina a mwakilishi wa wanawake.

Manaibu wa maafisa hawa pamoja na wanachama wa kamati za matawi sio wanachama wa baraza hili na hivyo, hawaruhusiwi kuwania nyadhifa za uongozi katika ngazi ya kitaifa.

Wanachama wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) Kamati Shikilizi ya Kitaifa (NSC) na Wadhamini wa Kitaifa sasa watachaguliwa miongoni mwa wanachama wa NAC katika chaguzi zijazo.

Wanachama wa NEC sasa wataanzisha mpango wa utekelezaji wa mageuzi hayo ya kikatiba huku Kongamano la Wajumbe wa Knut (ADC) likitarajiwa kufanyika katikati mwa mwaka ujao.

Mikutano ya matawi ya Knut (AGMs) itaanza kufanyika kote nchini kuanzia mwezi wa Februari mwaka ujao. Hiyo ndio itakuwa mikutano ya kwanza kufanyika tangu Bw Oyuu na maafisa wake wa kitaifa, walipoingia mamlakani.

Wakati huohuo, mvutano kati ya Bw Oyuu na mtangulizi wake, Bw Wilson Sossion haujaisha kwani wawili hao wameendelea kulumbana kuhusu masuala ya Knut.

“Mageuzi tunayofanya yanaungwa mkono na maafisa wote wa zamani wa Knut kwa sababu yanalenga kuvutia wanachama wengi kujiunga nasi. Lakini Bw Sossion pekee ndiye anaendelea kupinga mageuzi hayo,” akasema Bw Oyuu.

Katibu huyo Mkuu alisema hayo baada ya Bw Sossion ambaye ni mbunge maalum wa ODM, kudai maafisa wa Knut waliongeza umri wa kustaafu ili waendelee kusalia mamlakani kuzidi muda uliowekwa.