Connect with us

General News

Kumekucha! Taifa Leo mpya mambo mapya – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kumekucha! Taifa Leo mpya mambo mapya – Taifa Leo

TAHARIRI: Kumekucha! Taifa Leo mpya mambo mapya

KITENGO CHA UHARIRI

MABADILIKO NI sehemu ya maisha na hayawezi kuepukika. Kuna msemo kuwa usipokubali kubadilika, mabadiliko yatakubadilisha. Na ukikataa kabisa, basi utaangamia.

Katika kutambua umuhimu wa mabadiliko, leo ni siku mpya kwa uanahabari nchini, gazeti la Taifa Leo linapopata sura mpya.Gazeti hili ambalo lilianzishwa miaka 63 iliyopita, limekuwa sehemu ya historia ya Kenya.

Limerekodi matukio makuu ambayo yameipa Jamhuri ya Kenya sura yake ya sasa na mustakabali wa siku zijazo.Taifa Leo ni gazeti la kipekee. Ndilo la pekee kitaifa linalochapishwa kila siku kwa lugha ya Kiswahili, ambayo ndiyo lugha ya taifa na rasmi ya Kenya.

Hatua hii imefanya gazeti hili kutambuliwa na wengi, si tu kama chombo muhimu cha habari, bali pia sehemu ya utaifa wa Wakenya.Sura mpya ya gazeti hili imetokana na haja ya kuendeleza maono ya waasisi wake, ambao walitaka chombo cha mawasiliano ambacho kingetoa jukwaa kwa Mkenya kujieleza na kufahamishwa yaliyo muhimu katika jitihada zake za kujikomboa kutokana na ukoloni.

Baada ya kutekeleza wajibu mkuu katika kupatikana kwa uhuru, gazeti hili limekuwa likibadilika ili kuendelea kuwa chombo cha ukombozi wa Mkenya kutokana na changamoto zinazochipuka kila uchao.

Taifa Leo lenye sura mpya, kwanza linatambua umuhimu wa kujenga uzalendo wa Mwafrika kupitia kwa lugha yake asilia ya Kiswahili. Katika kuafikia ndoto hii, gazeti hili jipya limeweka mikakati ya kuwa kitovu cha kupigia debe na kufanikisha matumizi ya Kiswahili hapa Kenya na kote duniani.

Gazeti hili kama sauti ya mwananchi, pia limeundwa kuendelea kutetea maslahi ya Wakenya kwa ujasiri na uhuru, ili kuhakikisha walio madarakani ama katika nafasi za kutumikia umma, wanatimiza majukumu yao kwa mwananchi.

Na kwamba wanaheshimu haki za kila mmoja kwa mujibu wa Katiba.Taifa Leo jipya pia linaongeza thamani katika maisha ya wasomaji, kupitia habari na makala ya kitaalamu na yaliyofanyiwa utafiti wa kina.

Mabadiliko mengine ni kwamba, kwa mara ya kwanza, wakazi wa Pwani watakuwa na gazeti lao, linaloangazia masuala yanayowahusu kiuchumi, kijamii na kisiasa.Katika sekta ya elimu, kuanzia sasa gazeti hili limegeuzwa kuwa mwenzi wa mwalimu na mwanafunzi kwani limerutubishwa kwa makala kemkem ya Lugha, Fasihi na Elimu.

Jua linapochomoza huwa kumekucha. Ujumbe kwa kila mmoja ni kuwa, hii ni fursa mpya ya mafanikio maishani mwake. Leo kumekucha Kenya na duniani kwa gazeti la Taifa Leo jipya.