Connect with us

General News

Kuna haja ya kuanza kutahini Kiswahili kama lugha ya kigeni – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kuna haja ya kuanza kutahini Kiswahili kama lugha ya kigeni – Taifa Leo

NGUVU ZA HOJA: Kuna haja ya kuanza kutahini Kiswahili kama lugha ya kigeni

NA PROF IRIBE MWANGI

KUTOKANA na tajriba yangu, ni tabia ya kila lugha iliyokua na kuenea kuwa na mjarabu kwa wageni wanaoingia katika taifa tumizi. Mjarabu huo kwa kawaida hutahini stadi nne muhimu za lugha: kusoma, kusikiliza, kuandika na kuzungumza.

Katika nchi zitumiazo Kiingereza kama lugha ya kwanza, kila anayeazimia kupata elimu na ambaye Kiingereza ni lugha ya kigeni kwake, hulazimika kupita mtihani ujulikanao kama, TOEFL (Test of English as a Foreign Language).

Wanaoenda Ujerumani ni sharti wapite TELC ilhali wanaotamani kusomea Ufaransa ni sharti wapite TEF.

Kupita kwa mitihani hii kunatoa hakikisho kwamba mgeni anayefika katika nchi husika ataweza kuwasiliana, kusoma na kufanya mambo yake ya kibinafsi bila kuwasumbua wengine na bila kutatizika sana.

Mitihani hii imesawazishwa na huwa sawa kwa wote.

Ninapendekeza kwamba Kiswahili kama lugha inayokua na kuenea kwa kasi pia kiwe na mtihani wa aina hiyo.

Kila anayefika katika mataifa ya Afrika Mashariki anafaa kuwa na uwezo wa kusoma, kuelewa, kuandika na kuzungumza Kiswahili.

Mtihani huo unafaa kusawazishwa na mataifa yote husika na uwe mmoja.

Napendekeza uitwe MKILUKI (Mjarabu wa Kiswahili kama Lugha ya Kigeni).

Mjarabu huo unafaa kutahini stadi nne zilizotajwa.

Mbali na kuleta mapato kwa nchi kupitia walimu na watahini, mjarabu huo utakuwa muhimu katika kusambaza Kiswahili na kukipa mashiko.

Pia, utakuza uandishi wa Kiswahili pamoja na kufanikisha mawasiliano kwa kukitumia katika nyanja mbalimbali kama vile biashara na elimu. Hili ni wazo ambalo wakati wake umefika na linafaa.