Connect with us

General News

Kura za Wapwani ‘zisinywe maji’ 2022, eneo lina uwezo kuamua rais – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kura za Wapwani ‘zisinywe maji’ 2022, eneo lina uwezo kuamua rais – Taifa Leo

VALENTINE OBARA: Kura za Wapwani ‘zisinywe maji’ 2022, eneo lina uwezo kuamua rais

Na VALENTINE OBARA

ENEO LA Pwani ni miongoni mwa yale ambayo kura za raia wake hupiganiwa sana na wagombeaji urais katika kila mwaka wa uchaguzi.

Mwaka huu, kaunti sita za ukanda wa Pwani zinatarajiwa kuwa na takriban wapigakura milioni mbili kwa jumla.Hakika, hii ni idadi ya kura ambayo inaweza kumfanya mgombeaji urais atimize au akose kutimiza sharti la asilimia 50+1 la kura ili atangazwe mshindi uchaguzini.

Huu ni msimu mwingine tena wa kampeni za kisiasa, na eneo hili tayari limeshuhudia mihemko si haba licha ya kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haijapuliza rasmi kipenga cha kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.

Hata hivyo, kila mara baada ya uchaguzi, wakazi na baadhi ya viongozi katika eneo hili hulalamika sana kuhusu kutengwa na serikali ya kitaifa.

Kupuuzwa

Hii ni kutokana na kuwa masuala mengi ambayo yametatiza Wapwani tangu jadi bado huendelea kushuhudiwa.Mifano ni kama vile ukosefu wa nafasi za kutosha za ajira ikilinganishwa na maeneo mengine nchini, uhaba wa maji safi miferejini nyumbani, mizozo kuhusu umiliki wa ardhi miongoni mwa masuala mengine.

Wakati wa kampeni, imekuwa kama ibada kwa vigogo wa kisiasa wanaomezea mate urais kukutana na makundi ya wanasiasa au hata viongozi wa kijamii na kidini ili kujadili kuhusu mwelekeo unaofaa kuchukuliwa kutatua matatizo haya.

Ahadi tele hutolewa huku makubaliano yakipitishwa kati ya wawaniaji urais na viongozi wa Pwani kuhusu jinsi eneo hili litaokolewa.Mbali na kura ya urais, ugatuzi ulileta hali ambapo wawaniaji ubunge na udiwani pia hutaka kuwa karibu na gavana aliye mamlakani ili maeneo yao yapokee miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali za kaunti.

Kinachosikitisha ni kuwa, haya yote husahaulika punde baada ya uchaguzi kwani wakazi wa Pwani hurejea katika matatizo yao na kusubiri tena miaka mingine mitano ili waletewe ahadi zile zile za awali. Pwani ina uwezo wa kujifufua kiuchumi kwa kiwango ambacho kitaleta nafuu kwa wakazi.

Tatizo lililopo ni kuwa, kufikia sasa, ni viongozi wachache mno ambao wamejitolea kuchapa kazi kwa manufaa ya raia kwani wengine wengi huamua kujali tu mahitaji yao ya kibinafsi pamoja na yale ya jamaa zao na wandani.

Wakati raia wanapoacha shughuli zao muhimu kuenda kupanga foleni ya kupiga kura, wengi wao huamini kuwa wanaenda kuchagua viongozi ambao watatwikwa jukumu la kuwawakilisha katika mabaraza tofauti ya kufanyia maamuzi ambayo yatanufaisha jamii.

Mioyo yao huvunjika kila wakati maazimio yao yanapokosa kutimizwa, na huishi kuona watoto na wajukuu wao wakipitia changamoto zile zile ambazo wao waliahidiwa zingetatuliwa miongo iliyopita. Raia wanafaa kutambua kuwa, umuhimu wao katika kufanya maamuzi ya uongozi huwa hauko tu wakati wa kupiga kura.

Ni muhimu kwao kushiriki katika kila hatua ya uchaguzi ikiwemo ndani ya vyama vya kisiasa ndipo hata wanapoamua kuchagua kiongozi kwa misingi ya umaarufu wa chama, jinsi ilivyo desturi katika maeneo mengi ya nchi, kuwe kuna mgombeaji anayeweza kuwaletea mabadiliko wanayotamani.

Valentine Obara ni mwanahabari wa Kampuni ya Nation Media Group