Connect with us

General News

Kwale yamulikwa kwa visa vya ugaidi Pwani – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kwale yamulikwa kwa visa vya ugaidi Pwani – Taifa Leo

Kwale yamulikwa kwa visa vya ugaidi Pwani

NA SIAGO CECE

MAAFISA wa usalama wametaja eneo la Kwale kuwa chimbuko la visa vya ugaidi katika eneo la Pwani, huku machifu wawili wakienda mafichoni baada ya kutishiwa maisha yao.

Mshirikishi wa usalama eneo la Pwani, Bw John Elungata, alisema kaunti hiyo kwa sasa ina vituo viwili vya magaidi ambapo watu hufunzwa itikadi kali kabla kwenda kutekeleza mashambulio nchini na nje ya nchi.

Bw Elungata pia alisema kaunti hiyo imegeuka ngome ya kusafirisha watu wenye itikadi za kigaidi nchini Msumbiji na Somalia, kwani wengi wa wale wanaokamatwa katika nchi hizo ni wazaliwa wa Kwale.

“Mara kwa mara polisi wanapochukua hatua huwa wanalaumiwa na mashirika ya haki za binadamu. Magaidi hao huwa ni watu hatari kwani huwa tunawapata wakiwa na mabomu. Wao ni tishio kwa maendeleo ya uchumi na kijamii katika nchi hii na utalii utaathirika ikiwa kuna vituo hivi hapa karibu,” akasema.

Alikuwa akizungumza katika hoteli ya Jacaranda Beach iliyo Diani wakati wa kongamano kuhusu kuzuia na kukabiliana na itikadi za kigaidi.

Kulingana na Bw Elungata, serikali ingali inawachunguza washukiwa kadhaa katika kaunti hiyo ambao wanahusishwa na ugaidi.

Akitoa mfano wa Kaunti ya Lamu ambapo watu 15 waliuawa majuzi, alieleza kuwa mashambulio hupangwa na vijana wa humu nchini wala si wa kutoka nchi za nje ilivyokuwa zamani.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na maafisa wa usalama, serikali, watafiti na mashirika ya kutetea haki za binadamu kutoka kaunti za Kwale, Nakuru na Isiolo.

Kwa upande wake, Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya, alisema kaunti hiyo inafanya juhudi zikiwemo utafiti ili kukabiliana na ugaidi katika eneo hilo.

“Ikiwa bado tuna vituo viwili vya ugaidi, hilo ni jambo ambalo tunahitaji kuangalia. Nina hakika watafiti wataongoza tafiti ili tujue nini zaidi tunaweza kufanya katika hali hiyo,” alisema.

Aliongeza kuwa serikali yake inaangalia namna ya kutoa fursa kwa vijana ili wasijiunge na makundi ya ugaidi.